Mwanza. Ukatili dhidi ya wanawake unaendelea kuwa moja ya changamoto kubwa na sugu duniani, huku takwimu mpya za ripoti ya Shirika la Afya Duniani (WHO) na waathirika wake, zikionesha kuwa kwa miongo miwili jitihada za kukomesha tatizo hilo hazijazaa matunda ya kutosha.
Kwa mujibu wa ripoti hiyo, karibu mwanamke mmoja kati ya watatu duniani, sawa na wanawake milioni 840, amewahi kupitia ukatili wa kimwili au kingono uliofanywa na mwenza wake. Katika kipindi cha mwaka mmoja uliopita pekee, wanawake milioni 316 walikumbwa na ukatili wa aina hiyo.
Ripoti inaonesha kuwa kiwango cha ukatili kimeendelea kushikilia kasi ile ile, kwani kwa miaka 20 iliyopita kumekuwa na kupungua kwa wastani wa asilimia 0.2 tu kwa mwaka, kiwango kinachotajwa kuwa kidogo na kisichoweza kuleta mabadiliko ya haraka.
Utafiti wa ripoti hiyo uliotathmini takwimu kati ya mwaka 2000 na 2023 kutoka nchi 168, ni wa kwanza wa WHO kujumlisha pia ukatili wa kingono unaofanywa na watu wasiokuwa wenza ambapo zaidi ya wanawake milioni 263 wameripoti kukumbwa na ukatili huo tangu wakiwa na umri wa miaka 15.
Licha ya kuongezeka kwa mbinu za kuzuia ukatili, ripoti inaonya kuwa ufadhili kwa programu za mapambano umeshuka kwa kiwango cha kutisha. Mwaka 2022, ni asilimia 0.2 tu ya misaada ya kimataifa ilielekezwa kwenye programu za kuzuia ukatili dhidi ya wanawake, na hali imeripotiwa kuwa mbaya zaidi mwaka 2025.
Ripoti inaonesha kuwa ukatili huanza mapema, ambapo wasichana milioni 12.5 wenye umri wa miaka 15–19 wamepitia ukatili wa kimwili au kingono ndani ya mwaka uliopita.
Bara la Oceania (bila kujumuisha Australia na New Zealand) linaongoza kwa matukio ya ukatili wa wenza kwa kiwango cha asilimia 38, ambacho ni mara tatu ya wastani wa dunia unaokadiriwa kufikia asilimia 11.
Tanzania nayo haijaepuka tatizo hili. Ripoti mbalimbali zinaonesha kuwa zaidi ya asilimia 40 ya wanawake wenye umri wa miaka 15–49 wamepitia ukatili wa kimwili, huku asilimia 17 wakikumbwa na ukatili wa kingono.
Takribani asilimia 44 ya wanawake wamewahi kukumbwa na ukatili wa wenza wao angalau mara moja maishani.
Kwa mujibu wa ripoti ya taasisi za kijamii na usawa wa kijinsia (SIGI), asilimia 23 ya wanawake wenye wenza waliripoti ukatili ndani ya mwaka uliopita, huku asilimia 48 wakikiri kukumbwa na ukatili maishani.
Takwimu kutoka. Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC) zinaonesha kuwa zaidi ya matukio 20,000 ya ukatili huripotiwa kila mwaka, ingawa wataalamu wanaamini kuwa idadi hiyo ni sehemu ndogo ya uhalisia kutokana na wengi kutoripoti.
Mila kandamizi, imani potofu, changamoto za kiuchumi na ukosefu wa nguvu ya maamuzi kwa wanawake zinatajwa kuwa miongoni mwa vyanzo vikuu vinavyoendeleza tatizo hili nchini.
Mratibu wa Mradi wa Vijana Elimu, Malezi na Ajira (VEMA) wa Shirika la Plan International, Gadiely Kayanda, anataja kutowajumuisha wanaume ipasavyo katika programu za kuzuia ukatili kama moja ya changamoto zinazorudisha nyuma juhudi za kupunguza ukatili.
“Ushirikishwaji wa wanaume ni nguzo muhimu sana katika kupunguza ukatili kwa wanawake… Nadhani kinachokwamisha juhudi hizo ni uwekezaji mkubwa katika kuwajengea uwezo wanawake/wasichana huku hatuwajumuishi wanaume katika juhudi hizo kwa kiasi cha kutosha,” anasema.
Kwa upande wake, Mkuu wa Programu wa Shirika la WoteSawa, Demitila Faustine, anasema maendeleo ya teknolojia yamezidi kuongeza misuguano ya kifamilia, hasa pale matumizi yasiyo sahihi yanapoathiri malezi.
“Kumekuwa na malalamiko kwenye kesi za ukatili tunazopokea. Kinamama badala ya kutimiza majukumu ya malezi, muda mwingi wanakuwa kwenye mitandao. Mwisho wa siku wanajikuta wakiingia kwenye migogoro ya kifamilia inayopelekea kupigwa,” anasema.
Anaongeza kuwa ugumu wa maisha na gharama za familia pia mara nyingi husababisha migogoro inayoishia kwenye ukatili.
“Mfano kwenye programu tulizofanya vijijini… tuligundua bado kuna imani potofu. Mazao yakivunwa yanaonekana ya baba, na mama anabaki bila haki. Hapo ndipo ukatili wa kiuchumi na hata vipigo vinapoibuka,” anasema.
Anashauri kuimarishwa kwa elimu ya jamii kuhusu matumizi sahihi ya teknolojia, malezi, usawa wa kijinsia na madhara ya ukatili ili kuondoa mizizi ya tatizo.
Naye Mwenyekiti wa Mashujaa wa Kupinga Ukatili wa Kijinsia Mkoa wa Mwanza (SMAUJATA), Gasto Didas, anasema mapambano haya yanakwamishwa na kukosekana kwa mshikamano kati ya wadau.
“Wadau wanaosaidia kupinga ukatili hatuna sauti moja… Tusipokuwa na mshikamano, ukatili utaendelea kushamili,” anasema.
Anaeleza kuwa mara nyingine watenda ukatili hujipenyeza kwa watoa haki na kujilinda kupitia njia za rushwa.
“Mwathirika akifika kwa watoa haki halafu wanaanza kumlinda mtuhumiwa, lazima kazi iwe ngumu,” anasema Didas.
Anashauri vyombo vya utoaji haki kufanya kazi kwa uwazi, bila upendeleo, na kuongeza umoja wa wadau chini ya Mpango wa Taifa wa Kudhibiti na Kupambana na Ukatili dhidi ya Wanawake na Watoto (MTAKUWWA). Aidha, anasisitiza kuwa wananchi wana jukumu la kutoa taarifa za ukatili mara tu zinapotokea.
WHO na wadau wake wanatoa wito kwa Serikali duniani kuongeza ufadhili, kuboresha mifumo ya ukusanyaji takwimu, kuimarisha huduma rafiki kwa waathiriwa na kutekeleza sheria zinazolinda wanawake.
Mkurugenzi Mkuu wa WHO, Dk Tedros Ghebreyesus, anasema:
“Ukatili dhidi ya wanawake ni dhuluma ya muda mrefu katika historia ya binadamu, na bado hatujawekeza vya kutosha kukomesha tatizo hili. Dunia haiwezi kuwa salama wakati nusu ya watu wake wanaishi kwa hofu.”
Mashirika ya Umoja wa Mataifa (UN) yanasisitiza kuwa mabadiliko yanawezekana endapo kutakuwa na uongozi thabiti na uwekezaji wa kutosha.
Kwa sasa, ripoti inaonesha dunia haijapiga hatua kubwa, lakini bado kuna nafasi ya kubadilisha mwenendo endapo juhudi zitaongezwa na kila kundi, hasa wanaume litashirikishwa kikamilifu katika mapambano haya.