Serikali yahoji wakimbizi 52 Kigoma, M23 ikidhibiti Uvira

Dar es Salaam. Wakati kikundi cha waasi wa M23 kutoka Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) kikiudhibiti mji wa Uvira uliopakana na Tanzania, wakimbizi 52 wameingia Mkoa wa Kigoma, ambako kwa sasa wanaendelea kuhojiwa na vyombo vya usalama.

Uvira, mji unaodhibitiwa na waasi wa M23, ni makao makuu ya Mkoa wa Kivu ya Kusini. Mji huo upo mashariki mwa nchi hiyo na unapakana na Tanzania kupitia Ziwa Tanganyika.

Kutoka Uvira hadi kuingia Mkoa wa Kigoma ni umbali mfupi, ambapo nauli ya usafiri ni takribani Sh15, 000 kwa njia ya maji.

Akizungumza na Mwananchi, leo Desemba 14, 2025, Mkuu wa Mkoa wa Kigoma, Balozi Simon Sirro amesema mkoa huo umejipanga kukabiliana na changamoto zozote za kiusalama.

Sirro amesema hatua za ulinzi na ufuatiliaji zimeimarishwa katika maeneo ya mipakani, hususan kupitia Ziwa Tanganyika, ili kuhakikisha usalama wa wananchi unaendelea kudhibitiwa huku akieleza wanawahoji wakimbizi 52 waliokimbia machafuko hayo.

Amesema maandalizi yalianza mapema mara baada ya kupokea taarifa za kudhibitiwa kwa Uvira na Serikali ilichukua hatua kwa kushirikiana na Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Wakimbizi (UNHCR).

“Tumejipanga tangu mwanzo. Tunapakana na DRC kwa maji kupitia Ziwa Tanganyika na tayari tulishafanya mazungumzo na UNHCR,” amesema Sirro ambaye ni IGP mstaafu.

Ameeleza kuwa vyombo vya ulinzi na usalama, ikiwemo Jeshi la Polisi, vimeimarishwa na vinaendelea kufanya doria za muda wote, zikiwemo doria za kuzuia uhalifu na unyang’anyi ziwani.

Sirro amesema mkoa umepokea wakimbizi 52 kutoka DRC, ambao kwa sasa wanaendelea kufanyiwa mahojiano ili kubaini uhalali wao kabla ya kukabidhiwa UNHCR kwa ajili ya kupelekwa kwenye makambi rasmi ya wakimbizi.

“Tunaendelea kuwahoji ili kubaini kama ni wakimbizi halali kabla ya kuchukuliwa hatua zaidi,” amesema.

Ameongeza kuwa Serikali inaendelea kuchukua tahadhari kutokana na uwezekano wa baadhi ya watu kuingia nchini wakiwa na silaha kwa kujichanganya na raia wa kawaida.

Akizungumzia hali ya usalama kwa ujumla, Sirro amesema Mkoa wa Kigoma uko shwari na ametoa maelekezo kwa kamati za ulinzi na usalama kuanzia ngazi ya kijiji, kata hadi mkoa kuhakikisha zinatekeleza wajibu wao ipasavyo.

“Wananchi wawe macho na watoe taarifa mara moja wanapoona mgeni au jambo lisilo la kawaida. Ulinzi na usalama ni jukumu la kila Mtanzania,” amesema Sirro.

Amesema mkoa utaendelea kuchukua hatua zote muhimu kuhakikisha amani na usalama wa wananchi na mali zao vinaendelea kulindwa.

Wakati Sirro akitoa kauli hiyo, Balozi wa Tanzania nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC), Said Mshana amezungumzia changamoto za kiusalama zinazowakabili madereva raia wa Tanzania, wanaofanya kazi nchini humo.

Gazeti hili lilimtumia Mshana kipande cha video kinachosambaa mitandaoni, kinachomwonesha dereva raia wa Tanzania aliyeko Uvira, akilalamikia hali mbaya ya usalama, huku milio ya risasi ikisikika, hali inayoashiria hatari kubwa inayowakabili raia hao.

Mshana amesema eneo la Mashariki mwa DRC ni kubwa kijiografia na kuwa majimbo ya Ituri, Kivu Kaskazini na Kivu Kusini yanakabiliwa na changamoto za kiusalama.

Amesema baadhi ya maeneo hayo yanadhibitiwa na waasi wa makundi ya M23, AFC na ADF, hali inayosababisha hatari kwa wasafiri na wafanyabiashara.

“Kila mara tumekuwa tukitoa elimu na kuwaelekeza madereva pamoja na waajiri wao kuchukua tahadhari za kutosha wanaposafiri katika maeneo hayo,” amesema Mshana.

Ameongeza kuwa ni muhimu kwa madereva kufahamu hali ya usalama wa maeneo wanayokusudia kuyafikia ili kuepuka kukumbana na madhila yanayosababishwa na makundi ya waasi.

“Endapo dereva atakumbana na changamoto, anapaswa kuwasiliana na ndugu zake au mwajiri wake ili kufanikisha mawasiliano nasi. Ni muhimu kujua namba yake ya simu, eneo alilopo pamoja na umbali wake kutoka mpakani,” amesema.

Mshana amesema kuwa lengo la kukusanya taarifa hizo ni kuwezesha ubalozi kushirikiana na nchi jirani, ikiwemo Burundi au Rwanda, ili kutoa msaada wa haraka na salama kwa raia wanaokumbwa na matatizo.

Amefafanua kuwa tangu kuzuka kwa machafuko katika maeneo hayo, amekuwa akisaidia raia wengi wa Tanzania kupitia utaratibu huo wa ushirikiano wa kidiplomasia.

“Mfano mzuri juzi kuna baadhi baada ya kunitafuta, niliwasiliana na ubalozi wa Tanzania mjini Kigali, ambao uliwasaidia raia wetu kuvuka kutoka Bukavu hadi Tanzania kupitia Rwanda,” amesema.