Dar es Salaam. Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa (UN), Antonio Guterres amesema matukio yaliyotokea katika uchaguzi mkuu wa mwaka huu, yalikuwa jaribio kwa taswira ya amani ya Tanzania na kwamba nchi hiyo imevuka.
Mtendaji Mkuu huyo wa UN, ametoa kauli hiyo leo, Jumapili, Desemba 14, 2025 alipopokea ujumbe wa Tanzania kutoka kwa Rais Samia Suluhu Hassan, uliowasilishwa na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Mahmoud Thabit Kombo.
Amegusia Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 29, mwaka huu akisema, ulikuwa jaribio kubwa kwa taswira ya amani ya Tanzania, lakini Taifa limevuka, licha ya changamoto zilizojitokeza.
Katika maelezo yake, Guterres amesema Tanzania imeendelea kuwa kielelezo cha amani na mshikamano wa kijamii barani Afrika na duniani, akisisitiza kuwa dunia inalitazama Taifa hilo kama mfano wa kuigwa.
“Tungependa kuona Tanzania ikiendelea kuwa Taifa lililoungana na mfano bora wa amani,” amesema Guterres.
Pia amesisitiza umuhimu wa mazungumzo ya kitaifa jumuishi na yenye maana, ili kushughulikia chanzo cha matukio ya vurugu yaliyotokea wakati wa uchaguzi na kuzuia yasijirudie.
Pia ameahidi msaada wa Umoja wa Mataifa kwa Tanzania, hususan wakati na baada ya Tume ya Uchunguzi iliyoundwa na na Serikali kukamilisha majukumu yake.
Kauli hiyo ya Katibu Mkuu wa UN, inakuja katikati ya matamko ya jumuiya mbalimbali za kimataifa zinazoshinikiza uwajibikaji kwa waliohusika na mauaji ya raia wakati wa vurugu za Oktoba 29.
Matamko hayo yamekwenda mbali zaidi na mengine yanatishia kuathiri uhusiano na ushirikiano wa jumuiya hizo na Tanzania, kwa kile yanachosisitiza ni muhimu haki izingatiwe.
Hata Marekani, imesema inatathmini upya uhusiano wake na Tanzania kutokana na matukio hayo iliyoyaita ya uvunjifu wa amani, huku taifa hilo likiwa katika hatua za mwisho za mazungumzo ya uwekezaji katika Gesi Asilia ya Kimiminika (LNG).
Yote hayo, yametokana na tukio la maandamano yaliyozaa vurugu Oktoba 29 na kusababisha vifo vya watu, uharibifu wa mali za umma na za watu binafsi.
