Sydney, Australia. Watu 11 wamefariki dunia na wengine kadhaa kujeruhiwa baada ya shambulio la risasi lililotokea leo Jumapili Desemba 14, 2025, katika ufukwe wa Bondi, mashariki mwa Jiji la Sydney nchini Australia.
Taarifa ya polisi wa Jimbo la New South Wales zinaeleza kuwa tukio hilo limetokea wakati watu walipokuwa wamekusanyika kusherehekea sikukuu ya Hanukkah (Chanukah), moja ya sikukuu muhimu kwa jamii ya Waisrael.
Washambuliaji waliokuwa na silaha wamefyatua risasi hovyo, hali iliyosababisha vifo na majeruhi wengi kabla ya polisi kuingilia kati.
Uchunguzi wa awali unaonyesha tukio hilo lina viashiria vya shambulio la kigaidi lenye mwelekeo wa chuki dhidi ya jamii ya Waisrael.
Mashuhuda wameiambia Shirika la Habari la ABC News kuwa walisikia milio ya risasi mfululizo na kuona watu wakikimbia ovyo kutafuta usalama, huku magari ya wagonjwa na vikosi vya polisi vikifika eneo la tukio kwa haraka.
Viongozi wa Australia, akiwamo Waziri Mkuu, Anthony Albanese, wamelaani vikali shambulio hilo na kutoa pole kwa familia za zilizopoteza ndugu zao, wakisisitiza kuwa taifa hilo halitavumilia vitendo vya chuki na ugaidi hata hivyo eneo la Bondi Beach limefungwa mara moja kwa sababu za kiusalama.
Mamlaka zinaendelea na uchunguzi kubaini chanzo na mtandao wa washambuliaji, huku usalama ukiimarishwa katika maeneo ya mikusanyiko ya umma nchini humo.
Kati ya waliouawa yumo Rabbi Eli Schlanger
Kwa mujibu wa The Jerusalem post na Times of Israel kati ya waliouawa yupo mjumbe wa shirika la Kiyahudi la Chabad aitwaye Rabbi Eli Schlanger.
Schlanger alikuwa kiongozi wa Kiyahudi na mtumishi wa Chabad aliyefanya kazi kwa miaka mingi kukuza shughuli za jamii ya Kiyahudi huko Bondi Beach, Sydney, Australia.
Schlanger alikuwa mjumbe (emissary) wa Chabad-Lubavitch, shirika la Kiyahudi la kimataifa linayojikita katika huduma za kidini, kijamii na kielimu kwa Wayahudi walioko nje ya Israel.
Alikuwa rabbi (mwalimu) wa Chabad aliyekuwa akihudumu katika jumuiya ya Wayahudi Sydney, Australia, alijihusisha na kuandaa na kusimamia shughuli za kidini, ikiwemo sherehe za Hanukkah, ibada, elimu ya dini na msaada wa kijamii.
Aidha alikuwa miongoni mwa maelfu ya wajumbe wa Chabad duniani kote wanaotumwa hata katika maeneo yenye idadi ndogo ya Wayahudi.
Hata hivyo taarifa zaidi zinasema zikinukuu polisi mmoja wa washukiwa ameuawa kwa kupigwa risasi na askari wa usalama, huku mwingine akikamatwa akiwa mahututi.
Kutokana na vifo hivyo tukio hilo limelaaniwa vikali na viongozi wa kisiasa na kidini wa Israel na dunia kwa ujumla.