Dar es Salaam. Viongozi wanane wa Halmashauri za Wilaya za Mafia, Mkoa wa Pwani na Kilolo, mkoani Iringa wamesimamishwa kazi kwa tuhuma za usimamizi dhaifu wa fedha za miradi ya maendeleo inayotekelezwa katika wilaya hizo.
Waliosimamishwa kazi ni Mkuu wa Idara ya Fedha na Ofisa Utumishi na Rasilimali Watu wa Wilaya ya Mafia na Mkuu wa Idara ya Fedha na Mkaguzi wa Ndani wa Halmashauri ya Wilaya ya Kilolo, Iringa.
Hatua ya kusimamishwa kazi kwa maofisa hao, imetangazwa leo, Jumapili Desemba 14, 2025 na Naibu Waziri wa Ofisi ya Waziri Mkuu, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi) anayeshughulikia Elimu, Reuben Kwagilwa wakati wa vikao vya majumuisho ya ziara ya kukagua miradi ya maendeleo Kilolo na Mafia.
Amesema hajaridhishwa na namna fedha za miradi zinavyosimamiwa na utekelezaji wake, akieleza tangu Rais Samia Suluhu Hassan aingie madarakani, Serikali imepeleka zaidi ya Sh24 bilioni wilayani Mafia.
Amemtaka Katibu Mkuu Tamisemi (Adolf Ndunguru) kutuma timu maalumu kufuatilia mwenendo wa Ofisa Utumishi na Rasilimali Watu wa halmashauri hiyo ili kubaini uzingatiaji wa taratibu za kiutumishi.
Ametaka ndani ya siku 21 apelekwe Mkuu wa Idara ya Ujenzi katika halmashauri hiyo ili miradi ya maendeleo ipate usimamizi wa karibu na kuepusha ucheleweshaji na matumizi yasiyo sahihi ya fedha.
Sababu waliosimamishwa Kilolo
Kwa upande wa Wilaya ya Kilolo, viongozi hao wamesimamishwa ili kupisha uchunguzi wa matumizi ya fedha za ujenzi wa Shule ya Sekondari ya Wasichana ya Lugalo iliyogharimu zaidi ya Sh4.7 bilioni na haijakamilika.
Amesema hiyo ni tofauti na miradi mingine ya aina hiyo iliyotekelezwa kwa takribani Sh4.45 bilioni na kukamilika kama ilivyopangwa.
Wakati huohuo, Kwagilwa amemuagiza Ndunguru kuwapangia majukumu mengine Ofisa Elimu Sekondari na Msingi na Ofisa Taaluma Sekondari na Msingi wa Wilaya ya Kilolo kwa kushindwa kutekeleza majukumu yao ipasavyo.
“Watumishi wa umma, hasa walio chini ya wizara yetu ya Tamisemi, jifunzeni kuziheshimu na kuziogopa fedha za umma zinazoletwa kwa ajili ya kufikisha huduma kwa wananchi,” amesema.
