Zambia kuendelea kushirikiana na Tanzania kiuchukuzi

Dar es Salaam. Zambia imesema itaendelea kuwa mdau muhimu wa sekta ya usafiri na uchukuzi nchini Tanzania, ikibainisha kuwa  ushirikiano kati ya nchi hizo mbili umeleta matokeo chanya kiuchumi kwa wananchi wake na katika ukanda wa kusini mwa Afrika.

Hayo yameelezwa na Katibu Mkuu wa Wizara ya Uchukuzi ya Zambia, Fredrick Mwalusaka wakati wa uzinduzi wa mtambo mpya wa kupakia kontena ulionunuliwa na kampuni ya usafirishaji ya Zambia Cargo and Logistics Limited (ZCL), utakaokuwa ukitoa huduma katika ofisi za kampuni hiyo kituo cha Mukuba bandari ya Dar es Salaam.

Akizungumzia uzinduzi wa mtambo huo mwishoni mwa wiki iliyopita Mwalusaka alisema uwekezaji huo una lengo la kuongeza uwezo wa kuhudumia mizigo mingi zaidi, kwani unaonyesha utayari wa wawekezaji kutoka Zambia kuimarisha sekta ya uchukuzi katika ukanda wa kusini mwa Afrika na barani kwa ujumla.

“Kukua kwa uwezo wa kampuni ya ZCL katika utoaji wa huduma hapa nchini ni ishara pia ya kuimarika kwa ushirikiano wetu wa muda mrefu, na sisi tunadhamiria kuendelea kuimarisha zaidi kwa manufaa ya nchi zetu mbili,” alisema Mwalusaka.

Kwa upande wake Naibu Waziri wa Uchukuzi wa Tanzania, David Kihenzile aliyehudhuria uzinduzi huo alisema Serikali ya Tanzania nayo inaendelea kufanya maboresho ya sekta ya uchukuzi kwa ajili ya Zambia na bara la Afrika kwa ujumla.

Alisema maboresho hayo ni pamoja na kuongeza gati katika bandari ya Dar es Salaam, ujenzi wa bandari mpya ya Bagamoyo, kuongeza mtandao wa reli ya kisasa (SGR) pamoja na upanuzi wa barabara muhimu.

“Serikali yetu imedhamiria eneo la uchukuzi kuwa uti wa mgongo wa uchumi wa nchi ndiyo maana tunafanya maboresho ya miundombinu muhimu ili kufanikisha hilo. Mathalani Bandari ya Dar es Salaam tuna gati 12 tunataka kuongeza nyingine 10 ziwe 22 na kuongeza matanki ya kuhifadhi mafuta,” alisema Kihenzile.

Kadhalika Kihenzile aligusia kufufuliwa kwa reli ya Tazara akisema lengo ni iwe na uwezo wa kusafirisha tani milioni tano za mizigo kwa mwaka kiwango ambacho hakijawahi kufikiwa tangu ijengwe.

Awali akitoa neno la ukaribishao Ofisa Mtendaji Mkuu wa ZCL, Vyonsi Manda alisema kwa muda ambao kampuni hiyo imefanya kazi hapa nchini imekuwa ikipata ushirikiano wa Serikali ya Tanzania, Zambia pamoja na wafanyakazi akisema hivyo ndiyo siri ya ufanisi wao mzuri.

Alisema kampuni hiyo imekuwa ikishuhudia mwenendo mzuri wa ukuaji katika kipindi cha miaka ya hivi karibu akitolea mfano kuwa miaka mitano iliyopita walikuwa wakihudumia kontena 15,000 kwa mwaka, lakini sasa wanahudumia 50,000.

“Kwa mtambo huu tulionunua tuna imani kuwa sasa idadi ya kontena tunazozihudumia kwa mwaka itafikia 70,000 jambo ambalo linaonesha mwanga wa kufikia malengo yetu ya kuhudumia kontena 200,000 miaka 15 ijayo,” alisema Manda.

Aidha mamlaka nyingine zilizohudhuria uzinduzi wa mtambo huo ikiwemo Mamlaka ya Mapato (TRA), Mamlaka ya Bandari (TPA) na Shirika la uwakala wa meli Tanzania (Tasac) wote waliahidi kuendelea kutoa ushirikiano wenye manufaa kwa Zambia na Tanzania.