ZDCEA yataifisha mali za  Sh169 milioni za mtuhumiwa dawa za kulevya 

Unguja. Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya Zanzibar (ZDCEA), imetaifisha nyumba nne za mtuhumiwa wa dawa za kulevya, Mohamed Omar Ali (44) zenye thamani ya Sh169 milioni.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotumwa kwenye vyombo vya habari leo Jumapili Desemba 14, 2025, Kamishna Mkuu wa Mamlaka hiyo, Kanali Burhani Zubeir Nassor amesema nyumba tatu zilizopo Jondeni Mkoa wa Kusini Pemba zina thamani ya Sh131 milioni.

Pia, amesema nyumba iliyopo Kihogoni, Shehia ya Ng’ombeni, Wilaya ya Mkoani, Mkoa wa Kusini Pemba ina thamani ya Sh37 milioni zote zimetaifishwa kuwa mali ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ).

“Kwa uwezo niliopewa chini ya kifungu cha 73 (1) cha Sheria ya Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya Zanzibar, Sheria namba 8 ya 2021, nimetaifisha nyumba nne za mtuhumiwa huyo zenye thamani ya Sh169 milioni kuwa mali ya Serikali,” amesema Kanali Burhani. 

Amefafanua kuwa, hatua hiyo imekuja baada ya Ofisi ya Pemba ya ZDCEA kufanya operesheni Aprili 14, 2025 eneo la Jondeni Mkoa wa Kusini Pemba na kufanikiwa kumkamata mtuhumiwa Haji Khamis Haji (40) akiwa na dawa za kulevya aina ya hiroin kete 700 ndani ya nyumba namba 157 inayomilikiwa na mtuhumiwa Mohamed Omar Ali.

Ameeleza kuwa, mtuhumiwa huyo alifanikiwa kutoroka siku ya tukio na kuelekea kusikojulikana hivyo juhudi za kumtafuta zinaendelea na akipatikana atafikishwa mahakamani kujibu tuhuma zinazomkabili.

Amesema, katika uchunguzi uliyofanywa umebaini kuwa mtuhumiwa Haji ni mfanyabiashara haramu wa dawa za kulevya anayechukua dawa hizo kutoka kwa Mohamed Omar Ali, kwa lengo la kuuza kwa vijana na kusambaza kwa wafanyabiashara wengine wa maeneo mbalimbali Pemba.

Kanali Burhani amesema, kupitia biashara hiyo haramu mtuhumiwa huyo Mohamed amefanikiwa kumiliki nyumba nne zilizopo shehia ya Ng’ombeni, Mkoa wa Kusini Pemba.

Amesema, kufuatia uchunguzi huo, mtuhumiwa Haji atafikishwa mahakamani kujibu tuhuma zinazomkabili kwa mujibu wa sheria.

Vilevile, amesema endapo kuna mtu yeyote ambaye hajaridhika na tamko hilo anaweza kuiomba mahakama kufanya mapitio na ombi lake, ambapo linatakiwa kuwasilishwa mahakamani ndani ya siku 30 kutoka tarehe ya leo kama inavyoelekezwa na kifungu cha 73(4) cha Sheria namba nane ya mwaka 2021 cha Sheria ya Zanzibar.

Burhani amesema ikiwa mamlaka hiyo haitachukua hatua hizo, wahalifu watapata mwanya wa kutakatisha fedha haramu na kuhadaa jamii kwa lengo la kuonekana wao ni watu wema kumbe ni wahujumu uchumi wa Taifa.

Pia, ametoa wito kwa wananchi kuendelea kushiriki katika kudhibiti na kupambana na dawa za kulevya kwa kutoa taarifa za wahalifu wa dawa za kulevya katika maeneo yao, na taarifa hizo zitafanyiwa kazi kwa usiri na ambao watatoa taarifa zitakazosaidia kukamatwa kwa wafanyabiashara wakubwa wa dawa za kulevya watapatiwa zawadi.

Kuanzia mwaka 2023 hadi 2025, mamlaka hiyo imeshataifisha mali za wafanyabiashara wakubwa wa dawa za kulevya zikiwemo nyumba 15, beach villa moja, viwanja au mashamba manane, magari saba, pikipiki mbili na boti tatu, zote zikiwa na thamani ya Sh17.4 bilioni zikiwemo zilizotangazwa leo.

Kanali Burhani amesema, mamlaka hiyo imejipanga vyema kukabiliana na wafanyabiashara haramu wa dawa za kulevya, hivyo wale wote wanaojihusisha na biashara hiyo waache mara moja na watafute kazi nyingine halali za kufanya.