Ajali zilivyokatisha maisha ya watu 2025

Dar es Salaam. Bado jinamizi la ajali za barabarani limeendelea kuikumba Tanzania mwaka 2025, likiacha majeraha yasiyofutika katika familia, jamii na kuzidi kuathiri uchumi wa Taifa pamoja na Kaya.

Desemba 31, 2024 Rais Samia Suluhu Hassan akitoa salamu za mwaka mpya, alitoa maelekezo kwa Wizara ya Mambo ya Ndani na jeshi la Polisi kuongeza mikakati ya kuzuia ajali zinazosababishwa na uzembe.

Katika maelezo yake alirejea takwimu za Jeshi la Polisi zilizoonesha kulitokea jumla ya ajali 1,7315 Kwa mwaka huo na watu 1,715 walipoteza maisha kati ya Januari hadi Desemba mwaka jana.

Gari aina ya Fuso lililopata ajali kwa kugongana na basi mkoani Dodoma likiwa katika eneo la ajali. Picha na Maktaba.

Licha ya juhudi zinazochukuliwa na Serikali na wadau wa usalama barabarani, mwenendo wa ajali bado unaonesha taswira ya kutisha, ukipoteza nguvu kazi, ulemavu wa kudumu, kuua ndoto za wananchi na kusababisha hasara ya mali na rasilimali watu.

Mwaka huu ajali nyingi zimeripotiwa, huku ikielezwa chanzo ni  changamoto za miundombinu, uzembe wa madereva, magari chakavu na mazingira hatarishi ya barabara.

Juni 28, 2025 eneo la Sabasaba, Same mjini, watu takribani 41 walifariki dunia.

 Ajali hiyo ilihusisha Basi la Chanel One lililotokea Moshi kwenda Tanga na basi dogo aina ya Toyota Coaster kutoka Same kwenda Moshi.

Magari hayo yaligongana uso kwa uso na baadaye kushika moto na kusababisha ajali kwa abiria waliokuwamo ndani ya mabasi hayo.

Aprili 3,2025  eneo la Kikweni, Kijiji cha Mamba wilayani Mwanga, watu saba walipoteza maisha papo hapo na wengine 32 kujeruhiwa baada ya basi la Kampuni ya Mvungi kupinduka.

Basi lililopata ajali kwa kugongana na Fuso na kusababisha vifo vya watu tisa wilayani Chemba, Dodoma likiwa katika eneo la ajali. Picha na Maktaba.

Basi hilo lilikuwa likisafirisha abiria kutoka Ugweno kwenda Dar es Salaam.

Uchunguzi wa awali unaonesha kuwa, ajali hiyo ilitokana na basi hilo kupoteza uelekeo wakati likipishana na gari jingine eneo lenye tope, na hivyo kupinduka.

Usiku wa kuamkia Januari 13, 2025, majozi na vilio vilitanda Kata ya Segera, Wilaya ya Handeni mkoani Tanga, kufuatia vifo vya watu 11 na majeruhi 13, kutokana na ajali ya gari.

Ajali hiyo ilisababishwa na lori la mizigo lenye namba T 782 BTU. liliacha barabara na kuelekea mahali walipokuwa watu wakiwaokoa majeruhi kutoka kwenye ajali nyingine ya gari iliyotokea awali, ikilihusisha gari aina ya Tata

Ajali nyingine ilikuwa Machi 30, 2025 Wilaya ya Same ilipoteza watu saba, wakiwamo wanakwaya sita wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), katika ajali hiyo gari aina ya Coaster iliyotokea katika milima ya Upare.

Gari hilo lilipoteza mwelekeo katika Barabara ya Bangalala, likapinduka na kuua watu saba huku 23 wakijeruhiwa.

Julai 26, 2025 alfajiri, ajali ya kushtua iliikumba Wilaya ya Chunya, Mbeya, huku wanafunzi sita wa Shule ya Sekondari ya Chalangwa wakifariki dunia wakati wakifanya mazoezi ya viungo.

Basi la Kampuni ya Safina Coach liligonga kundi hilo la wanafunzi na kujeruhi wengine tisa.

 Tukio hilo liliibua mijadala mikali kuhusu ulinzi wa wanafunzi na utunzaji wa barabara zinazopitia maeneo yenye makazi na shule.

Agosti 27, 2025 Katika Halmashauri ya Mji wa Tunduma, watu watano walifariki dunia na watatu kujeruhiwa baada ya gari aina ya Toyota Hiace kugongana na lori la mizigo katika maeneo ya Chapwa.

Eneo hilo linalojulikana kwa msongamano wa magari ya mizigo, limekuwa likitajwa mara kwa mara kama hatari kutokana na ufinyu wa barabara na mwendo kasi.

Usiku wa kuamkia Desemba 12 2025, watu watano ambao ni madereva bodaboda walifariki dunia papo hapo baada ya kugongwa na lori lililofeli breki eneo la Dodoma Makulu jijini Dodoma.

Lori hilo aina ya Fao lenye namba za usajili T824 DKS lililokuwa linatokea barabara ya Chuo Kikuu cha Dodoma (Udom),  lilifeli breki na kwenda kuparamia kijiwe cha bodaboda cha Amani kilichopo kando ya barabara hiyo na kusababisha maafa hayo.

Wadau wa sekta ya usafiri nchini wametoa tathmini yao juu ya ongezeko la ajali barabarani, wakibainisha sababu kuu za matukio hayo na kutoa mapendekezo ya namna ya kulikwepa jinamizi hilo.

Katibu wa Chama cha Wamiliki wa Mabasi (Taboa), Priscus John amesema ajali nyingi zilizoripotiwa mwaka huu zimehusisha magari kutoka nje ya nchi.

“Magari haya mengi ni ya Kichina, hayana mwendo wa kutosha na madereva wake hupenda kusafiri usiku wakihofia kukutana na Polisi wa Tanzania,” amesema John.

Amesema madereva wanaotumia magari yenye usukani upande wa kushoto wanahitaji elimu maalumu ya kuendesha katika mazingira ya Tanzania ili kupunguza ajali.

John amezitaja barabara zilizotelekezwa kama chanzo kikuu cha ajali akisema, “barabara ya Singida–Arusha ina mashimo mengi kama ilivyo Dodoma. Hata barabara ya Dar es Salaam kwenda Zambia inahitaji kufanyiwa maboresho ya haraka.”

Amesema maeneo ambayo ajali hurudiwa mara kwa mara yanapaswa kupanuliwa au kutafutiwa barabara mbadala.

Huku akitaka Serikali kuangalia upya uwekezaji wa miundombinu ukilinganishwa na ukuaji wa uchumi na ongezeko la mizigo bandarini.

Uzembe wa madereva na mfumo dhaifu wa usimamizi, John amesema mwanzoni mwa mwaka huu, ajali nyingi zilisababishwa na mabasi madogo aina ya Coaster kutokana na madereva kukosa muda wa kupumzika.

Amependekeza polisi kusimamisha magari yenye hitilafu badala ya kutoza faini pekee ambazo zinazoacha chombo kibovu kiendelee na safari na kusababisha vifo mbele ya safari.

“Polisi kujivunia kukusanya fedha nyingi kupitia faini za magari wakati chombo kibovu kinapita na kuua watu, ni aibu,” amesema

Mwenyekiti wa Chama cha Madereva wa Mabasi yaendayo mikoani (Uwamata), Majura Kafumu amesema miundombinu mibovu ndiyo chanzo kikubwa cha ajali, huku madereva wakibeba lawama zisizo za kweli.

“Barabara ni finyu na kila mtu ana aina yake ya udereva. Watu wengi wanafundishwa na ndugu zao bila umahiri halafu wanatafutiwa leseni,” amesema.

Amesema mazingira duni ya kazi, mishahara midogo na kukosa bima za afya huchangia kushuka kwa ufanisi wa madereva.

Hoja ya idadi ya magari imeongezeka, lakini madereva bora wamepungua, Kamishna Mstaafu wa Polisi, Jamal Rwambo amesema kuwa wimbi la ajali linaweza kuongezeka endapo hakutakuwepo udhibiti wa madereva wasio na ujuzi.

“Wengi wanaitwa madereva kwa sababu tu wanajua kuhamisha gari, lakini hawana maarifa ya msingi. Wengine wanajua kuendesha lakini hawafuati sheria za barabarani,” amesema.

Ameongeza kuwa wakati mwingine askari huonesha huruma kwa watu wasiostahili, na hata watembea kwa miguu na waendesha pikipiki nao wanachangia ajali kwa kukaidi sheria.

Hatua za Serikali zimesaidia, lakini bado kuna changamoto, Mwenyekiti wa Chama cha Wamiliki wa Malori Wadogo na Wakati (Tamstoa), Chuki Shaban, amesema ajali kutokana na malori zimepungua ukilinganisha na miaka iliyopita kutokana na hatua madhubuti za Serikali na utoaji wa elimu kwa madereva.

Hata hivyo, ametaja changamoto kwa madereva wa malori ya ndani yanayobeba mazao kama nyanya, ndizi na mbao ambao ni vigumu kuwabana kwa kuwa wengi hawako kwenye vyama vinavyowapa mwongozo wa usalama.

“Kama malori ya nje ya nchi yanazingatia sheria hadi kuacha kazi saa 12 jioni, basi hata hawa wa ndani wanapaswa kuwekewa utaratibu na kupewa elimu,” amesema.

Kuhusu changamoto ya barabara, Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Barabara Tanzania (Tanroads), Mohamed Besta amesema changamoto ya barabara katika maeneo korofi inaanza kupatiwa ufumbuzi baada ya Serikali kupata fedha kwa ajili ya ujenzi wa barabara za kupita pembeni (by-pass).

Amesema by-pass ya Mbalizi tayari imekamilika, huku ujenzi wa by-pass ya Mlima Nyoka mkoani Mbeya ukiendelea baada ya kupatikana kwa fedha wiki iliyopita, na wakandarasi wakiwa tayari eneo la mradi.

“Kazi zinaendelea baada ya kupata fedha, na makandarasi wapo saiti kuanza utekelezaji,” amesema Besta.

Amesema barabara kuu ya kutoka Dar es Salaam hadi Zambia inaendelea kufanyiwa upanuzi kutokana na ongezeko la magari yanayotumia Bandari ya Dar es Salaam.

“Serikali inaendelea kutafuta fedha kwa ajili ya kupanua barabara hizi muhimu, na mchakato huo unaendelea,” amesema.

Besta amesema mwaka uliopita Tanroads ilifanya kazi kubwa iliyoacha historia, ikiwamo ufunguzi wa Daraja la Kigongo–Busisi pamoja na utekelezaji wa miradi mbalimbali iliyoanzishwa kufuatia uharibifu uliosababishwa na mvua za El Nino.

Amesema madaraja mengi, hususan katika ukanda wa kusini, yalibomoka lakini karibu yote yamejengwa upya na yapo hatua za mwisho za ukamilishaji.

“Kwa sasa madaraja mengi yamekamilika kwa zaidi ya asilimia 95, ikiwamo Daraja la Somanga Mtama,” amesema.

Pia, ameeleza kuwa madaraja ya Mikeremende, Kikwata pamoja na makaravati katika mikoa ya Rukwa na Mbeya yanaendelea kukamilishwa baada ya kupatikana kwa ufadhili kutoka Benki ya Dunia.