WAKATI dirisha dogo la usajili likitarajiwa kufunguliwa rasmi Januari Mosi, 2026, uongozi wa Azam unaangalia uwezekano wa kuipata saini ya beki wa kulia wa AS Vita Club, Mkongomani Henoc Lolendo Masanga, ili kuongeza ushindani wa nafasi.
Taarifa ambazo Mwanaspoti imezipata, zinaeleza uongozi wa Azam unaangalia uwezekano wa kupata saini ya beki huyo mwenye miaka 21, ili akaongeze ushindani zaidi kwa nahodha wa kikosi hicho, Lusajo Mwaikenda anayefanya vizuri kikosini humo.
Lusajo ni muhimili mkubwa wa timu hiyo katika eneo la beki wa kulia, ambapo licha ya uwepo wa nyota mwenzake, Nathaniel Chilambo anaye-weza kucheza pia akitokea beki ya kushoto, ila ameshindwa kupenya kwenye kikosi cha kwanza mara kwa mara.
Kiu ya Azam ni kupata beki wa kulia na sasa wanaendelea kufuatilia uwezekano wa kumpata Lolendo, baada ya dirisha kubwa la usajili lililopita kushindwa kumsajili mkongomani mwingine, Steven Ebuela anayeichezea Al Hilal Omdurman ya Sudan.
Hata hivyo, chanzo kutoka ndani ya uongozi wa Azam, kimeliambia Mwanaspoti kinachoangaliwa kwa sasa ni namna ya kuuvunja mkataba wake ndani ya kikosi cha AS Vita Club, kwa sababu bado amebakisha miaka minne zaidi kikosini humo.
Beki huyo alijiunga na AS Vita Januari 2025, akitokea AC Rangers ya kwao DR Congo, ingawa tayari ameonyesha uwezo mkubwa unaoivutia Azam kuanza kuiwinda saini yake, huku mazungumzo baina ya pande mbili yakiendelea ili kukamilisha dili hilo.
