WAKATI beki wa kati wa Coastal Union, Haroub Mohamed, akibakisha miezi sita katika mkataba wake na kikosi hicho cha jijini Tanga, tayari timu mbalimbali zimeanza kuiwinda saini yake zikiwamo za KMC, TRA United na maafande wa JKT Tanzania na Mashujaa.
Mtu wa karibu na nyota huyo aliliambia Mwanaspoti, licha ya ofa mbalimbali za kuhitajika, uongozi wa Coastal umeanza mazungumzo ya kumuongezea mkataba mpya, japo hadi sasa hakuna muafaka uliofikiwa baina ya pande mbili.
“Mazungumzo hayo yalianza tangu msimu uliopita, lakini mchezaji mwenyewe aliomba kwanza kusubiri, nadhani aliona thamani yake sokoni itaongezeka zaidi ndio maana akaacha kusaini tena mkataba mpya na hao waajiri wake,” alisema kiongozi huyo.
Kiongozi huyo alisema tayari timu nne zimeonyesha uhitaji wa beki huyo wa kati ambazo ni KMC, TRA United, JKT Tanzania na Mashujaa, ingawa hadi sasa hakuna makubaliano yaliyofikiwa na yoyote, kwa sababu bado wanafanyia tathimini ofa hizo.
“Kwa sasa tunaweza kusema ni timu tano zinazomhitaji kwa sababu hata Coastal yenyewe bado inamtaka, ndio maana inataka kumpa mkataba mpya, licha tu ya kuangalia pia ofa nzuri, ila changuo litabakia kwa mchezaji mwenyewe,” alisema.
Nyota huyo alijiunga na Wanamangushi, Julai 10, 2024, akitokea Malindi ya visiwani Zanzibar kwa mkataba wa miaka miwili unaofikia mwisho Julai mwakani, jambo linalotoa nafasi kwa nyingine kuiwinda saini yake.