China yaendelea kuimarisha, kulinda afya za watoto nchini

Dar es Salaam. Balozi wa China nchini, Chen Mingjian, amesema dhamira ya nchi yake ni kulinda na kuendeleza afya na ustawi wa watoto, akisema watoto ndio msingi wa maendeleo ya taifa na daraja muhimu la urafiki wa muda mrefu baina ya mataifa hayo mawili.

Balozi Chen ameeleza hayo wakati wa sherehe ya kuadhimisha mwaka wa pili wa mpango wa uhamasisha afya kwa watoto (Warm Children’s Hearts: A China-Africa Joint Action,) uliofanyika Desemba 13 na 14 Dar es Salaam, katika kituo cha kulea yatima cha Zaidia.

Miradi ya afya kwa wanawake na watoto barani Afrika iliyoasisiwa na Profesa Peng Liyuan, ambaye ni mke wa Rais Xi Jinping wa China, imeendeleza ustawi wa afya za watoto na kufikia ndoto zao nchini.

Katika hafla hiyo, Balozi Chen mpango huo unatekelezwa katika nchi mbalimbali za Afrika, ukilenga kuwafikia watoto wasiojiweza kwa kuwapatia huduma za afya, ili kuhakikisha anayekosa matibabu kutokana na ukosefu wa rasilimali.

Balozi Chen amesisitiza umuhimu wa msaada wa China katika sekta ya afya na ustawi wa watoto, amefurahishwa kurejea katika kituo hicho miaka miwili baada ya uzinduzi wa mpango huo.

“Miaka miwili iliyopita tulikusanyika hapa kuanzisha mpango huu. Leo tunafurahi kuona watoto hawa wakiendelea kukua wakiwa na afya njema, nguvu, na matumaini,” amesema Balozi Chen.

Balozi Chen pia amepongeza juhudi za Mkurugenzi wa Kituo cha Kulea Watoto Yatima cha Zaidia , Aisha Sudi na wafanyakazi wake kwa kujitolea kwenye kituo chao kusaidia ustawi wa watoto kufikia ndoto zao.

Kwa mujibu wa Balozi Chen, Tanzania imekuwa mshiriki muhimu katika mpango huu, ikipokea msaada wa chakula, dawa, na vifaa vya kielimu, huku ikinufaika na huduma za madaktari wa China walioko hapa.

“Kuwaona watoto hawa wakiendelea kukua wakiwa na kujiamini kunanifanya nijisikie furaha kubwa. Watoto hawa pia ni ishara ya urafiki wa kudumu kati ya China na Tanzania,” amesema Balozi Chen.

Mkurugenzi wa kituo hicho, Aisha Sudi amesema kujitolea kwao ni huruma katika kuwahudumia watoto wa kitanzania katika kutimiza ndoto zao.

Amesema lengo lao ni kuhakikisha watoto hao wanapata fursa ya kustawi kimaisha, kisaikolojia na kiafya, hali inayowasaidia kufuata ndoto zao bila vizuizi vya ukosefu wa rasilimali au changamoto za maisha.

Aisha amesema wanatambua kuwa kila jitihada ya kuwahudumia watoto, kwa malezi, elimu, lishe na huduma za afya, inachangia katika kujenga mustakabali thabiti kwa kila mtoto.

Kiongozi wa timu ya madaktari hao, Dk Bao Zengtao, amesema mpango huo ni alama ya urafiki na uwajibikaji wa pamoja kati ya nchi hizo mbili.