::::::::::
Naibu Waziri wa Uchukuzi,David Kihenzile (Mb), leo Desemba 15, 2025 ametembelea banda la Mamlaka ya Udhibiti Usafiri Ardhini (LATRA) katika maonesho ya Mkutano wa 18 wa Tathmini ya Utendaji wa Sekta ya Uchukuzi, na kushuhudia shughuli za Udhibiti zinazo tekelezwa na LATRA.
Akiwa katika banda la mamlaka hiyo, Mhe. Kihenzile ameipongeza LATRA kwa kazi nzuri inayofanywa ikiwemo matumizi ya mifumo mbalimbali ya TEHAMA ambayo imerahisisha upatikanaji wa huduma za usafiri kwa abiria na watumiaji wengine ikiwemo mfumo wa Safari Tiketi unaowezesha ukataji wa tiketi za mabasi yote na tiketi za treni, Mfumo Tumizi wa LATRA (LATRA App) unaowezesha taarifa kwa abiria wa mabasi ya mikoani na nchi jirani na Mfumo wa Kufuatilia Mwenendo wa Magari (VTS).
Kwa upande wake, CPA, Dkt. Habibu Suluo, Mkurugenzi Mkuu LATRA, amesema kuwa, LATRA imejipambanua kwenye matumizi ya mifumo mbalimbali ya TEHAMA na itaendelea kusimamia utekelezaji wa maono ya viongozi wa Nchi kwa kuongeza ufanisi katika usafirishaji wa abiria na mizigo katika sekta zinazodhibitiwa nchini.
Mkutano huo wa siku tatu unafanyika katika Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Arusha (AICC) kuanzia Desemba 15 hadi 17, 2025 wenye kaulimbiu Mifumo Jumuishi ya Usafiri kama Nguzo ya Mageuzi ya Kiuchumi.









