Dhamana ya Mwambe anayeshikiliwa polisi kusikilizwa leo

Dar es Salaam. Mahakama ya Hakimu Mkazi, Dar es Salaam, Kisutu, leo Jumatatu, Desemba 15, 2025 inasikiliza shauri la maombi ya dhamana ya waziri wa zamani, Geofrey Mwambe anayeshikiliwa na Jeshi la Polisi, Dar es Salaam.

Mwambe ambaye amewahi kuwa mkurugenzi wa Kituo cha Uwekezaji (TIC), mbunge wa Masasi, Mtwara (CCM), Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu, Uwekezaji na Waziri wa Viwanda na Biashara amekuwa akishikiliwa na Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam tangu Desemba 7, 2025.

Hata hivyo, Desemba 11, 2025, Mwambe kupitia wakili wake Hekima Mwasipu alifungua shauri la maombi ya dhamana mahakamani hapo dhidi ya Mkuu wa Jeshi la Polisi, Inspekta Jenerali (IGP) na wenzake wawili.

Wajibu maombi wengine katika shauri hilo ni Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP) na Mkuu wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai Kanda Maalumu Dar es Salaam (ZCO).

Katika shauri hilo la maombi namba 289778/2025,  lililofunguliwa chini ya hati ya dharura sana Mwambe anaiomba mahakama hiyo iamuru afikishwe mahakamani na  apewe dhamana kwa masharti yatakayowekwa na mahakama hiyo.

Shauri hilo limepangwa kusikilizwa leo Desemba 15,2025 saa 3:00 asubuhi na Hakimu Mkazi Mkuu, Hassan Makube.

Kwa mujibu wa hati ya kiapo inayounga mkono maombi hayo, Mwambe alikamatwa katika makazi yake eneo la Tegeta (Wilaya ya Kinondoni) jijini Dar es Salaam, usiku wa tarehe hiyo na watu waliojitambulisha kama maofisa wa Polisi, akapelekwa katika kituo cha Polisi Mbweni, ambako alihojiwa kwa tuhuma za uchochezi.

Kisha alihamishiwa kituo kikuu cha Polisi (Central) kwa usimamizi wa mjibu maombi wa tatu (ZCO) ambako alihojiwa kwa mara ya pili kwa tuhuma za uchochezi na baada ya mahojiano hayo ya pili, siku hiyohiyo alipelekwa mahabusu katika Kituo cha Polisi Kigamboni.

Desemba 8, 2025 wakili Mwasipu alikwenda na kuzungumza naye katika kituo cha Polisi Kigamboni, ambapo Mwambe alimsimulia mateso aliyopitia pamoja na kunyimwa dhamana ambayo ni haki yake ya Kikatiba na tangu tarehe hiyo alipokamatwa amekuwa kizuizini kinyume na sheria.

“Sheria inaelekeza kuwa mtuhumiwa lazima afikishwe mbele ya mahakama ya sheria ndani ya saa 24 tangu kukamatwa. Mwombaji amekuwa kizuizini kwa zaidi ya saa 24. Amekuwa kizuizini kwa zaidi ya siku nne sasa (Desemba 11) bila sababu yoyote ya msingi au maelezo kutoka kwa wajibu maombi,” inasomeka hati hiyo na kuongeza:

“Mwombaji ana haki ya kikatiba ya uhuru wa kutembea, haki ya kuishi kama mtu huru, na haki ya dhamana. Alinielekeza kuomba dhamana katika mahakama ya sheria ili kuhakikisha uhuru wake.”

Katika hati ya dharura, Wakili Mwasipu amethibitisha kuwa  uamuzi wa maombi hayo unahitaji kushughulikiwa kwa dharura sana.

Amefafanua mwombaji amekamatwa na kushikiliwa kinyume cha sheria kwa zaidi ya siku nne sasa (Desemba 11), bila kupewa dhamana ya polisi au kufikishwa mahakamani ili kushughulikiwa kwa mujibu wa sheria.

Pia amedai mwombaji ameshikiliwa na kunyimwa dhamana ya polisi bila sababu au maelezo yoyote halali kutoka kwa mjibu maombi wa kwanza (IGP) na wa tatu.

Vilevile wakili Mwasipu amedai katika hati hiyo ya dharura kuwa  kushikiliwa huko kunamsababishia madhara makubwa kuliko manufaa, hususan ikizingatiwa kuwa mwombaji si mtu mwenye vurugu na hajawahi kuonesha dalili zozote za kutumia nguvu.

Desemba 11, Wakili. Mwasipu alilieleza Mwananchi  Mwambe  alihamishwa kutoka Kituo cha Polisi Kigamboni na kupelekwa mahali ambako mpaka siku anafungua shauri hilo walikuwa  hawajapafahamu.

“Leo asubuhi familia ilimpelekea chakula wakaambiwa kuwa hayupo wameshamtoa, sasa mpaka sasa hivi hatujui yuko katika kituo gani cha Polisi. Tunazidi kufuatilia pamoja na familia ili kujua amepelekwa kituo gani cha polisi,” amesema wakili Mwasipu.

Siku moja baada kuripotiwa kwa  taarifa za Mwambe kufungua shauri hilo akipinga kile anachokiita kuwekwa kizuizini isivyo halali, Desemba 12 ndipo Jeshi la Polisi Dar es Salaam lilipotoa taarifa kwa umma likikiri kumshikilia Mwambe kwa mahojiano kuhusiana na tuhuma za kijinai ambazo hata hiyo halikuzitaja.