DKT. KIJAJI: USHINDI WA TUZO ZA UTALII DUNIANI NI MATUNDA YA FILAMU YA ‘TANZANIA: THE ROYAL TOUR’.

Na Philipo Hassan – Dodoma

Waziri wa Maliasili na Utalii Mhe. Dkt. Ashatu Kijaji (Mb) ameeleza kuwa Tanzania kuibuka mshindi wa Tuzo mbalimbali za utalii duniani ni matunda ya filamu ya “Tanzania: The Royal Tour” iliyochezwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan.

Waziri Dkt. Kijaji amesema hayo leo Desemba 15, 2025 katika hafla ya kupokea na kusherehekea tuzo za kimataifa ambazo Tanzania imeshinda katika sekta ya utalii kwa mwaka 2025. Hafla hiyo imefanyika katika Ofisi za Wizara ya Maliasili na Utalii, Mtumba Jijini Dodoma.

“Tunautambua na kuuthamini kwa upekee mchango wa Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan katika Filamu ya “Tanzania: The Royal Tour”. Hakika mafanikio haya ni jitihada zake mahsusi kwa yeye binafsi kufungua milango ya kutangaza utalii wa Tanzania kimataifa, ambapo leo hii tunashuhudia jumla ya tuzo 5 za utalii ambapo zimeendelea kuipeperusha bendera ya Tanzania duniani” ~ alieleza Dkt. Kijaji.

Dkt. Kijaji aliongeza kuwa “Tanzania kuteuliwa kuandaa tuzo wa utalii duniani kwa mwaka 2026 ni ishara kuwa Tanzania inaendelea kuongoza katika sekta ya utalii duniani. Hivyo, tujipange vizuri kuipokea heshima hiyo kubwa na maandalizi yaanze mapema kwa kuunda kamati ya kimkakati ya maandalizi ili kufanikisha zoezi hilo la kimataifa ambalo litaileta dunia katika nchi yetu ya Tanzania.

Awali, akitoa maelezo kuhusu tuzo hiyo Katibu Mkuu wa Wizara ya Maliasili na Utalii, Dkt. Hassan Abbasi alieleza kuwa Tanzania imeibuka mshindi wa tuzo tano (5) ambazo zinajumuisha tuzo ya nchi ya Tanzania, Taasisi za Serikali pamoja na wadau binafsi.

“Tanzania ilishinda tuzo hizi katika Hafla ya 32 ya “World Travel Awards 2025”, iliyofanyika tarehe 6 Desemba 2025 nchini Bahrain, ambapo Tanzania iliendelea kushikilia taji la Nchi Inayoongoza Duniani kwa Utalii wa Safari kwa mara ya tatu mfululizo. Pia, Hifadhi ya Taifa Serengeti ilishinda tuzo ya Hifadhi Bora ya Taifa Duniani 2025, Kisiwa cha Zanzibar (Spice Islands) kiliibuka mshindi wa “World MICE Awards 2025 kama Eneo Bora Afrika kwa Mikutano na Matukio ya Kitaasisi.” Alieleza Dkt. Abbasi

Aidha, tuzo za wadau na makampuni binafsi zilikuwa ni pamoja na Serengeti Balloon Safaris ambayo ilitwaa tuzo ya Kampuni Bora ya Utalii wa wa Puto Duniani, na Jumaira Thanda Resort iliyopo Kisiwa cha Mafia iliyotangazwa mshindi katika kipengele cha Kisiwa Bora cha Mapumziko Duniani hali iliyothibitisha  hadhi na ubora wa vivutio vya mapumziko na huduma za ukarimu nchini kwa viwango vya kimataifa.

Hafla hiyo ilihudhuriwa na viongozi mbalimbali wa Wizara ambao ni pamoja na Naibu Katibu Mkuu Bw. Nkoba Mabula, Mkurugenzi wa Utalii Tanzania, Dkt. Thereza Mugobi, Mkurugenzi wa Bodi ya Utalii Tanzania Ephraim Mafuru, Kamishana wa Uhifadhi TANAPA CPA Musa Nassoro Kuji pamoja na wadau mbalimbali wa sekta ya uhifadhi na utalii nchini Tanzania.