Gereza la Kibondo lageukia ubunifu nishati safi ya kupikia

Kigoma. Jeshi la Magereza wilayani Kibondo mkoani Kigoma limeanza kutumia mkaa mbadala unaotokana na mchanganyiko wa randa za miti na udongo unaozalishwa ndani ya gereza hilo, ikiwa ni sehemu ya utekelezaji wa agizo la Serikali la matumizi ya nishati safi ya kupikia.

Serikali, kupitia Mkakati wa Taifa wa Matumizi ya Nishati Safi ya Kupikia (2024–2034), imeelekeza taasisi zake kutumia nishati safi, juhudi ambazo ni sehemu ya kufikia lengo kuu la kitaifa la kuhamia kwenye matumizi ya nishati safi ya kupikia.

Kuanzia Julai 2024, kila wizara, idara na taasisi za umma, tawala za mikoa na mamlaka za serikali za mitaa zilijumuisha masuala ya nishati safi ya kupikia katika mipango na mikakati yao.

Akizungumza leo Jumatatu, Desemba 15, 2025, wilayani Kibondo, baada ya kuwapokea wataalamu kutoka Wizara ya Nishati waliotembelea gereza hilo, Mkuu wa Gereza la Kibondo, Peter Shabani, amesema wamechukua agizo la Serikali kama fursa ya ubunifu na kujitegemea kwa kutumia rasilimali zilizopo.

“Baada ya agizo la Serikali la matumizi ya nishati safi ya kupikia, sisi kama Gereza la Kibondo tulilichukulia kama fursa. Kupitia wataalamu tulionao na kwa kushirikiana na wafungwa, tulibuni nishati yetu wenyewe kwa kutumia malighafi tulizonazo ili kupunguza gharama za kuagiza nishati kutoka nje,” amesema Shabani.

Ameeleza mkaa mbadala umebuniwa na wafungwa waliopo gerezani kama sehemu ya programu za urekebishaji tabia, na kwa sasa unatumika kwa matumizi ya ndani pekee kutokana na uhaba wa vifaa vya kisasa vya uzalishaji.

Kwa upande wake, Mtaalamu kutoka Shirika la Viwango Tanzania (TBS), Masumbuko Noha, amepongeza hatua hiyo na kusisitiza umuhimu wa kufuata taratibu na viwango vya TBS endapo gereza hilo litaanza uzalishaji wa nishati hiyo kwa kibiashara.

“Ubunifu huu una tija, lakini ni muhimu kuhakikisha bidhaa inakidhi viwango vya ubora na usalama kabla ya kuanza kuuzwa kwa matumizi ya jamii,” amesema.

Naye mtaalamu kutoka Wizara ya Nishati, Omary Khalifa amesema ubunifu huo ni mfano mzuri wa utekelezaji wa sera ya nishati nchini, akilishauri Jeshi la Magereza Kibondo kuendeleza wazo hilo ili liwe fursa ya kiuchumi na chachu kwa taasisi nyingine.

“Hatua hii inaweza kuwa dira kwa taasisi nyingine nchini kuiga na kuhamasisha matumizi ya nishati mbadala, sambamba na kulinda mazingira na afya za wananchi,” amesema Khalifa.

Septemba 12, mwaka huu, akizindua kongamano la nishati safi ya kupikia lililoandaliwa na Kampuni ya Mwananchi Communications Limited (MCL), Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati, Felchesmi Mramba alisema matumizi ya nishati safi ya kupikia nchini yameongezeka kutoka asilimia 6.9 mwaka 2021 hadi asilimia 20.3.

Mramba alisema lengo la Serikali ni kufikia asilimia 80 ndani ya miaka 10, ambapo hadi sasa imebakia miaka 9.