Jinsi ya kutunza vyakula visiharibike haraka, athari za utunzaji mbovu

Dar es Salaam. Katika mazingira ya sasa, ambako gharama za maisha zimepanda na upatikanaji wa chakula umekuwa mgumu katika baadhi ya maeneo, utunzaji sahihi wa vyakula ni suala lisiloepukika kwa kila kaya.

Baada ya sintofahamu ya Desemba 9 ya uwepo wa maandamano, familia nyingi nchini zilinunua na kuhifadhi vyakula kwa wingi kama hatua ya tahadhari.

Hata hivyo, changamoto inayowakabili wengi sasa ni namna ya kuhakikisha vyakula hivyo haviharibiki kabla ya kutumiwa.

Wataalamu wa lishe na uhifadhi wa chakula wanasema hatua rahisi za kupanga, kusimamia na kutunza vyakula zinaweza kuzuia upotevu mkubwa wa fedha na rasilimali za nyumbani.

Wanashauri kutumia kanuni ya ‘First In, First Out’ (Fifo), ambapo vyakula vilivyonunuliwa mapema vitumike kwanza.

Akizungumza jana, Desemba 14, 2025, kuhusu uhifadhi wa vyakula vinavyotumika majumbani, mshauri wa masuala ya kisera na chakula kutoka Shirika la Kimataifa la Global Alliance for Improved Nutrition (GAIN), Leticia Ishengoma, anasema aina ya chakula na mazingira ndicho kigezo kikuu cha kuchagua mbinu ya uhifadhi.

Anasema katika vipindi vya joto, wadudu huzaliana kwa kasi kubwa endapo nafaka au mikunde haijahifadhiwa kwa usahihi. “Mahindi na maharage yasipotunzwa vizuri, wadudu huweka mayai na baadaye kula chakula hicho, na hapo ndipo sumu mbalimbali hutengenezwa.”

Anaonya pia juu ya hatari ya fangasi na sumu ya aflatoxin, ambayo hujitokeza kwenye chakula kilichohifadhiwa vibaya.

“Aflatoxin ni sumu hatari. Inaweza kusababisha saratani, kuathiri uzazi, waliokula sana sumu hiyo uwezekano wa kuzaa ni mdogo, wanapata uzazi wa shida kwa kuwa na mbegu za kiume zisizobora, na wengine wakipambana na nguvu za kiume. Kwa watoto, huathiri maendeleo ya ubongo na uwezo wa kufikiri,” anasema kwa tahadhari.

Anaonya vikali dhidi ya kutumia chakula kilichoanza kuoza au kuchacha kwa kisingizio cha kuepuka hasara.

“Kula chakula kilichoharibika kunaweza kusababisha magonjwa ya tumbo, kuhara na madhara ya muda mrefu. Kama kuna uwezekano wa kuepuka, ni bora kukitupa,” anasema.

Kwa mujibu wa Ishengoma, kuwekeza katika uhifadhi sahihi wa chakula si tu kunalinda afya ya familia, bali pia kunazuia upotevu wa chakula na hasara za kiuchumi.

Wataalamu wa lishe na uhifadhi wa chakula wanasema hatua rahisi za kupanga, kusimamia na kutunza vyakula zinaweza kuzuia upotevu mkubwa wa fedha na rasilimali za nyumbani.

Wanaeleza zaidi ya asilimia 30 ya chakula kinachonunuliwa majumbani hupotea kutokana na uhifadhi usiofaa, hasara inayoeza kuepukika kwa mbinu rahisi za kila siku.

Wanashauri kutumia kanuni ya ‘First In, First Out’ (Fifo), vyakula vilivyonunuliwa mapema vitumike kwanza.

“Ni muhimu kuandika tarehe juu ya vifungashio ili kutambua kipi kilitangulia. Vyakula vibichi kama samaki, nyama, mboga mboga na matunda huhitaji kuhifadhiwa kwenye friji au friza ili kudhibiti uharibifu wa haraka, hasa katika maeneo yenye joto,” anashauri Ishengoma.

Ishengoma anasema ongezeko la joto na mabadiliko ya tabianchi pia yamechangia kuongezeka kwa kasi ya uharibifu wa vyakula, jambo linalowalazimu wananchi kubadili namna wanavyovitunza ndani ya nyumba.

Kwa vyakula vinavyohitaji ukavu kama nafaka, maharage na karanga, anasema kukausha vizuri kwa jua ni hatua ya msingi kabla ya kuhifadhi.

“Ni muhimu chakula kikauke hadi kufikia kiwango sahihi cha unyevu. Chakula kisipokauka vizuri kina uwezekano mkubwa wa kushambuliwa na wadudu na fangasi,” anafafanua.

Kwa kaya zenye akiba kubwa ya nafaka kama mahindi au mchele, Ishengoma anapendekeza matumizi ya mifuko maalumu ya ‘kinga njaa’ iliyothibitishwa kitaalamu.

“Mifuko hii huzuia hewa na wadudu, hivyo kuhifadhi chakula kwa muda mrefu bila kuathiri usalama wake,” anasema.

Hata hivyo, kwa kaya zisizokuwa na mifuko hiyo, anashauri matumizi ya vyombo visivyopitisha hewa kama ndoo za plastiki zenye vifuniko vinavyofunga vizuri, au makasha yasiyopenya hewa, ili kuepusha wadudu kama funza.

“Mradi chakula kimekauka ipasavyo na hewa haipiti, nafaka kama mchele, unga wa sembe, unga wa ngano na maharage zinahitaji sehemu kavu zisizo na unyevu zinaweza kudumu bila kuharibika,” anasema.

Pia anasema mikate inaweza kudumu wiki moja hadi mbili ikihifadhiwa frijini. Kwa matumizi ya muda mrefu, anashauri kugawa mkate vipande na kuufungia kwenye friza.

Kwa upande wa maziwa na mtindi, ni vyema yahifadhiwe ndani ya friji, si kwenye mlango wa friji ambako mabadiliko ya joto hutokea mara kwa mara.

Ishengoma anasema mboga ambazo hazihitaji friji kama viazi, vitunguu maji na vitunguu saumu zinapaswa kuhifadhiwa katika sehemu kavu na yenye uingizaji hewa, na kwamba kuzihifadhi kwenye plastiki bila hewa husababisha joto na unyevu kujikusanya, hali inayochochea kuoza mapema.

Pia anasema nyama mbichi, kuku na samaki ni miongoni mwa vyakula vinavyoweza kuharibika ndani ya saa machache iwapo havitahifadhiwa kwenye joto sahihi.

Kwa wafanyabiashara sokoni na maghala makubwa, Ishengoma anasisitiza umuhimu wa kuweka magunia juu ya mbao ili kuruhusu mzunguko wa hewa na kuzuia unyevunyevu.

“Kulaza magunia moja kwa moja chini huongeza hatari ya wadudu na kuoza,” anasema.

Kwa upande wake, daktari bingwa wa magonjwa ya wanawake na uzazi, Isaya Mhando, anasema mchele ili udumu kwa muda mrefu ni muhimu kuhifadhiwa kwenye chupa isiyopenya hewa, na vivyo hivyo kwa maharage na vyakula vingine vya nafaka.

“Ili kuhifadhi kwa usahihi, matumizi sahihi ya friji, usafi, na udhibiti wa unyevu ndani ya nyumba ndiyo ngao kubwa dhidi ya uharibifu wa chakula. Kwa kaya nyingi, mbinu hizi rahisi zinaweza kupunguza gharama ya maisha na kuhakikisha usalama wa chakula muda wote,” anasema.