ULE upepo mzuri ilioanza nao Malindi katika Ligi Kuu Zanzibar (ZPL), umekata baada ya kucheza mechi saba mfululizo sawa na dakika 630 bila kuonja ushindi, huku ikielezwa tatizo ni kutimuliwa kwa makocha wasaidizi wawili kikosini.
Mabingwa hao wa zamani wa Tanzania na moja ya timu zilizowahi kutamba katika michuano ya CAF miaka ya 1990, walianza msimu kwa kucheza mechi sita za mwanzo kibabe na kuwafanya wakae kileleni mwa msimamo kwa kukusanya pointi 14 na sasa wameporomoka hadi nafasi ya 10.
Pointi 17 ilizokusanya hivi sasa baada ya kucheza mechi 13, ni sawa na Polisi ambayo ina mechi moja pungufu, hivyo ikishinda au kutoka sare, itaishusha Malindi kwa nafasi moja zaidi na kuwa ya 11 kati ya timu 16 zinazoshiriki ligi hiyo msimu huu.
Mara ya mwisho Malindi kupata ushindi katika ligi hiyo ilikuwa Oktoba 25 ilipoichapa KVZ mabao 3-0, lakini baada ya hapo imeshuka uwanjani mara saba bila ya kupata ushindi, ikiambulia sare tatu na kupoteza nne, vikiwamo vipigo vitatu mfululizo vya mwisho.
Katika mechi hizo saba ambazo Malindi imekata upepo ipo ile dhidi ya KMKM iliyoisha kwa suluhu Novemba 9, kisha suluhu nyingine na Mafunzo (Novemba 13), kipigo cha 3-0 kutoka Mlandege (Novemba 20), sare ya 1-1 na Polisi (Novemba 28) na vipigo vitatu mfululizo vya mabao 2-1 kutoka kwa Muembe Makumbi (Desemba 6), Kipanga (Desemba 11) na New King (Desemba 14).
Timu hiyo kwa sasa imesaliwa na mechi mbili za kufungia mwaka 2025 zote itakuwa nyumbani dhidi ya Zimamoto itakayochezwa Jumapili na ile ya Desemba 26 dhidi ya Uhamiaji kabla ya Ligi kusimama kupisha michuano ya Kombe la Mapinduzi 2026 iliyopangwa kuanza Desemba 28.
Baadhi ya mashabiki wa Malindi wanaamini kuondoka kwa makocha wasaidizi wawili Mohammed Ali ‘Tedy’ na Mohammed Salah ‘Rijkaard’ huenda ni tatizo lililochangia kuyumba kwa timu, japo kocha mkuu wa Malindi, Joseph Mutyaba alisema kinachoitafuna timu hiyo kwa sasa ni wachezaji kucheza wakiwa na presha ya kutafuta ushindi baada ya kuukosa kwa muda mrefu hali inayofanya kupoteza utulivu.
Kocha huyo raia wa Uganda, alisema jukumu lake kwa sasa ni kutumia mbinu mbalimbali ili kuwarudisha wachezaji katika hali ya kawaida, huku akikiri si jambo la kawaida kushindwa kupata ushindi katika mechi saba mfululizo kwa timu iliyozoea kushinda.
“Kila kitu kinawezekana katika mpira mguu, tunachofanya ni kuwatuliza wachezaji na kuwaambia hawapaswi kukata tamaa kwa hali wanayoipitia sasa,” alisema Mutyaba na kuongeza kuwa, Malindi bado ipo vizuri na hivi karibuni mashabiki na wadau wa wataiona ikirudi katika ubora ule wa awali.
Hata hivyo, wakati hayo yakijiri, taarifa za uhakika kutoka ndani ya Malindi zinasema, Mutyaba kwa sasa anafanya kazi bila ya wasaidizi waliokuwapo kikosini hapo ambao ni Tedy na Rijkaard.
Mtoa taarifa huyo alisema makocha hao wameondoka katika timu hiyo na kutafuta changamoto sehemu nyingine huku Rijkaard akiwa ametambulishwa kuwa mkuu wa ufundi wa Annour FC.
Alipotafutwa Ofisa Habari wa Malindi, Namala Suleiman kuzungumzia taarifa hizo, alikiri ni kweli hawapo na timu kwa sasa.
“Kwa sasa hakuna wasaidizi. Makocha wana changamoto za kifamilia. Kocha Tedy ameomba kupumzika ila atarejea na Rijkaard naye ana changamoto,” alisema Namala.
Kwa upande wa Rijkaard, aliliambia Mwanaspoti: “Kwa sasa nipo Annour FC, hao Malindi nimeshamalizana nao kitambo, takribani mechi nne zimepita tangu nimeondoka.”
Huku kwa upande wa Tedy alipotafutwa na Mwanaspoti alisema kwa kifupi; “Sihusiki na chochote kinachohusiana na Malindi, kwani kwa sasa sio kocha msaidizi, niliondoka mapema kabla mambo hayajaharibika.”