Mkataba mpya wa Marekani waanza kuing’ata Kenya

Dar es Salaam. Mahakama ya Kenya imesitisha utekelezaji wa mkataba wa msaada wa afya wenye thamani ya Dola 2.5 bilioni za Marekani (Sh6.13 trilioni) uliosainiwa na Marekani wiki iliyopita, kutokana na hofu kuhusu faragha ya data.

Hatua hiyo inatokana na kesi iliyofunguliwa na kundi la watetezi wa haki za watumiaji likitaka kuzuia kile kinachodaiwa kuwa ni uhamishaji na ushirikishaji wa taarifa binafsi za Wakenya chini ya makubaliano hayo.

Sakata hilo linatokea zikiwa zimepita wiki tatu, tangu wataalamu wa afya ya uzazi nchini Tanzania, kuitaka Serikali kuchukua tahadhari kubwa kabla ya kuridhia mkataba huo, ambao kwa sasa unajadiliwa katika nchi kadhaa za Afrika.

Ingawa hati ya mkataba huo bado haijatolewa hadharani, taarifa kutoka kwa wataalamu wa kikanda zinaashiria kuwa, unaweza kuweka masharti yanayozuia utoaji wa taarifa na huduma muhimu za afya ya uzazi.

Makubaliano hayo ni mkakati mpana wa afya ya kimataifa ambao ni pamoja na utekelezaji wa memoranda of understanding (MoUs) na nchi kadhaa za Afrika, Tanzania ikiwemo.

America First Global Health Strategy ilizinduliwa na Marekani hivi karibuni, miezi michache baada ya Shirika la Marekani la Maendeleo ya Kimataifa (USAID) kufungwa.

Mpango huo unaoweka mwelekeo mpya wa usaidizi wa afya wa kimataifa, badala ya kupeleka pesa za misaada kwa asasi za kiraia, NGO’s na mashirika ya kimataifa, Marekani inataka kufanya makubaliano ya moja kwa moja (bilateral) na serikali za nchi wanufaika.

Marekani tangu wakati huo imeingia mikataba kama hiyo na Rwanda, Lesotho, Liberia na Uganda.

Uamuzi wa muda wa Mahakama unazuia mamlaka za Kenya kuchukua hatua zozote za kutekeleza mkataba huo kadri unavyotoa au kuwezesha uhamishaji, ushirikishaji au usambazaji wa taarifa za kitabibu, za magonjwa (epidemiolojia) au taarifa nyeti za afya za binafsi.

Tangu kusainiwa kwa mkataba huo na Kenya, utawala wa Rais Donald Trump umesaini makubaliano kama hayo na nchi nyingine za Afrika, huku ukibadili mkakati wake wa misaada ya kigeni.

Waziri wa Afya, Aden Duale alisema Desemba 12, Serikali itazingatia uamuzi wa Mahakama, lakini itaendelea kupinga uamuzi huo.

Kwa mujibu wa Duale, uamuzi wa Mahakama unaathiri sehemu za mkataba zinazohusu ushirikishaji wa data pekee, na si mkataba mzima kama ilivyoripotiwa.

“Tunaeleza kwamba, maagizo ya sasa ya zuio yanahusu mahsusi ushirikishaji wa data na hayasitishi ushirikiano mpana zaidi,” alisema Duale.

Chini ya mkakati mpya wa kimataifa wa misaada ya afya, Marekani inapendelea mikataba ya moja kwa moja na Serikali badala ya kupitisha fedha kupitia mashirika ya misaada.

Nchi husika zinatakiwa kuongeza mchango wao katika matumizi ya afya.

Kwa kesi ya Kenya, Marekani inachangia Dola 1.7 bilioni (Sh4.17 trilioni) huku (Sh2.08 trilioni) na kuchukua wajibu mkubwa zaidi hatua kwa hatua.

Katika hafla ya kusainiwa kwa mkataba huo wiki iliyopita, Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani, Marco Rubio, aliuelezea kama mkataba wa kihistoria.

Hata hivyo, Wakenya wengi wameeleza wasiwasi kwamba mkataba huo unaweza kuiruhusu Marekani kuona rekodi binafsi za kitabibu, ikiwamo hali ya mtu kuhusu Virusi vya Ukimwi (VVU), historia ya matibabu ya kifua kikuu (TB) na taarifa za chanjo.

Moja ya makundi yaliyofungua kesi hiyo ni Shirikisho la Watumiaji la Kenya (Cofek), lilidai kuwa Kenya iko katika hatari ya kupoteza udhibiti wa kimkakati wa mifumo yake ya afya, iwapo dawa za magonjwa yanayoibuka na miundombinu ya kidijitali (ikiwamo hifadhi ya data ghafi kwenye mifumo ya wingu) vitadhibitiwa na wahusika wa nje.

Mahakama Kuu ilikubaliana kusitisha utekelezaji wa mkataba huo hadi kesi itakaposikilizwa kikamilifu.

Serikali ya Kenya imekuwa ikijaribu kuwahakikishia wananchi kuhusu mkataba huo.

“Tunasisitiza kwamba mfumo huu uliandaliwa kwa kuzingatia kikamilifu taratibu za kisheria, kuhakikisha kuwa mamlaka ya Kenya, umiliki wa data na haki miliki zinalindwa ipasavyo,” alisema Waziri wa Afya katika taarifa yake ya Ijumaa.

Rais William Ruto alisema Jumatano kuwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali alichambua mkataba huo kwa umakini mkubwa ili kuhakikisha kuwa sheria inayotawala data ya wananchi wa Kenya ni sheria ya Kenya.

Marekani haijatoa maoni kuhusu wasiwasi wa faragha ya data. Kesi hiyo inatarajiwa kurejea mahakamani Februari 12, 2026.

Mkataba unaopendekezwa unaweza kuweka vizuizi katika utoaji wa taarifa za afya ya uzazi, kupunguza huduma zinazoweza kutolewa na hata kuathiri utoaji wa huduma za dharura za baada ya utoaji mimba, ambazo ni halali kisheria na ni muhimu kwa kuokoa maisha.

Katika nchi ambazo mikataba inayofanana imetekelezwa, kumekuwa na mkanganyiko kwa watoa huduma, kupungua kwa elimu ya jamii, kukoma kwa baadhi ya huduma za mkoba na madaktari kuhofu kutoa huduma kamili kwa hofu ya kukiuka masharti ya wahisani.

Wataalamu nchini wamesema iwapo Serikali itasaini mkataba huo, upatikanaji wa uzazi wa mpango unaweza kupungua,  hivyo kuongeza mimba zisizotarajiwa, utoaji mimba usio salama na vifo vya kina mama, hali itakayoongeza mzigo mkubwa kwa mfumo wa afya nchini.

Mkurugenzi Mkaazi wa Shirika la Engender Health Tanzania, Dk Moke Makoma alisema nchi nyingi zikikubali kichwakichwa zinaweza kupata shida, hasa katika uzazi wa mpango na huduma baada ya mimba kuharibika, hivyo njia za kisasa bado ni muhimu.

“Wao kupangilia uzazi si kipaumbele sasa masharti yake yanaweza kupunguza utoaji wa huduma za uzazi, kuongeza vifo vya kina mama na kurudisha nyuma mafanikio yaliyopatikana katika upatikanaji wa uzazi wa mpango,” alisema.

Pia, alisema ikiwa Marekani itapunguza usaidizi wake wa moja kwa moja au kuhamisha mfuko kupitia MoU, kuna hatari kuwa baadhi ya huduma za uzazi wa mpango zitapungua.

Mwakilishi Mkazi wa UNFPA nchini Tanzania, Jacqueline Mahon alisisitiza kuwa, kila dola moja inayowekezwa kwenye uzazi wa mpango inaweza kuokoa hadi dola sita katika gharama za matibabu ya dharura na athari za kijamii na kiuchumi.

Mtaalamu mmoja mwandamizi wa afya ya uzazi nchini aliliambia gazeti hili kuwa, “sera yoyote itakayozuia uzazi wa mpango au huduma za baada ya kutoa mimba, itaongeza moja kwa moja vifo vya akina mama. Wanawake wa vijijini ndiyo watakaoteseka zaidi.”

Wataalamu hao wanaonya kuwa kusaini mkataba wenye masharti kandamizi kutakuwa na madhara makubwa kwa Taifa, ongezeko la mimba zisizotarajiwa, vifo vya kina mama na gharama kubwa kwa mfumo wa afya.

Tanzania inapaswa kusimama imara na kulinda mafanikio yake katika afya ya uzazi ambayo ni msingi wa ustawi wa vizazi vijavyo.