Dar es Salaam. Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, leo Jumatatu, Desemba 15, 2025 imeyaondoa maombi ya kesi ya dhamana iliyokuwa imefunguliwa na waziri wa zamani, Geofrey Mwambe.
Maombi hayo yameondolewa mahakamani hapo baada ya Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam iliyokuwa ikimshikiliwa kwa tuhuma za kijinai kumwachia kwa dhamana.
Hata hivyo kwa mujibu wa Wakili wake, Hekima Mwasipu licha ya Mwambe kuachiwa kwa dhamana, lakini ameongezewa shitaka lingine la kula njama za kutaka kumuua Mkuu wa Jeshi la Polisi.
Mwambe, ambaye amewahi kuwa Mkuu wa Wilaya ya Manyoni, Mkurugenzi wa Kituo cha Uwekezaji (TIC), Mbunge wa Masasi mkoani Mtwara na baadaye Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Uwekezaji na Waziri wa Viwanda na Biashara amekuwa akishikiliwa na Jeshi la Polisi tangu Desemba 7, 2025.
Hata hivyo, Desemba 11, 2025, Mwambe kupitia wakili wake Hekima Mwasipu alifungua shauri la maombi ya dhamana mahakamani hapo dhidi ya Mkuu wa Jeshi la Polisi, Inspekta Jenerali (IGP) na wenzake wawili.
Wajibu maombi wengine katika shauri hilo ni Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP) na Mkuu wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai Kanda Maalumu Dar es Salaam (ZCO).
Katika shauri hilo la maombi namba 289778/2025, lililofunguliwa chini ya hati ya dharura Mwambe anaiomba mahakama hiyo iamuru afikishwe mahakamani na apewe dhamana kwa masharti yatakayowekwa na mahakama hiyo.
Shauri hilo lilipangwa kusikilizwa leo saa 3:00 asubuhi na Hakimu Mkazi Mkuu, Gwantwa Mwankuga, lakini halikuweza kuendelea baada ya mahakama hiyo kufahamishwa kuwa tayari mwombaji alishaachiwa kwa dhamana.
Kwa mujibu wa Wakili wa Serikali Titus Aron, Mwambe aliachiwa kwa dhamana ya Jeshi la Polisi Jumapili ya Desemba 14, 2025.
Wakili Mwasipu ameithibitishia mahakama kuhusu taarifa za kuachiwa mteja wake.
“Mheshimiwa Hakimu ni kweli mwombaji aliachiwa kwa dhamana ya Jeshi la Polisi jana (Jumapili Desemba 14, 2025) asubuhi, kwa mazingira haya tunaomba kuliondoa mahakamani shauri hili,” amesema wakili Mwasipu.
Kutokana na taarifa hizo na maombi ya upande wa mwombaji kuliondoa mahakamani shauri hilo, mahakama imeridhia ya kuamuru kuwa shauri hilo limeondolewa rasmi mahakamani.
Desemba 12, 2025, Kamanda wa Polisi, Kanda Maalum ya Dar es Salaam, Jumanne Muliro alitoa taarifa kwa umma ikieleza kumshikiliwa Mwambe kwa tuhuma za jinai ambazo walikuwa wanaendelea kuzichunguza.
Muliro alisema waliomkamata Mwambe usiku wa Desemba 7, 2025 eneo la Tegeta jijini Dar es Salaam.
Alichokisema Mwasipu na nyongeza ya tuhuma
Akizungumza na wanahabari baada ya kutoka mahakamani, Wakili Mwasipu amedai kuwa Mwambe alipokamatwa alihojiwa kwa tuhuma za uchochezi wa kimtandao, lakini kwa sasa anakabiliwa na tuhuma mbili baada ya kuongezewa nyingine ya njama za kutaka kumuua Mkuu wa Jeshi la Polisi.
“Tuhuma kuu zinazomkabili ni mbili, kwanza anatuhumiwa kula njama za kutaka kumuua Mkuu wa Polisi lakini hawajaeleza ni mkuu gani na tuhuma ya pili ni uchochezi wa kimtandao, ambao pia hawajaufafanua.
“Tulifungua shauri la kuomba dhamana baada ya kushikiliwa kwa kinyume cha sheria kwa zaidi ya saa 24. Shauri lilikuwa limepangwa kusikilizwa leo lakini jana saa tatu asubuhi aliachiwa kwa dhamana ya Jeshi la Polisi na leo tumekwenda kuripoti polisi.”
Wakili Mwasipu amesema bado Jeshi la Polisi linaendelea na upelelezi wa tuhuma hizo na kwamba, ametakiwa kuripoti tena Ofisi ya ZCO, Jumanne ya juma lijalo.
Kwa mujibu wa hati ya kiapo kilichokuwa kinaunga mkono maombi hayo aliyokuwa ameyafungua, Mwambe alikamatwa katika makazi yake eneo la Tegeta (Wilaya ya Kinondoni) jijini Dar es Salaam, usiku wa tarehe hiyo na watu waliojitambulisha kama maofisa wa Polisi.
Baada ya kukamatwa usiku huo alipelekwa katika kituo cha Polisi Mbweni, ambako alihojiwa kwa tuhuma za uchochezi.
Kisha alihamishiwa kituo kikuu cha Polisi kwa usimamizi wa mjibu maombi wa tatu (ZCO) ambako alihojiwa kwa mara ya pili kuhusu tuhuma za uchochezi na baada ya mahojiano hayo ya pili, Mwambe siku hiyohiyo alipelekwa mahabusu katika kituo cha Polisi Kigamboni.
Desemba 8, 2025 wakili Mwasipu alikwenda na kuzungumza naye katika kituo cha Polisi Kigamboni, ambapo Mwambe alimsimulia mateso aliyopitia pamoja na kunyimwa dhamana ambayo ni haki yake ya Kikatiba na kwamba tangu tarehe hiyo alipokamatwa amekuwa kizuizini kinyume na sheria.
“Sheria inaelekeza kuwa mtuhumiwa lazima afikishwe mbele ya mahakama ya sheria ndani ya saa 24 tangu kukamatwa. Amekuwa kizuizini kwa zaidi ya saa 24. Mwombaji amekuwa kizuizini kwa zaidi ya siku nne sasa (Desemba 11) bila sababu yoyote ya msingi au maelezo kutoka kwa wajibu maombi,” inasomeka hati hiyo na kuongeza:
“Mwombaji ana haki ya kikatiba ya uhuru wa kutembea, haki ya kuishi kama mtu huru, na haki ya dhamana. Alinielekeza kuomba dhamana katika mahakama ya sheria ili kuhakikisha uhuru wake.”
Katika hati ya dharura, Wakili Mwasipu anathibitisha kuwa uamuzi wa maombi hayo unahitaji kushughulikiwa kwa dharura sana.
Anafafanua mwombaji amekamatwa na kushikiliwa kinyume cha sheria kwa zaidi ya siku nne sasa (Desemba 11), bila kupewa dhamana ya polisi au kufikishwa mahakamani ili kushughulikiwa kwa mujibu wa sheria.
Pia anadai kuwa mwombaji ameshikiliwa na kunyimwa dhamana ya polisi bila sababu au maelezo yoyote halali kutoka kwa mjibu maombi wa kwanza (IGP) na wa tatu.
Vilevile wakili Mwasipu anadai katika hati hiyo ya dharura kuwa kushikiliwa huko kunamsababishia madhara makubwa kuliko manufaa, hususan ikizingatiwa kuwa mwombaji si mtu mwenye vurugu na hajawahi kuonesha dalili zozote za kutumia nguvu.
Desemba 11, Wakili Mwasipu alilieleza Mwananchi kuwa baadaye Mwambe alihamishwa kutoka kituo cha Polisi Kigamboni na kupelekwa mahali ambako hawakupafahamu, amehamishwa kutoka katika kituo cha Polisi Kigamboni alikokuwa anashikiliwa na kwamba hawajui amepelekwa wapi.
“Leo asubuhi familia ilimpelekea chakula wakaambiwa kuwa hayupo wameshamtoa, sasa mpaka sasa hivi hatujui yuko katika kituo gani cha Polisi. Tunazidi kufuatilia pamoja na familia ili kujua amepelekwa kituo gani cha polisi,” amesema wakili Mwasipu.
