KIKOSI cha Yanga bado kipo mapumziko kupisha fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika (Afcon) 2025 zinazoanza wikiendi hii huko Morocco, lakini kuna hesabu mpya ndani ya timu hiyo zinapigwa sasa ambazo zimelazimika kubadilishwa kutokana na maendeleo ya straika Clement Mzize.
Mzize yupo nje ya uwanja kwa muda mrefu kutokana na kuumia, japo hivi karibuni alionekana kuanza mazoezi mepesi, lakini ukweli ni kwamba straika huyo aliyemaliza kinara wa mabao wa klabu wa msimu uliopita wa Ligi Kuu kwa kufunga mabao 14 mambo yametibuka na kuulazimisha uongozi kurudi tena sokoni fasta kuangalia mashine nyingine ya kufunga mabao.
Taarifa kutoka ndani ya Yanga ni kwamba presha kubwa kwa Mzize ni kwamba anaweza kuanza mazoezi kamili mwisho wa Februari mwakani au wiki ya kwanza Machi ambapo madaktari wa timu hiyo hawataki kuharakisha mshambuliaji huyo kurudishwa mapema.
Bosi mmoja wa Yanga, ameliambia Mwanaspoti kuwa Mzize jeraha alilonalo lilikuwa hatarishi na kwamba hata upasuaji wake ulihitaji umakini ambapo sasa anaendelea vizuri, lakini hawaoni kama anaweza kuwa sawa haraka kwani anahitaji muda kupona vizuri.
Hesabu hizo zimewalazimisha mabosi wa Yanga na hata makocha kuanza kuangalia upya kutafuta mshambuliaji mwingine wa maana ambaye atakuja kusaidiana na Prince Dube ambaye kocha Pedro Goncalves hana shida naye.
Yanga inatafuta mshambuliaji mpya ili awahi mechi zijazo za Ligi ya Mabingwa Afrika ambapo wakirudi tu, wanatakiwa kuwafuata Al Ahly ya Misri Januari 23, 2026 kisha timu hizo kurudiana tena Januari 30, 2026 hapa nchini.
Endapo Yanga itasajili mshambulaiji mpya, inaweka hatarini nafasi ya mshambuliaji Andy Boyeli ambaye bado ameshindwa kuonyesha makali yake huku pia akikosa mechi nyingi za kuanza, akitokea zaidi benchini.
“Kocha (Pedro) anamfahamu Mzize vizuri, wote tulikuwa tuna imani kwamba atarudi haraka, lakini kwa namna tulivyopokea ripoti yake kuna uwezekano tukahitaji muda zaidi kumsubiri apone sawasawa,” amesema bosi huyo.
“Kama Mzize angekuwa na uwezekano wa kuwahi mapema kocha aliamini kwamba tungekuwa tumepata mtu sahihi mwenye kasi lakini pia anaweza kufanya kitu kikubwa kwenye mechi kubwa kama hizi zijazo. “Tunatafuta mshambuliaji mwingine wakati tukimsubiri Mzize apone sawasawa, hizi mechi zilizosalia zina uzito mkubwa, tunatakiwa kuwa na watu bora zaidi ambao wataamua hizi mechi, tunataka kabla ya mechi za makundi tuwe tumepata mtu ili akaanze kuzoea presha ya timu kwenye mashindano haya.”
Mbali na mshambuliaji huyo Mwanaspoti linafahamu kuwa Yanga pia inahaha sokoni kusaka kiungo mshambuliaji wa maana yaani namba kumi kuja kuongeza nguvu kwenye timu hiyo ukiwa ni msisitizo wa kocha wa timu hiyo Pedro.
Yanga inaona bado kuna wasiwasi juu ya ubora na Mamadou Doumbia ambaye hana asisti wala hajafunga na Lassine Kouma mwenye bao moja ambao mpaka sasa hawajaonyesha maajabu makubwa kama ambavyo ilitarajiwa kabla.
Licha ya kwamba kumekuwa na usiri juu ya straika mpya anayewindwa na Yanga, lakini duru za kispoti zinadokeza kuwa, Laurindo Dilson Maria Aurelio ‘Dupe’ kutoka Angola yupo katika hesabu hizo, lakini ikielezwa kuna straika mwingine kutoka DR Congo naye anaviziwa kuletwa Jangwani.
Dupe mwenye umri wa miaka 25 aliyewahi kuzitumikia Sagrada Esperanca na Petro Atletico zote za Angola na kuwa Mfungaji Bora wa michuano ya Kombe la Cosafa misimu miwili mfululizo ya 2024 na 2025 kwa sasa yupo Radomiak Radom ya Poland.
