NAIBU WAZIRI KIHENZILE AFUNGUA MKUTANO WA 18 WA PAMOJA WA MAPITIO YA SEKTA YA USAFIRISHAJI

Naibu Waziri wa Uchukuzi, Mhe. David Kihenzile, Disemba 15, 2025 amefungua rasmi Mkutano wa 18 wa Pamoja wa Mapitio ya Sekta ya Usafirishaji unaofanyika katika Ukumbi wa AICC jijini Arusha.

Akizungumza wakati wa ufunguzi, Mhe. Kihenzile alisema kaulimbiu ya mkutano huo isemayo “Integrated Transport System as a Foundation for Economic Transformation Toward Vision 2050” inaonesha nafasi ya sekta ya usafirishaji kama nguzo muhimu ya mabadiliko ya kiuchumi na utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050.

Ameongeza kuwa Serikali itaendelea kuimarisha mfumo jumuishi wa usafirishaji unaounganisha barabara, reli, bandari, usafiri wa anga, maji, pamoja na kukamilisha na kupanua miradi mikubwa ya miundombinu ikiwemo reli ya kisasa (SGR) ambayo sasa inaenda mpaka nje ya nchi, bandari, ununuzi wa ndege na uboreshaji wa viwanja vya ndege, huku akihamasisha ushiriki wa sekta binafsi.

Upande wa meli amesema Serikali inaendelea na ukarabati wa meli zilizopo, ujenzi wa meli mpya na kiwanda cha kutengeneza meli hali itakayochochea muunganiko na ukuaji wa uchumi kikanda vilevile amewapongeza LATRA na TASAC kwa mifumo imara ya udhibiti wa usafiri ardhini na majini

Aidha, amesema Serikali inaendelea kukuza usafiri wa reli na biashara ya kikanda kupitia uboreshaji wa reli ya TAZARA hali ambayo itaongeza uwezo wa kuhudumia mizigo na kupunguza muda wa ushughulikiaji wa shehena.

Kwa upande wake, Katibu Mkuu wa Wizara ya Uchukuzi Prof. Godius Khayarara amesema mkutano huo ni jukwaa muhimu la kutathmini utekelezaji wa mipango ya sekta ya usafirishaji na matokeo yake yatasaidia kuboresha sera, mipango na uwekezaji wa Serikali.

Awali, Kaimu Mkurugenzi wa Ufuatiliaji na Tathmini kutoka Wizara ya Uchukuzi alisema mkutano huo unalenga kufanya tathmini ya utekelezaji wa miradi na programu za sekta ili kubaini mafanikio, changamoto na kuweka mikakati ya kuboresha utekelezaji kwa kuzingatia thamani ya fedha.

Mkutano wa 18 wa pamoja wa mapitio ya sekta ya Uchukuzi utafanyika kwa siku tatu kuanzia tarehe 15 mpaka 17 Desemba, 2025 ambapo unatarajiwa kutoa mapendekezo muhimu yatakayosaidia kuboresha Sera.

Naibu Waziri wa Uchukuzi, Mhe. David Kihenzile akikagua mabanda ya taasisi mbalimbali zilizoshiriki Mkutano wa 18 wa Pamoja wa Mapitio ya Sekta ya Usafirishaji unaofanyika katika Ukumbi wa AICC jijini Arusha.
Naibu Waziri wa Uchukuzi, Mhe. David Kihenzile akisoma hotuba ya ufunguzi wa mkutano wa 18 wa Pamoja wa Mapitio ya Sekta ya Usafirishaji unaofanyika katika Ukumbi wa AICC jijini Arusha.

Katibu Mkuu wa Wizara ya Uchukuzi Prof. Godius Khayarara akizungumza jambo wakati wa mkutano wa 18 wa Pamoja wa Mapitio ya Sekta ya Usafirishaji unaofanyika katika Ukumbi wa AICC jijini Arusha.

Baadhi ya wadau wa usafiri wakifuatilia hotuba ya mgeni rasmi Naibu Waziri wa Uchukuzi, Mhe. David Kihenzile wakati wa ufunguzi mkutano wa 18 wa Pamoja wa Mapitio ya Sekta ya Usafirishaji unaofanyika katika Ukumbi wa AICC jijini Arusha.