Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Mhe. Wanu Hafidh Ameir, amemtaka Mkandarasi wa COMFIX & ENGINEERING kuongeza kasi ya ujenzi wa miundombinu ya Mradi wa Kujenga Ujuzi na Ushirikiano Afika Mashariki (EASTRIP ) katika Taasisi ya Teknolojia Dar es Salaam (DIT) Kampasi ya Mwanza, ili ikamilike kwa wakati kulingana na maktaba.
Naibu Waziri huyo, ametoa maagizo hayo jijini Mwanza wakati akikagua maendeleo ya utekelezaji wa mradi huo. Pia amewataka wazabuni wote kuhakikisha vifaa na mitambo vinawasili na kufungwa kwa wakati ili kuwezesha utoaji wa mafunzo kwa wakati.
Mhe. Wanu Ameir amesema ucheleweshaji wa ujenzi unaweza kuathiri malengo ya Serikali ya kuhakikisha vijana wanapata ujuzi na umahiri unaohitajika katika soko la ajira la ndani na kimataifa, kama alivyoelekeza Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Mhe. Ameir amewahakikishia wananchi na uongozi wa DIT kuwa Serikali itaendelea kuimarisha uwezo wa kampasi hiyo, ikiwemo kuongeza udahili wa wanafunzi kutoka 358 wa sasa hadi 2,000
Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, Prof. Daniel Mushi, amesema kuwa katika Kampasi ya DIT Mwanza kinajengwa Kituo cha Kikanda cha Umahiri cha uchakataji na utengenezaji wa bidhaa za Ngozi ambacho kinatekelezwa kupitia Mradi wa EASTRIP. Amesema kuwa ujenzi huo unahusisha majengo matano ambayo ni jengo la kufundishia, jengo la taaluma, hosteli mbili na karakana ya kisasa kwa ajili ya mafunzo ya utengenezaji wa bidhaa za ngozi.
Prof. Mushi ameongeza kuwa ujenzi wa majengo hayo unatekelezwa na Serikali kwa kushirikiana na Benki ya Dunia ambayo imetoa mkopo wa riba nafuu kufanikisha mradi huo. Ambapo gharama za utekelezaji wa mradi DIT Mwanza ni shilingi bilioni 37.
Mkurugenzi wa Taasisi ya Teknolojia ya Dar Es Salaam (DIT) Kampasi ya MWANZA Dkt. John Msumba amesema kuwa Kampasi hiyo imefufua Sekta ambayo ilikuwa imekufa nchini kutokana na kukosekana Kwa wataalamu na kwamba Viwanda Kwa sasa vinapata wataalamu tofauti na awali ambapo walikuwa wakilazimika kuwatoa nje ya nchi.
