Rushwa barabarani bado mwiba | Mwananchi

Dar es Salaam.  Licha ya hatua na marufuku zilizowahi kutolewa na Serikali dhidi ya rushwa barabarani, vitendo hivyo vimeendelea kuota mizizi kwa askari wa usalama barabarani na madereva.

Madereva wa magari hasa ya biashara wanakiri kutoa rushwa kwa askari hao wakisema imeshageuka kuwa mfumo wa maisha ya kazi yao na kuna athari ukiiepuka kuliko kujihusisha nayo.

Baadhi ya askari, wanasema yapo mazingira yanayowalazimu kujihusisha na vitendo hivyo, ikiwamo magari yanayostahili adhabu kumilikiwa na wakubwa ndani ya Serikali, hivyo bora wapokee chochote kitu kuliko kulazimisha kutoza faini itakayogharimu kazi yao.

Katikati ya hoja hizo, Serikali inasema ili kuikabili rushwa barabarani, inapaswa kuanza na madereva kuacha kutenda makossa kwa kuwa, kutaziba mianya ya kutoa na kuombwa rushwa.

Mitazamo hiyo inakuja siku mbili tangu ishuhudiwe picha jongefu ya askari wa usalama barabarani, mkoani Iringa anayeomba Sh10,000 kwa dereva ili amrudishie leseni yake.

Desemba 13, mwaka huu, Jeshi la Polisi lilitangaza limeshamchukulia hatua askari huyo kwa mujibu wa sheria, baada ya kuona picha hiyo ya mjongeo.

Askari huyo alionekana akiomba leseni ya dereva aliyekuwa raia wa kigeni, kisha kumuomba ampe Sh10,000 aliyodai ya soda.

Hata hivyo, dereva huyo hakumpa kiasi hicho cha fedha zaidi ya kumweleza kuwa, kufanya hivyo ni kutoa rushwa na kwamba ni kosa kisheria.

Kelele kuhusu rushwa katika sekta ya usafiri hasa wa barabara hazikuanza sasa, zilianza kitambo na ripoti ya Jeshi la Polisi Kikosi cha Usalama Barabarani ya 2023/2024 inalithibitisha hilo.

Ripoti hiyo inaeleza kuwa, katika kipindi cha Juni 2023 hadi Juni 2024, askari 168 wa usalama barabarani walichukuliwa hatua kwa makosa mbalimbali yakiwamo ya rushwa.

Miongoni mwao, wapo walioshitakiwa kijeshi, waliohamishwa vituo vya kazi na wengine kufukuzwa kazi kutoka katika jeshi hilo.

Katika kudhibiti matukio hayo, Mei 11, mwaka jana aliyekuwa Makamu wa Rais, Dk Philip Mpango alisema tayari Serikali ilishakuwa na mpango wa kuwavalisha majaketi yenye kamera ‘Body Cam Jackets’ askari wote wa usalama barabarani.

Kamera hizo, alisema zitawezesha kuonekana na kusikika kile askari hao wanachozungumza na madereva barabarani, hivyo kuziba mianya ya kuomba na kupokea rushwa.

Akizungumza leo Jumapili Desemba 14, 2025, Mwenyekiti wa Umoja wa Madereva Tanzania, Majura Kafumu amesema rushwa kwa madereva  vyombo vya usafiri hasa vya biashara imeshakuwa kama mtindo wa maisha ya kawaida.

Hilo linatokana na kile alichoeleza, madereva wanalazimishwa na kulazimika kutoa rushwa, kwa sababu hawana chaguo zaidi ya kujihusisha na vitendo hivyo.

Katika ufafanuzi wake, amedai kuwa, ikitokea dereva amegoma kutoa rushwa, atabambikiwa makosa zaidi na kuandikiwa faini kubwa itakayomgharimu fedha nyingi kuliko angekitoa rushwa.

“Askari ana nguvu na mamlaka ya kukuandikia makosa hata bila uthibitisho, anaweza kuamua kukuandikia tu kukukomesha kwa sababu umekataa kumpa rushwa. Kuliko utozwe faini ya Sh60,000 dereva anaona bora ampe rushwa ya Sh10,000,” amesema.

Pia, amesema madereva wengi waliogoma kutoa rushwa wamefukuzwa kazi na mabosi zao, baada ya kuripotiwa kuwa hawatoi ushirikiano kwa askari wa usalama barabarani.

“Mimi nina kesi za madereva waliofukuzwa kazi kwa sababu waligoma kutoa rushwa na askari wakawaripoti kwa wamiliki wa kampuni za usafirishaji. Mtu kuliko akose kazi anaona bora atoe hiyo rushwa,” amesema.

Kafumu amesema kwa mazingira kuanzia sheria na taratibu, dereva amenyimwa nafasi ya kuiepuka rushwa, kwa sababu askari ana mamlaka na nguvu zaidi dhidi yake.

“Ukiwa dereva huna pa kuikwepa rushwa, huna wa kumlalamikia, ukimripoti askari unageukwa wewe. Yaani hatuana cha kufanya ni kutoa rushwa,” amesema.

Pia, amesema anazo kesi za madereva waliofungiwa leseni kwa muda kadhaa kwa sababu tu wamegoma kutoa rushwa na wengine wamewaripoti askari waliowaomba.

“Sasa fikiria dereva ana familia, asipotoa rushwa anafungiwa leseni kwa muda fulani, kwa hiyo hatafanya kazi kwa muda huo. Watoto watakula nini, wataishi vipi, lazima tutoe rushwa ili tuishi,” amesema.

Ameeleza mwenendo huo umefanya madereva waone rushwa kuwa sehemu ya maisha yao ya kazi, hivyo bila kujali wamekosea au hawajakosea wanalazimika kutoa.

Mbali na hilo, amesema tatizo lingine linaanzia kwenye utaratibu wa askari kujikita zaidi kwenye kuadhibu kuliko kufunza na kuonya.

“Tunagugumia mioyoni na hata nikisema nikashitaki, ni mimi ndiye nitakayefukuzwa kazi na matajiri wanaambiana kwamba huyu dereva hafai kabisa hivyo hupati kazi popote,” amesema.

Amesisitiza kuwa, anaona bora atoe kiasi kidogo cha fedha kama rushwa kuliko kukataa akose kazi kabisa, kwa sababu hawatoi kwa hiari bali wanalazimika.

“Sio siri rushwa zipo na tunalazimishwa kuzitoa. Wanakupiga tochi lakini ukienda na Sh5,000 wanakuachia unaondoka,” amesema Kafumu.

Katika maelezo yake, amesema wapo askari wanaolalamikia madereva kuingiza barabarani magari mabovu, ilhali yamepewa vibali na mamlaka kutembea.

Hata hivyo, amesema barabara nazo zinachangia uharibifu wa magari kwa kile alichoeleza nyingi hazikidhi mahitaji.

Mmoja wa askari wa usalama barabarani aliyezungumza kwa sharti la kutotajwa jina, amesema kama wanavyolalamika madereva, ndivyo ilivyo kwa askari kwa kuwa nao wanalazimika kupokea.

Ulazima wa kupokea rushwa kwa askari unatokana na kile anachoeleza, wanaposimamia haki kwa kuwatoza faini wakosaji barabarani, wakati mwingine mambo huwageukia.

“Unakuta unamtoza faini dereva au unasema hii gari haiwezi kutembea ni mbovu, dereva anapiga simu mbili tatu, unakuta unaletewa simu uongee, kumbe mmiliki wa gari ni mkubwa unakosa namna unaruhusu,” amesema.

Katika mazingira hayo, amesema wanakosa ari ya kuifanya kazi kwa namna inavyopaswa na ukizingatia taratibu za kazi yao, mkubwa akielekeza ni vigumu kupingana naye.

“Hivi mwandishi unajua kuna askari wamewahi kuadhibiwa kwa kuonewa, tu kwa sababu walisimamia sheria? Haya ndio maisha yetu ya kazi ndugu yangu. Mambo ni mengi,” amesema.

Askari mwingine, amesema rushwa imeshaota mizizi kwenye sekta hiyo kwa sababu mnyororo wa wapokeaji wake ni mrefu, ingawa walio chini ndio wanaoonekana.

“Sisi wa barabarani tunaonekana zaidi, lakini sio kila unachokipokea cha kwako, nyingine unapeleka kwa ambaye haonekani barabarani,” amesema.

Alipotafutwa kuzungumzia hilo, Mkuu wa Polisi Kikosi cha Usalama Barabarani, William Mkonda simu yake iliita bila kupokewa.

Hata alipotafutwa mwanasheria wa kikosi hicho, Mussa Manyama alisema hana mamlaka ya kuzungumza kwa niaba ya kikosi hicho.

Alipoulizwa kuhusu mazingira hayo ya rushwa barabarani, Waziri wa Mambo ya Ndani, George Simbachawene amesema vitendo hivyo vinavunja na kukiuka misingi ya utawala bora, hivyo lazima kupingana navyo.

Amesema mzizi wa rushwa barabarani ni kutenda makosa, iwapo ingetokea watu hawakosei kusingekuwa na mwanya kwa askari kuomba kitu.

“Kama watenda makosa wanakuwa wengi maana yake na ushawishi wa rushwa unakuwepo pale pale. Wananchi wanaweza wakawa wachochezi zaidi wa kuwapa rushwa askari kuliko askari kuomba rushwa, kwa sababu wao ndio wakosaji,” amesema.

Hata hivyo, amesisitiza lazima apambane kuhakikisha anashughulikia na kukomesha vitendo hivyo, kwa kuwa vinakwenda kinyume na misingi ya utawala bora.

Kuhusu majaketi yenye kamera kwa askari wa usalama barabarani, Simbachawene amesema Jumanne ya Desemba 16, anatarajia kukutana na wadau wa masuala hayo kujua hatua zilizofikiwa.

“Nina kikao Jumanne kuhusu masuala ya usalama barabarani na kuna wadau wengi tutakutana nao. Kusema ukweli sikuwa nimepata mrejesho kuhusu mambo ya majaketi na natarajia nitaupata kupitia kikao hicho,” amesema.

Hata hivyo, ameeleza kwa kipindi kifupi tangu ameingia kwenye nafasi hiyo amebanwa zaidi na masuala ulinzi kutokana na vurugu zilizotokea na zinazopangwa na sasa atapata nafasi ya kugeukia maeneo mengine.