Serikali, kampuni za simu wabanwa kuzima intaneti

Dar es Salaam. Hatua ya Serikali kuzima Intaneti kwa siku saba kuanzia Oktoba 29, 2025 inazidi kupingwa baada ya Chama cha Wanasheria wa Tanganyika (TLS) na wanaharakati wamefungua kesi ya kikatiba Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam.

Hii inakuwa kesi ya pili baada ile iliyofunguliwa na Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC) katika Mahakama ya Afrika Mashariki (EACJ), kikidai kuzimwa kwa Intaneti kulikiuka vifungu 6(d), 7(2) na 8(1(c) vya Mkataba wa Afrika Mashariki.

Katika kesi mpya iliyofunguliwa na TLS kama mleta maombi wa kwanza na wanaharakati Bob Chacha Wangwe, Twaha Mwaipaya na Kumbusho Dawson kama waleta maombi wa 2,3,4, ni dhidi ya Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari.

Wajibu maombi wengine katika kesi hiyo inayosimamiwa na mawakili Jebra Kambole, Mpale Mpoki na Hekima Mwasipu ni Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) kama mjibu maombi wa pili na kampuni nne binafsi ya simu nchini.

Kampuni hizo ni Vodacom Tanzania Public Limited, Airtel Tanzania Public Limited, Honora Tanzania PLC ‘Mixx by Yas’, Viettel Tanzania PLC maarufu ‘Halotel’ na pia Shirika la Mawasiliano Tanzania (TTC) ambalo ni la umma limeunganishwa.

Lakini walalamikaji pia wamemuunganisha Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG) na wanaiomba mahakama itoe amri za mambo 10 dhidi ya kuzimwa intaneti kuanzia Oktoba 29, 2025 saa 5:00 asubuhi hadi Novemba 4, 2025 saa 11 jioni.

Katika shauri hilo lililofunguliwa Desemba 11, 2025 na kusajiliwa namba 000031421/2025, mahakama inaombwa itamke kuwa kuzimwa huko kwa intaneti kulikiuka ibara 10 za Katiba ambazo ni 13(6), 14, 15(1), 17(1), 18, 19(1), 20(1), 21(1), 26(1 na 29.

Pia wanaiomba mahakama itamke kuwa kuzimwa kabisa (total shutdown) kwa intaneti ni dhihirisho lisilofuata fundisho la uhalali, uwiano na umuhimu, kwa kuwa halina msingi ulio wazi, mahususi na unaokubalika kikatiba.

Pia wanaomba Mahakama Kuu itamke kuwa kuzimwa huko kabisa kwa mtandao kulikofanywa na mleta maombi wa 1 hadi wa 7 kulisababisha madhara makubwa kwa haki za wananchi kiuchumi, kijamii, kisiasa na kiraia.

Mbali na hayo, wanaomba mahakama itamke kuwa mjibu maombi wa kwanza (waziri), wa pili (TCRA) na wa nane ambaye ni AG, walikiuka wajibu wao wa kulinda umma, watu na haki zao zinazolindwa na Katiba na mikataba ya kimataifa.

Wanaiomba mahakama pia itoe amri ya zuio la kudumu kuwazuia wajibu maombi, mawakala wao au mtu mwingine yeyote, kuzima intaneti na huduma ya data kwa simu za kiganjani au kuzuia kufikiwa kwa mitandao ya kijamii.

Waleta shauri hilo wanataka wajibu maombi wasizime intaneti na huduma ya data bila kuwapo kifungu mahsusi cha sheria iliyotungwa na Bunge, kinachowapa mamlaka hayo au bila kuwapo kwa amri kutoka mahakama ya sheria.

Halikadhalika, wanaiomba mahakama itoe amri kwa wajibu maombi kutoa tangazo kupitia vyombo vya habari na mitandao ya kijamii, la kuwaomba radhi Watanzania wote na mataifa mengine duniani kwa kukiuka haki za kikatiba walipozima intaneti.

Kama haitoshi, wanaiomba itoe amri kwa wajibu maombi kutoa hakikisho la maandishi kupitia vyombo vya habari na mitandao ya kijamii, kwamba kamwe hawatarudia kuzima intaneti, kupunguza kasi yake wala kuzuia baadhi ya anuani za IP au IP Addresses.

Sababu za kufungua shauri

Kulingana na nyaraka za shauri hilo zilizowasilishwa mahakamani kupitia mfumo wa e-Services Portal, waleta shauri wanadai kuzimwa kwa intaneti kulikuwa hakuna msingi wowote na kulizuia mamilioni ya watu kuwasiliana.

Waleta shauri wanadai uamuzi wa wajibu maombi kuzima mtandao wa intaneti waliufanya bila kuwapo kifungu cha sheria kinachowaruhusu kufanya hivyo na kwamba TCRA haikutimiza wajibu wake wa kulinda umma na usumbufu huo.

Wanadai sheria ya kupata taarifa (Access to Information Act), inatoa fursa ya watu kupata taarifa na sheria ya makosa ya kimtandao inawazuia wajibu maombi wa 1 hadi 7 kuingilia mifumo ya kompyuta, lakini wao walipuuza na kuzima intaneti.

Wajibu maombi hao, wa kwanza 1 hadi saba wanalalamikiwa kwa kuamua kuzima intaneti kabla ya kutoa taarifa kwa umma na wateja wa makampuni ya simu za mkononi walijikuta katika mshangao kwa vile hapakuwepo notisi ambayo ingewaandaa.

Wanalalamika kulikuwa hakuna umuhimu wowote wa kuzima intaneti katika nchi ya kidemokrasia, hususan wakati upigaji wa kura katika uchaguzi unaobishaniwa ukiendelea na intaneti ilihitajika kurahisisha uhakiki na mawasiliano.

Kwa mujibu wa walalamikaji, mawasiliano ya intaneti yalihitajika sana kusaidia kuhakiki wapiga kura kwenye mfumo, mawasiliano na vituo vya ujumlishaji, kazi ambayo isingewezekana kufanyika pasipokuwepo mtandao wa intaneti.

Pia wanadai utaratibu wa kuzima intaneti ikiwamo kutoa notisi hazikufuatwa wala sababu za kufanya hivyo hazikutolewa kwa watumiaji na muda wa kuzima haukuwa sahihi kutokana na uwepo wa ‘lockdown’, ukiukwaji wa haki na maandamano.

“Kwamba kuzimwa kwa intaneti kuliminya taarifa muhimu za umma kwa ujumla kuhusu afya ya umma na usalama wakati wa tukio muhimu la kitaifa, kwani idadi kubwa ya watu wanategemea intaneti kupata habari na kupata dawa muhimu,” wanadai.

Wameongeza kudai: “Kuzimwa kwa mtandao kulisababisha mwingiliano mkubwa wa shughuli za kiuchumi na biashara ikijumuisha mauzo ya mtandaoni, utangazaji, uuzaji wa bidhaa na huduma na kuathiri wote wanaotegemea mitandao.”

Wanalalamika katika shauri hilo kuwa kitendo cha wajibu maombi kuzima intaneti hakikuzingatia ukubwa wa athari zake ikiwamo kuathiri uchumi, taasisi za fedha ambazo hazikufanya kazi, hospitali na maduka ya dawa hayakufanya kazi.

Katika shauri hilo ambalo bado halijapangiwa majaji wa kulisikiliza wala tarehe ya kusikilizwa, waombaji wameorodhesha maeneo kadhaa ya ukiukwaji wa Katiba.

Wanadai kuzima Intaneti kulikiuka Ibara ya 12(1) na (2) kwani kulidhoofisha utu wa asili wa kila mtu kwa kukata kiholela mawasiliano ya katika kupokea kupokea, kusambaza na kubadilishana habari, na kushiriki mambo ya kijamii na ya umma.

Pia wanadai kitendo hicho kilikiuka Ibara ya 13(1(a) kwa kuzima Intaneti bila kutoa notisi yoyote kwa umma wala kutoa sababu za kufanya hivyo, wala bila kuwepo amri yoyote ya mahakama bila kusikiliza upande wa waathirika.

Kwa kuegemea Ibara ya 14, walalamikaji wanadai kitendo cha wajibu maombi kuzima Intaneti kilikuwa ni haramu kisheria na hiyo ilisababisha watu wengi kupoteza maisha kwa kupigwa risasi kwa kuwa hawakuwa na taarifa yoyote.

Pia kwa kuegemea ibara hiyo hiyo, wanadai majeruhi wengi wa risasi wangeweza kuita usafiri au kuomba msaada, lakini walishindwa kutokana na vizuizi vilivyokuwepo, hivyo kuzimwa intaneti kuliwanyima haki ya kikatiba ya kuishi.

Wakiegemea ibara ya 17(1), wanadai kuzimwa kwa intaneti kulizuia uhuru wa kutembea, kwa ni ilikuwa ni vigumu kuita huduma ya usafiri wa kukodi kama Bolt, Uber na watu walishindwa kukata tiketi za ndege.

Kuzimwa kwa intaneti kwa mujibu wa walalamikaji, kulikiuka Ibara ya 20(1) ya Katiba inayotoa haki ya uhuru wa watu kujumuika pamoja na iliathiri uchumi, kwani watu wanategemea makundi ya Whatsapp, Twitter na Tiktok kujumuika.

Mbali na ibara hiyo, kuzimwa kwa intaneti wanadai kulikiuka Ibara ya 22(1) kuhusu haki ya kufanya kazi kwani mawakili walishindwa kufungua kesi, kushughulikia mrejesho wa kodi (tax returns) na pia kushindwa kusajili makampuni mapya.

Lakini wameenda mbali na kudai kuwa hata wanahabari walishindwa kufanya kazi zao kupitia mitandao wakati madaktari walishindwa kubadilishana taarifa za kitabibu na majaji nao waliathirika kwani walishindwa kufanya tafiti za kesi.

Waleta shauri wameambatanisha na kiapo cha pamoja, wakielezea kwa kina kile kilichotokea wakati wote wa kuzimwa kwa intaneti wakiambatanisha taarifa mbalimbali zikiwamo za kimataifa kuelezea hasara iliyotokana na uamuzi huo.

Wamenukuu pia mahojiani kati ya Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mahamoud Kombo Thabiti aliyoyafanya na kituo cha BBC akikiri na kutetea Serikali kuzima Intaneti akidai ilichangia vurugu za Oktoba 29.