Simba kunafukuta… Waarabu watia mkono

WAKATI hatima ya kiungo mshambuliaji wa Simba, Jean Charles Ahoua aliyemaliza kinara wa mabao wa klabu na Ligi Kuu Bara msimu uliopita akifunga 16, ikiwa haijaeleweka kikosini humo, taarifa mpya kutoka Morocco zinaeleza matajiri wa Kiarabu wameanza kumpigia hesabu kumvuta.

Ahoua ambaye ameshindwa kuendeleza makali aliyokuwa nayo msimu uliopita akiwa hana namba ya kudumu katika kikosi cha kwanza, jina lake limetua mezani mwa mabosi wa Raja baada ya aliyekuwa kocha wa Simba, Fadlu Davids kulipeleka jina hilo akitaka akaungane naye tena akiwa huko Morocco.

Fadlu aliyeondoka Simba Septemba 22, 2025, baada ya kudumu kwa siku 444, tangu atambulishwe kuitumikia timu hiyo rasmi, Julai 5, 2024, amerejea tena Raja Casablanca msimu huu, baada ya kuondoka msimu wa 2023-2024 alipokuwa kocha msaidizi.

Taarifa zinaeleza Fadlu amempendekeza Ahoua asajiliwe katika dirisha dogo la Januari, baada ya kiungo huyo mshambuliaji kubakisha mkataba wa miezi sita unaofikia tamati Julai 30, 2026, huku mazungumzo ya kuongeza yakiwa bado hayajafikiwa.

Ahoua aliyejiunga na Simba Julai 3, 2024, akitokea Stella Club Adjame ya kwao Ivory Coast, msimu huu umekuwa mgumu kwake kutokana na ushindani wa nafasi na nyota wenzake, wakiwamo, Joshua Mutale na Morice Abraham wanaocheza mara kwa mara.

SIMB 01

Nyota huyo msimu uliopita wa 2024-2025, ambao ulikuwa wa kwanza kwake tangu ajiunge na timu hiyo, alifanya vizuri zaidi ambapo aliibuka mfungaji bora wa Ligi Kuu Bara, baada ya kufunga mabao 16, ingawa kwa msimu huu mambo yamekuwa tofauti.

Mbali na kuibuka mfungaji bora, kiungo mshambuliaji huyo aliiwezesha Simba kufika fainali ya Kombe la Shirikisho Barani Afrika, ikiwa ni kwa mara ya kwanza baada ya miaka 32, tangu ilipofika fainali ya michuano ya CAF mwaka 1993.

Katika fainali hiyo msimu wa 2024-2025, Simba ilikosa ubingwa mbele ya RS Berkane ya Morocco, baada ya kuchapwa jumla ya mabao 3-1, ikichapwa ugenini 2-0, Mei 17, 2025, huku marudiano yaliyofanyika Zanzibar yakiisha kwa sare ya 1-1, Mei 25, 2025.

Maisha ya nyota huyo ndani ya Simba, yalianza kuharibika baada ya kuondoka kwa Fadlu, kwani hata kocha, Dimitar Pantev, aliyejiunga na timu hiyo, Oktoba 3, 2025, alikuwa hampi nafasi ya kucheza zaidi, tofauti na aliyekuwa mtangulizi wake.

Hata alivyoondoka pia, Pantev aliyesitishiwa mkataba Desemba 2, 2025, bado Ahoua aliendelea kusugua benchini chini ya kocha msaidizi, Selemani Matola, jambo linalotishia mustakabali wa kiungo huyo kama ataendelea kubakia kikosini humo.

SIMB 02

Nyota huyo aliyezichezea pia, LYS Sassandra na Sewe Sports kabla ya kukipiga Stella, alikuwa ni mchezaji bora wa Ligi ya Ivory Coast msimu wa 2023-2024, baada ya kuhusika katika mabao 21 ya kikosi hicho, akifunga 12 na kuasisti tisa.

Taarifa zaidi zinasema kuwa, tayari Raja imeanza kuwasiliana na wakala wa mchezaji huyo ili kuweka mambo sawa kabla ya kuzungumza na klabu anayoichezea ili kumbeba katika dirisha hilo la Januari, lengo la benchi la ufundi ni kutaka kuisuka timu upya ili irejee michuano ya kimataifa.

Kwa msimu huu Raja haipo katika michuano ya CAF, kwani Morocco inawakilishwa na timu nne za AS Far Rabat na RS Berkane zilizopo Ligi ya Mabingwa Afrika, huku katika Kombe la Shirikisho zipo Wydad Casablanca na Olympic Safi zote zikiwa zimepenya hatua ya makundi.