Arusha. Tanzania imeanza kuchukua hatua madhubuti za kuchangamkia uchumi wa bluu kwa mpango wa kukarabati meli zote zilizokwama nchini, pamoja na kujenga meli mbili mpya kubwa za mizigo, ikiwa ni sehemu ya mkakati wa kuongeza mchango wa sekta ya usafirishaji wa majini katika kukuza uchumi wa taifa na kufikia lengo la uchumi wa shilingi trilioni moja ifikapo mwaka 2050.
Akizungumza katika Mkutano wa 18 wa Mapitio ya Pamoja ya Sekta ya Usafirishaji (JTSR) ulioanza leo Desemba 15, 2025 jijini Arusha, Naibu Waziri wa Uchukuzi, David Kihenzile, amesema Serikali tayari imeanza mchakato wa kutafuta mkandarasi wa kukarabati meli zote zilizokuwa zimesimama katika maeneo mbalimbali nchini, hususan mikoa ya Kigoma, Katavi na Rukwa inayotegemea Ziwa Tanganyika.
Amesema hatua hiyo inalenga kufufua usafiri wa majini ili kuchochea biashara, kupunguza gharama za usafirishaji na kuongeza ufanisi wa huduma za mizigo na abiria katika maziwa makuu ya nchi.
“Mbali na ukarabati wa meli zilizopo, serikali pia imepanga kujenga meli mbili mpya kubwa za mizigo zitakazohudumia usafiri wa kikanda na kimataifa,” amesema Kihenzile.
Amefafanua meli moja itajengwa katika Ziwa Tanganyika ikiwa na uwezo wa kubeba tani 3,500 za mizigo, huku meli nyingine ikijengwa kwa ajili ya Ziwa Victoria ikiwa na uwezo wa kubeba tani 3,000. Hatua hiyo inalenga kuimarisha biashara kati ya Tanzania na nchi jirani pamoja na kuongeza mapato ya Taifa kupitia sekta ya usafirishaji wa majini.
Katika kuimarisha juhudi hizo, Kihenzile amesema Serikali pia ina mpango wa kujenga kiwanda kikubwa cha kutengeneza na kukarabati meli hapa nchini, ili kupunguza gharama za kuzitengeneza nje ya nchi na kujenga uwezo wa ndani katika teknolojia ya baharini.
“Lengo kuu ni kuifanya Tanzania kuwa kitovu cha uchumi wa bluu katika ukanda wa Afrika Mashariki na Kati, sambamba na kuhakikisha sekta hii inachangia kwa kasi kufikia malengo ya Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050,” amesema.
Ametumia fursa hiyo kuwataka wajumbe wa mkutano huo wa siku tatu kujadili kwa kina utekelezaji wa mipango hiyo ya Serikali, changamoto zake na namna ya kuharakisha utekelezaji ili matokeo yaonekane kwa wakati.
Mkutano huo wa siku tatu unafanyika kuanzia Desemba 15 hadi 17, 2025, ukiwa na kauli mbiu isemayo “Mfumo jumuishi wa usafirishaji kama msingi wa mageuzi ya kiuchumi kuelekea Dira ya Maendeleo 2050”, na unalenga kutathmini utekelezaji wa sera, mipango na miradi mbalimbali ya sekta ya usafirishaji nchini.
Kwa upande wake, Katibu Mkuu wa Wizara ya Uchukuzi, Profesa Godius Kahyarara, amesema mkutano huo hufanyika kila mwaka kama jukwaa la kuwakutanisha wataalamu wa sekta ya usafirishaji, hususan wa ujenzi wa barabara, reli na bandari, kwa lengo la kupanga kwa pamoja na kutatua changamoto za utekelezaji wa miradi.
“Masuala ya usafiri rafiki kwa mazingira na mchango wa sekta ya usafirishaji katika kukuza uchumi wa taifa pia yamepewa uzito mkubwa,” amesema Profesa Kahyarara.
Akizungumza kwa niaba ya sekta binafsi, Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Ndege la Precision Air, Patrick Mwandri, amesema wadau binafsi wanatarajia mapendekezo yao yanayotolewa katika mikutano hiyo yazingatiwe na kutekelezwa ili kuimarisha ushirikiano wa vitendo kati ya serikali na sekta binafsi katika kukuza uchumi wa Taifa.
