Dodoma. Matumizi ya teknolojia yametajwa kupunguza urasimu na rushwa katika vyombo vya utoaji haki hapa nchini.
Kauli hiyo imetolewa leo Jumatatu Desemba 15, 2025 na Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Angellah Kairuki kwenye hafla ya makabidhiano ya vifaa vya Tehama kwa Wizara ya Katiba na Sheria na taasisi zake.
Vifaa hivyo vimelenga ofisi kuu ya wizara, ofisi ya mwandishi mkuu wa sheria, ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali na Ofisi ya Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP).
Waziri Kairuki amesema kabla ya matumizi ya Tehama ndani ya vyombo vya kutoa haki kulikuwa na msongamano mkubwa wa watu waliokuwa wanatafuta haki zao.
Amesema hivi sasa mambo mengi yamepungua na hasa kwenye ushahidi wa kielektroniki ambao umekuwa ukikubalika zaidi.
“Huduma nyingi kwenye vyombo vya utoaji wa haki siku hizi zinatolewa kwa kutumia Tehama, tunashukuru taarifa tunazopata ni kuwa urasimu na rushwa vimepungua kwani mambo mengi yamekuwa ya uwazi ukizingatia ushahidi wa kielektroniki unakubalika sana,” amesema Waziri Kairuki.
Akizungumzia vifaa vilivyokabidhiwa, amewataka waliopokea kuvitumia kwa usahihi na kuonya visitumike kinyume na makusudi.
Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Angelah Kairuki akikabidhi vifaa kidijitali kwa Wizara ya Katiba na Sheria na taasisi.
Kairuki amekabidhi kompyuta mpakato 70 na mashine kubwa za kudurufu mbili lakini kabla ya hapo walishatoa kompyuta mpakato 40.
Katibu Mkuu Wizara ya Katiba na Sheria, Eliakim Maswi amesema vifaa walivyokabidhiwa vitasaidia katika uwajibikaji na kujituma ndani ya wizara na taasisi zake.
Maswi amesema kwa sasa wanahama kutoka mfumo wa makaratasi na kwenda katika mfumo wa kidijitali.
Amewataka wote watakaopokea vifaa hivyo kuongeza misingi ya kiutendaji ambayo itapelekea uwajibikaji katika utoaji haki.
Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP) Sylvester Mwakitalu amesema vifaa hivyo vitapeleka mabadiliko makubwa kwani wameona katika kompyuta mpakato 40 walizotangulia kuzipata na sasa kumekuwa na mabadiliko makubwa.
