Ushahidi butu ulivyomnusuru Bukuku kifungo miaka 20 jela

Arusha. Mahakama Kuu Masjala Ndogo ya Mbeya, imemuachia huru Raphael Bukuku, aliyekuwa amehukumiwa kifungo cha miaka 20 jela kwa makosa ya kuvunja nyumba na kuiba mali zenye thamani ya zaidi ya Sh3 milioni.

Raphael na wenzake watatu( siyo warufani katika rufaa hiyo) walidaiwa kutenda makosa hayo usiku wa Desemba 28,2023 ambapo walivunja nyumba za watu wawili na kuiba televisheni, zulia pamoja na simu zilizogharimu zaidi ya Sh3 milioni.

Wakati wa usikilizwaji wa shauri hilo, Raphael alitiwa hatiani bila kuhudhuria mahakamani na kuhukumiwa adhabu hiyo ya kifungo cha miaka 20 jela.

Katika rufaa hiyo dhidi ya Jamhuri (mjibu rufaa), Raphael alikuwa na sababu tano za rufaa ambazo ni Mahakama ilikosea kisheria kumtia hatiani bila kuzingatia mashahidi wa kwanza hadi wa tatu ambao hawakumtambua katika eneo la tukio.

Nyingine ni Mahakama ilikosea kumtia hatiani bila kuzingatia kwamba ushahidi wa mashahidi wa kwanza hadi wa nne haukuthibitishwa na jirani yoyote au kiongozi wa mtaa, Mahakama ilikosea kumtia hatiani bila kuthibitisha alikutwa na mali yoyote ya wizi badala yake ikategemea ushahidi usio na uthibitisho.

Sababu nyingine ni Mahakama ilikosea kumtia hatiani na kumuhukumu kwa kuzingatia maelezo ya onyo ambayo yalikubaliwa kinyume cha sheria kwa kuwa hakuna wakili, ndugu au jamaa ambaye alishuhudia akirekodiwa maelezo hayo ya onyo ambayo alidaiwa kuwa alikiri kosa hilo.

Sababu ya tano ni Mahakama ilikosea kisheria kwa kumnyima mrufani haki ya kusikilizwa na fursa ya kujitetea, hivyo kusababisha ukiukwaji wa haki na kuwa katika kesi ya msingi baadhi ya vifungu havikuwa sahihi.

Jaji Joachim Tiganga aliyekuwa akisikiliza rufaa hiyo iliyokatwa na Raphael alitoa hukumu hiyo Desemba 12,2025 na nakala yake kuwekwa kwenye mtandao wa Mahakama.

Baada ya kupitia mwenendo na sababu za rufaa, Mahakama Kuu ilibaini kuwa ushahidi uliotumika kumuhukumu mrufani haukuwa wa kuaminika na haukuthibitisha mashtaka bila kuacha shaka.

Amesema baada ya kusoma kwa makini rekodi nzima ya Mahakama ya chini na sababu za rufaa Mahakama hiyo ya kwanza ya rufaa ina wajibu wa kutathmini upya na kuchambua upya ushahidi.

Jaji Tiganga amesema katika kesi ya msingi, maelezo ya onyo ya washtakiwa wenzake mrufani hayakuruhusiwa kupokelewa kama vielelezo mahakamani hapo, na kuwa maelezo ya onyo ya mrufani hayakuwa na uthibitisho ambao ni msingi usiotosha wa kuhukumiwa.

“Hata hivyo baada ya kutathmini upya ushahidi kwenye rekodi nimebaini kuwa hakuna ushahidi uliomhusisha mrufani na mali za wizi, upande wa mashtaka haukuwa na ushahidi wowote wa kumuhusisha na vitu vilivyoibiwa, hakuna shahidi aliyeshuhudia kumuona akiwa na televisheni au simu zilizoibiwa.”

“Hati ya mashtaka ilieleza tu lakini upande wa mashtaka ulishindwa kutoa utambulisho wa kimsingi zaidi wa uhusiano wao na mrufani kama vile ushahidi wa jaribio la kuziuza, kushindwa huko kunachangiwa na kukosekana kwa ushahidi wowote ikiwemo wa kimazingira unaomuunganisha na tukio hilo.

Mahakama hiyo ilihitimisha kuwa ushahidi wa utambuzi wa mshtakiwa haukuwa wa kutegemewa na ulikubaliwa isivyofaa, na uchunguzi wa polisi haukuwa wa kutosha na ulitiwa doa na upande wa mashtaka ulishindwa kuthibitisha kesi dhidi yake.

“Hivyo inaamriwa kuwa rufaa inaruhusiwa, hukumu iliyotolewa kwa mrufani inafutwa na kuwekwa kando na kuamuru mrufani aachiwe mara moja isipokuwa kama ameshikiliwa kihalali,” alihitimisha Jaji