Maswa. Vifo vya wajawazito katika Halmashauri ya Wilaya ya Maswa vimepungua kwa kiasi kikubwa kwa kipindi cha miaka miwili mfululizo, kutoka vifo vinane hadi viwili, hatua inayotajwa kuwa mafanikio ya uwekezaji katika sekta ya afya.
Kupungua huko kunatajwa kuchangiwa na kuimarika kwa huduma za afya, ikiwemo upatikanaji wa huduma za upasuaji wa dharura, ujenzi wa vituo vipya vya afya na kusogezwa kwa huduma karibu na wananchi, hususan maeneo ya vijijini.
Akizungumza leo, Desemba 15, 2025, Mganga Mkuu wa Wilaya ya Maswa, Dk Hadija Zegega, amesema halmashauri imejikita katika kuboresha huduma za mama na mtoto kama mkakati wa kudhibiti vifo vinavyozuilika.
Mganga Mkuu wa halmashauri ya wilaya ya Maswa, Dk Hadija Zegega akizungumza hali ya upungufu wa vifo vya akinamama wajawazito katika halmashauri hiyo. Picha na Samwel Mwanga.
“Tumehakikisha huduma za afya zinasogezwa kwa wananchi kwa kujenga zahanati na vituo vya afya katika maeneo ya vijijini. Hili limechangia kwa kiasi kikubwa kupunguza vifo vya wajawazito kwa mwaka 2024/2025,” amesema.
Ameongeza kuwa hata vifo vya watoto wachanga vimepungua kwa kiwango kikubwa ikilinganishwa na awali.
“Hapo nyuma tulikuwa tunapata vifo kati ya 12 hadi 16 vya watoto wachanga kwa mwezi, lakini sasa vimepungua kwa sababu huduma za uzazi pingamizi zinatolewa kwa wakati, mtoto anatoka salama na mama anatoka salama,” ameongeza.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Maswa, Maisha Mtipa, amesema Serikali imeendelea kuipatia halmashauri fedha kwa ajili ya kuimarisha miundombinu ya afya.
Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya wilaya ya Maswa, Maisha Mtipa akizungumza na waandishi wa habari (hawapo pichani) leo Jumatatu Desemba 15, 2025. Picha na Samwel Mwanga.
“Serikali imetupatia Sh500 milioni kwa ajili ya ujenzi wa kituo cha afya Sangamwalugesha na Kituo cha Afya Mwasayi, ambapo kila kituo kimetengewa Sh250 milioni kama fedha za awali,” amesema.
Ameeleza kuwa kwa kila kituo cha afya zinahitajika Sh500 milioni ili kukamilika, na kuishukuru Serikali kwa kuendelea kuwekeza katika sekta ya afya.
Kukamilika kwa vituo hivyo kutaiwezesha wilaya ya Maswa kuwa na jumla ya vituo vya afya nane pamoja na hospitali ya wilaya, ambayo huduma zake zimeboreshwa baada ya kukamilika kwa majengo ya wagonjwa wa dharura, jengo la mama na mtoto, maabara pamoja na wodi za wagonjwa wa daraja la juu.
Mkazi wa Kijiji cha Mwasayi, Rehema Shija, amesema maboresho hayo yamepunguza adha kwa wajawazito.
“Zamani tulilazimika kusafiri umbali mrefu kufuata huduma za kujifungua, lakini sasa kituo kipo karibu na huduma ni nzuri, tumeona tofauti kubwa,” amesema.
Mkazi wa Kijiji cha Ipililo, Paulo Ng’wana, amesema ujenzi wa vituo vya afya umeokoa maisha.
“Kinamama wengi walikuwa wanapata shida wakipata dharura usiku, lakini sasa huduma zinapatikana kwa wakati na vifo vimepungua,” amesema.
Naye mkazi wa Maswa Mjini, Halima Mwalongo, ameishukuru Serikali na halmashauri kwa kusikiliza kilio cha wananchi.
“Tunaona matokeo halisi, kinamama wanajifungua salama na watoto wanapata huduma bora tangu kuzaliwa,” amesema.