Dar es Salaam. Kundi la waasi la M23, linalodaiwa kuungwa mkono na Rwanda, limedhibiti mji wa Uvira mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) na kutishia kuendeleza mashambulizi yake nje ya Mkoa wa Kivu Kusini.
Kauli hiyo imetolewa na Gavana wa mkoa huo, Emmanuel Rwihimba, wakati wa mkutano na waandishi wa habari, akisema kundi hilo lipo tayari kupanua operesheni zake katika maeneo mengine endapo hali itaruhusu.
Uvira, mji wa pili kwa ukubwa katika Mkoa wa Kivu Kusini na eneo la kimkakati kando ya Ziwa Tanganyika karibu na mpaka wa Burundi, ni mojawapo ya maeneo yaliyodhibitiwa kwa mafanikio makubwa zaidi na waasi hao katika siku za karibuni.
Mji huo ulikuwa makao makuu ya serikali ya DRC katika mkoa huo, baada ya mji wa Bukavu kuangukia mikononi mwa waasi mwaka uliopita.
Marekani imeilaumu Rwanda ikiitaja kuhusika katika mashambulizi hayo, ikisema hatua hiyo inakiuka makubaliano ya amani yaliyoandaliwa kwa juhudi za Rais wa nchi hiyo, Donald Trump.
Hata hivyo, Rwanda imekuwa ikikanusha madai hayo na kusisitiza haina mchango wowote wa kijeshi kwa waasi wa M23 wanaoendelea kuchochea mzozo wa kiusalama katika taifa hilo kubwa zaidi la Afrika ya Mashariki.
Mashuhuda wa hali ya usalama Uvira wanasema, licha ya hofu iliyotanda awali, hali ya utulivu inaanza kurejea taratibu, ambapo Mkazi mmoja wa eneo lililoathiriwa na vita hivyo aliwaambia waandishi wa Shirika la Utangazaji la Uingereza (BBC), kuwa watu wameanza kutoka majumbani mwao kwa tahadhari, ingawa shughuli za kawaida bado hazijarejea kikamilifu.
Maduka mengi yamesalia kufungwa na shughuli za kiuchumi zimesimama, huku wakazi wakisubiri mwelekeo wa hali ya kisiasa na kiusalama katika eneo hilo. Kwa mujibu wa Umoja wa Mataifa, zaidi ya watu 200,000 wamekimbia makazi yao kutokana na mapigano hayo.
Inaelezwa kuwa wengi wao wamekuwa wakikimbilia nchi jirani ya Burundi, hali inayozidisha wasiwasi wa usalama na huduma za kibinadamu katika ukanda huo wa Maziwa Makuu.
Wakati hali hiyo ikiendelea, jumuiya ya kimataifa imekuwa ikitoa wito wa kusitishwa kwa mapigano na kurejea kwenye mazungumzo ya amani, ili kumaliza mzozo huo na kutoa fursa kwa wananchi kuendelea na shughuli za kijamii.
