Geita. Wamiliki wa magari yanayosafirisha abiria nchini, wametakiwa kufuata ushauri wa madereva badala ya kuwaingilia kwa kuwapangia ratiba ngumu za safari hali inayochangia ongezeko la ajali.
Baadhi ya wamiliki wa magari hayo wamekuwa wakiwapangia madereva muda na idadi ya safari na fedha pasipo kufanya matengenezo ya vyombo vyao, hivyo kuhatarisha usalama wa abiri ambapo amewataka madereva kuendelea kuwashauri wamiliki wa vyombo hivyo.
Kauli hiyo imetolewa leo Jumatatu Desemba 15,2025 na Butasyo Mwambene, Ofisa mnadhimu kikosi cha usalama barabarani nchini wakati akizungumza na madereva na mawakala wa mabasi katika kituo kikuu cha mabasi manispaa ya Geita.
Butasyo Mwambene,Ofisa Mnadhimu kikosi cha Usalama Barabarani nchini akizungumza na Madereva stendi kuu ya Mabasi Geita.
“Wamiliki wa magari unapompangia muda yeye atapaa? Tuwasikilize madereva mnatoa maelekezo lakini magari hamtengenezi na hasa yanayotoka mjini kwenda vijijini, wamiliki msikilize dereva tusiangalie fedha tu,” amesema Mwambene.
Katika hatua nyingine, Mwambene ameonya baadhi ya madereva kupiga muziki usio na maadili.
“Kumbuka kwenye gari unakuta wanasafiri baba, mke na watoto, sasa mnaonyesha picha za utupu yale ni maadili ya Tanzania? Mnaenda msibani una wakwe mle ndani lakini vitu vinavyoonyeshwa ni aibu, wekeni vitu vya maadili mnatudhalilisha nchi,” amesema.
Butasyo Mwambene,Ofisa Mnadhimu kikosi cha Usalama Barabarani nchini akizungumza na Madereva stendi kuu ya Mabasi Geita.
Aidha Masembo amewataka mawakala kuacha kupandisha nauli msimu wa mwisho wa mwaka ambao umekuwa na abiria wengi, ambapo amewataka kuongozwa na hofu ya Mungu na kuridhika na kile wanachokipata.
Naye Rajabu Selemani, Ofisa Mfawidhi kutoka Mamlaka ya Udhibiti Usafiri Ardhini (Latra) Mkoa wa Geita amesema wamekuwa wakishirikiana na Jeshi la Polisi katika ukaguzi wa vyombo vya moto kudhibiti vilivyochakaa pamoja na madereva walevi, ili kupunguza ajali nchini.
