Dar es Salaam. Vilio na huzuni vimetanda kila kona kwa wakazi wa Jimbo la Peramiho huku idadi kubwa ya watu ikijitokeza kutoa heshima ya mwisho kwa aliyekuwa Mbunge wa jimbo hilo, kupitia Chama cha Mapinduzi (CCM) Jenista Mhagama.
Jenista ambaye amekuwa mbunge wa Peramiho kuanzia mwaka 2005, amefariki dunia jana Alhamisi, Desemba 11, 2025 jijini Dodoma, ambapo mwili wake unatarajiwa kuzikwa kesho Jumanne ya Desemba 16, 2025 katika Kijiji cha Ruanda, Mbinga mkoani Ruvuma.
Wananchi hao ambao wengi walitarajiwa kuwa mashambani na wengine kwenye shughuli mbalimbali kama biashara au maofisini, leo Desemba 15, 2025 wamefunga biashara zao na kujitokeza katika misa ya kumuombea marehemu Jenista iliyofanyika katika Kanisa la Mtakatifu Benedict, Parokia ya Peramiho Jimbo kuu la Songea.
Daines Komba mkazi wa Peramiho A amesema, wananchi wamejitokeza kwa wingi kutokana na kumpenda mbunge wao ndio maana wamefunga biashara zao na kuahirisha shughuli zao za kila siku kwa ajili ya kutoa heshima ya mwisho.
“Umati huu mkubwa ni heshima kwa malkia wa Peramiho, ametupatia heshima na maendeleo makubwa mno tunamuombea apumzike kwa amani,” amesema Daines.
Bosco Ngonyani mkazi wa Parangu amesema hakuna mtu ambaye alijua kifo cha Jenista kingekuwa cha ghafla hivyo, ndio maana wameumia na kuja kutoa heshima zao.
“Kifo hiki kimetuumiza wengi, kwani wananchi walitarajia kuwa awamu hii wangepata maendeleo makubwa zaidi kutokana na mchango mkubwa aliokuwa nao kwa watu wake na alipenda jimbo hili,” amesema Ngonyani.
Akitoa mahubiri Naibu Askofu Jimbo Kuu katoliki la Songea aliyeongoza misa hiyo, Erick Mapunda amesema wengi hawapo tayari kukipokea kifo, au kupokea vifo vya wapendwa wao, akisema hali hiyo inachangia wengi wao kuzusha taharuki na kutokubali kuwa ni vifo vya kawaida.
“Kwa nini hatupo tayari, mimi nadhani wengi wetu tumejisahau tumeukumbatia sana ulimwengu tukidhani maisha yetu ni hapahapa duniani, tunaendelea kula anasa na mengineyo.”
Amesema wengi wanabaki kuishi maisha ya kila siku waliyoyazoea, akitaja sababu nyingine ya kutokukipokea kifo ni wengi kutojiandaa kiroho.
“Tunaogopa tukifa huko mbele itakuwaje, hatujajitayarisha kwa uhakika Mheshimiwa Jenista hakuogopa kifo, hakuukumbatia ulimwengu ndiyo maana maisha yake daima alikuwa mcha Mungu ndiyo maana alikuwa anasali sana hakukubali siku ipite bila kuomba.
“Kifo ukipenda, usipopenda utalazimika tu kukipokea.”
Mapunda ametaja jambo la pili ni kupokea vifo vya wenzetu, akisema siku ya kifo ikifika lazima upokee lakini kupokea vifo vya wenzetu mara nyingi huleta shida.
Ametaja mifano kuwa vifo vya wenzetu akifa mmoja maneno yanakua mengi sana, vurugu zinakuwa nyingi, magomvi na kutokuelewana miongoni mwa familia, jamii.
“Vifo vinaonekana vinaleta vurugu na utengano na mafarakano, utasikia hajafa bure ni mkono wa mtu kunakuwa na maneno mengi na vurugu nyingi, hiyo ni ishara kwamba hatuko tayari kupokea vifo vya wenzetu, tupokee vifo vya wenzetu kwa imani na kwa ujasiri tukimpigia Mungu magoti na kumshukuru kwa maisha ya wapendwa wetu hapa duniani,” amesema.
Akihitimisha mahubiri yake, Mapunda amewataka Watanzania kuwa na utaratibu wa kumtanguliza Mungu katika mipango yao, ili waendelee kuishi wakimtumaini Mungu.
“Inabidi tuseme Mungu akipenda kesho nitaenda kufanya hili na lile. Inatupasa tumshukuru Mungu kwa zawadi hii ya maisha ya Jenista, Mungu ametufanyia mengi sana katika familia zetu, jamii, kanisa na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia mtumishi wake huyu Jenista Mhagama, amewatumikia wananchi kwa miaka mingi,” amesema.
Akisoma wasifu wa marehemu, Katibu wa Bunge, Baraka Leonard, amesema Jenista Mhagama alizaliwa Juni 23, 1967, katika Kijiji cha Parangu, Peramiho, mkoani Ruvuma.
Alipata elimu ya msingi Parangu na kuendelea na elimu ya sekondari kuanzia mwaka 1982 hadi 1985, kabla ya kujiunga na Chuo cha Ualimu Korogwe, ambako alihitimu masomo ya ualimu.
Mwaka 1999, alipata Shahada ya Kwanza ya Uongozi na Utawala kutoka Chuo Kikuu cha Cambridge, na hadi anafariki dunia alikuwa akiendelea na masomo ya Shahada ya Uzamili (Masters) kwa njia ya masafa nchini Uingereza.
Mwili wa Jenista umepelekwa kwa wapiga kura wake Peramiho ambapo shughuli inafanyika Kanisa Katoliki la Peramiho, viongozi mbalimbali akiwemo Zungu, Dk Mwigulu wamehudhuria. Baada ya misa hiyo mwili wake utapelekwa nyumbani kwake eneo la Parangu.
