Dar es Salaam. Rais wa Ukraine, Volodymyr Zelensky amesema nchi yake ipo tayari kuachana na azma ya kujiunga na Jumuiya ya Kujihami ya Mataifa ya Magharibi (Nato), iwapo itapatiwa dhamana madhubuti za usalama.
Kauli hiyo ilitolewa kabla ya mkutano uliodumu kwa saa tano kati ya Zelensky na mjumbe maalumu wa Rais wa Marekani, Donald Trump, Steve Whitaker, uliofanyika mjini Berlin, ambapo Whitaker alisema mazungumzo hayo yamepiga hatua kubwa katika kutafuta suluhu ya kudumu ya vita nchini Ukraine.
Zelensky aliwaambia waandishi wa habari Ukraine ipo tayari kufanya uamuzi mgumu kwa ajili ya amani, lakini akasisitiza kuwa usalama wa nchi yake ni kipaumbele kikuu.
Hatua hiyo imekuja wakati juhudi za kimataifa za kumaliza vita vinavyoendelea kati ya Russia na Ukraine ambapo Zelensky aliongeza kuwa Kyiv inatarajia kuishawishi Marekani kubaki mstari wa mbele katika juhudi za kumaliza vita hivyo, badala ya kupunguza ushiriki wake.
Katika hatua nyingine, wiki iliyopita, Ukraine na Marekani zilifanya mazungumzo ya siku tatu huko Florida, ambako pande zote zilijadili mapendekezo ya Kyiv ambayo yanaweza kujumuishwa katika mpango wa amani wa Marekani.
Hata hivyo, hadi sasa bado haijafahamika ni mapendekezo gani hasa yamekubaliwa kuingizwa katika mpango huo, ambapo Mshauri wa Zelensky alisema maoni rasmi ya rais kuhusu mpango wa amani yatatolewa baada ya kukutana na viongozi wa Ulaya na wa Nato, katika mkutano uliopangwa kufanyika leo Jumatatu, Desemba 15, 2025.
Kwa mujibu wa taarifa zilizopo, Marekani imependekeza Ukraine iondoe wanajeshi wake kutoka mashariki mwa nchi hiyo, eneo ambalo Russia inadaiwa kulidhibiti kwa takribani asilimia 75.
Marekani imeeleza Russia itajiondoa katika maeneo mengine na kusitisha mapigano kutatekelezwa kama sehemu ya makubaliano ya amani. Hata hivyo, Ukraine imeonyesha kusitasita kukubali pendekezo hilo, ikisisitiza kuwa haipo tayari kutoa ardhi yake kwa Russia.
Mazungumzo kati ya Zelensky, viongozi wa Ulaya na wa Nato yanatarajiwa kuwa na uzito mkubwa katika kuamua mustakabali wa mpango wa amani na mwelekeo wa vita vinavyoendelea.
