150 zachuana kutafuta kina Novatus wengine

JIJI la Arusha limeendelea kung’ara kwenye ramani ya soka la vijana barani Afrika baada ya jumla ya timu 150 kushiriki mashindano ya African Chipkizi Cup 2025 yanayofanyika kwa msimu wa 16 mfululizo.

Mashindano hayo yanahusisha timu za vijana wa kike na kiume chini ya umri wa miaka 7, 9, 11, 13, 15, 17 na 20 kutoka nchi za Tanzania, Kenya, Uganda, Zimbambwe na Zambia, yakilenga kukuza vipaji na kuwa daraja la maendeleo ya soka la baadaye.

African Chipkizi Cup yameendelea kuthibitisha umuhimu wake kuibua wachezaji waliofika ngazi ya juu, akiwemo nyota wa Taifa Stars, Novatus Miroshi anayekipiga katika klabu ya Goztepe ya Uturuki na anayetarajiwa kuiwakilisha Tanzania kwenye AFCON 2025 nchini Morocco, akiwa amewahi kupita kwenye mashindano hayo.

Ushiriki wa benchi la ufundi na makocha wa ngazi za juu, umeongeza uzito wa mashindano hayo yanayoandaliwa na kituo cha Future Stars Academy, huku yakitazamwa kama jukwaa muhimu la kugundua vipaji vitakavyoimarisha timu za taifa za vijana na hatimaye kikosi cha wakubwa.

Kocha katika benchi la ufundi la timu za taifa za vijana Tanzania chini ya umri wa miaka 15 na 17, Haruna Adolf, wakati wa ufunguzi amesema mashindano hayo yanawapa fursa kubwa ya kuona vipaji vipya.

“Tunashukuru kila mwaka yanaendelea kuwepo na yanatuongezea kitu kikubwa katika mchakato wa kutafuta vijana wa kuijenga timu ya taifa ya baadaye,” amesema.

Kocha wa Fountain Gate FC inayohiriki Ligi Kuu Bara, Mohammed Laizer, amesema Chipkizi Cup imekuwa shule muhimu ya soka la kisasa kwa vijana na makocha.

“Modern Football ni eneo kubwa sana, mashindano haya si ya Tanzania pekee, kuna timu nyingi kutoka nje, kama kocha najifunza pia kwa kuona na kushuhudia wenzangu wanavyojenga timu zao,” amesema Laizer.

Meneja wa mashindano hayo, Abel Mtweve, amesema lengo kuu ni kuibua vipaji vya vijana kuanzia umri chini ya miaka saba hadi 20, akibainisha kuwa mafanikio yaliyopatikana yamesababisha mabadiliko ya jina kutoka East African Chipkizi Cup hadi African Chipkizi Cup ili kupanua wigo wa ushiriki.

Amesema anaamini msimu ujao timu kutoka maeneo mengine ya Bara la Afrika zitajiunga, pia mawakala wengi zaidi watakuja kuangalia vipaji.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Chama cha Soka Mkoa wa Arusha (ARFA), Zakayo Mjema, amesema wataendelea kushirikiana na waandaaji kuhakikisha vijana wanapata fursa zaidi za kutimiza ndoto zao kupitia soka na kuandaa hazina ya vipaji kwa ajili ya timu ya taifa.

Mashindano hayo yaliyaoanza jana Jumatatu, Desemba 15, 2025, yanafanyika katika viwanja vya TGT jijini Arusha na yanatarajiwa kufukia tamati Desemba 21, 2025.