Dar es Salaam. Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu imemuhukumu Irene Mabeche (58) kifungo cha nje cha mwaka mmoja na kutokujihusisha na makosa yoyote ya jinai, baada ya kukiri shtaka la kuhamasisha umma kufanya maandamano na kuzuia kufanyika kwa Uchaguzi Mkuu uliofanyika Oktoba 29, 2025.
Mabeche ambaye ni mjasiriamali na mkazi wa Wazo Tegeta mkoani Dar es Salaam, alikuwa anakabiliwa na kesi ya jinai namba 28914 ya mwaka 2025 yenye shtaka moja la kuhamasisha umma kufanya vitendo vya uhalifu na maandamano.
Anadaiwa kutenda kosa hilo kinyume na kifungu 340 na 35 cha Sheria ya Kanuni ya Adhabu, Sura 16 iliyofanyiwa marejeo mwaka 2023.
Leo, kesi hiyo iliitwa kwa ajili ya mshtakiwa kusomewa hoja za awali (PH) baada ya upelelezi wa shauri lake kukamilika.
Hata hivyo, kabla ya kusomewa maelezo hayo, mshtakiwa alikumbushwa shtaka lake na wakili wa Serikali Eric Davies, mbele ya Hakimu Mkazi Kisutu, Hassan Makube.
Irene baada ya kukubwa shtaka lake alikiri kutenda kosa hilo na ndipo upande wa Jamhuri walipomsomea hoja za awali.
Akisoma hoja hizo, Wakili Davies alidai Oktoba 29, 2025 saa 5:50 asubuhi, mshtakiwa akiwa katika gari aina ya Toyota Prado aliwakusanya madereva bodaboda na bajaji waliokuwa eneo hilo na kuwahamasisha kufanya maandamano na kufunga barabara ya Bagamoyo.
” Mshtakiwa aliwaeleza madereva hao wa bajaji na bodaboda kuwa maandamano yameshaanza Ubungo, hivyo ikishafika saa 9:00 alasiri nao waandamane na kufunga barabara ya Bagamoyo na wazuie kufanyika kwa uchaguzi mkuu ambao ulifanyika Oktoba 29, 2025,” alidai wakili Davies.
Mshtakiwa baada ya kuhamasisha vijana hao kufanya maandamano, alitoka eneo hilo kwenda eneo la Kisanga na Loliondo lililopo Wazo, Wilaya ya Kinondoni.
“Mshtakiwa baada ya kugundua kuwa alikuwa anafuatiliwa kwa nyuma, alirudi nyumbani kwake eneo la Wazo,” alidai Eric wakati anamsoma hoja za awali ya awali.
Baada ya kurejea nyumbani, mshtakiwa alikamatwa siku hiyo na walipomkagua walikuta akiwa na simu aina ya Sumsung A14.
“Simu ya mshtakiwa ilichukuliwa na kwenda kuchunguzwa Kitengo cha Uchunguzi wa Sayansi Jinai (Forensic Bureau), ambapo ilikutwa na ujumbe mfupi (sms) uliochapishwa kuwa anakusudia kuzuia uchaguzi mkuu wa mwaka 2025,” alidai.
Mshtakiwa baada kusomewa shtaka hilo alikiri shtaka na kuomba apunguziwa adhabu.
“Naiomba mahakama yako inipunguzie adhabu kulingana na umri wangu, nina presha, kisukari na nina wazazi wanaonitegemea, hivyo naomba kupunguziwa adhabu” alidai mshtakiwa baada ya Mahakama kumpa nafasi ya kujitetea.
Hata hivyo, hakimu Makube alimuuliza maswali kadhaa mshtakiwa huyo, kuhusiana na kesi yake na sehemu ya mahojiano ilikuwa kama ifuatavyo
Hakimu: Una miaka mingapi?
Hakimu: Bado kidogo ungestaafu kama ungekuwa mtumishi serikalini.
Hakimu: Ungekuwa kijana ningesema labda umri unasumbua, sasa wewe mtu mzima unatoka na kuhamasisha maandamano hivi huoni aibu?
Mshtakiwa: Mheshimiwa naomba unisamehe na unipunguzie adhabu.
Hakimu: Hivi hata mwenzako anakuonaje ? Na jamii inakuonaje?
Mshtakiwa: Ndio maana nakuomba mheshimiwa unipe adhabu ndogo.
Hakimu: Watoto wako wanavyokuja gerezani kukuangalia unajisikiaje?.
Hakimu: Wewe ukifanya hivyo, watoto wako wafanye nini eeh?
Mshtakiwa: Najutia kosa langu mheshimiwa hakimu naomba unisamehe.
Hakimu: Watoto wako unawaonyesha tabia gani?
Mshtakiwa: Nisamehe mheshimiwa.
Hakimu: Wewe kwa umri wako, ulitakiwa utulie nyumbani kwako.
Baada ya mahojiano hayo, wakili Davies aliomba mahakama itoe adhabu kwa mujibu wa sheria kwa sababu mshtakiwa amekiri shtaka lake mwenyewe bila kulazimishwa.
Akitoa uamuzi huo, hakimu Makube, alisema kwa kuangalia mazingira yenyewe, mahakama inadhani kuwa mshtakiwa anajutia kosa hilo na ni aibu.
” Mahakama imezingatia muda uliokaa magereza ni adhabu tosha kwako mshtakiwa,” alisema hakimu Makube na kuongeza;
“Baada ya kupitia maelezo ya upande wa Jamhuri na mshtakiwa, mahakama hii inakuachia huru kwa masharti ya kutofanya kosa lolote la jinai ndani ya kipindi cha mwaka moja, unatakiwa uwe balozi na raia mwema,” alisema hakimu Makube.
Mshtakiwa baada ya kuelezwa hayo, akiwa ndani ya chumba cha mahakama alinyanyua mikono juu ishara ya kumshukuru Mungu huku akibubujikwa na machozi ya furaha.
Kwa mara ya kwanza, mshtakiwa huyo alifikishwa mahakamani hapo Novemba 7, 2025 na kusomewa kesi ya uhaini akiwa na wenzake 94.
Desemba 10, 2025 mshtakiwa huyo alipandishwa kizimbani kwa mara ya pili na kusomewa kesi ya jinai yenye shtaka moja la kuhamasisha umma kufanya maandamano na kuzuia uchaguzi mkuu usifanyike.
