Baraza Kuu UN lapitisha azimio kukabili changamoto ya afya ya akili, NCDs

Dar es Salaam. Mkutano wa 80 wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa (UNGA) umepitisha azimio linalolenga kuimarisha mapambano dhidi ya magonjwa yasiyoambukiza (NCDs) pamoja na changamoto za afya ya akili kwa kutumia mkakati jumuishi na shirikishi.

Azimio hilo linakusudia kuleta mabadiliko chanya katika afya na ustawi wa watu duniani ifikapo mwaka 2030.

Azimio hilo ni matokeo ya majadiliano ya kina yaliyofanywa na serikali mbalimbali kabla na wakati wa Mkutano wa  nne wa ngazi ya juu wa Umoja wa Mataifa kuhusu kuzuia na kudhibiti magonjwa yasiyoambukiza na kuboresha afya ya akili, uliofanyika Septemba 25, 2025.

Likibeba kichwa cha habari “usawa na ujumuishi, kubadilisha maisha na kipato kupitia uongozi na hatua dhidi ya magonjwa yasiyoambukiza na kukuza afya ya akili na ustawi, azimio hilo linatajwa kuwa fursa muhimu ya kuharakisha maendeleo ya kimataifa kwa kuweka malengo mahsusi yatakayopimika.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Shirika la Afya Duniani (WHO) leo Jumanne Desemba 16, 2025, kupitishwa kwa azimio hilo kunatarajiwa kufungua ukurasa mpya katika juhudi za kukabiliana na changamoto kubwa za afya duniani.

WHO imeeleza kuwa, kwa sasa magonjwa yasiyoambukiza ni miongoni mwa visababishi vikuu vya vifo duniani, yakisababisha vifo vya mapema vya takribani watu milioni 18 kila mwaka, huku changamoto za afya ya akili zikiwaathiri zaidi ya watu bilioni moja.

Taarifa hiyo imefafanua kuwa magonjwa yasiyoambukiza kwa kiasi kikubwa husababishwa na vihatarishi vinavyozuilika, ikiwemo lishe duni, matumizi ya tumbaku, unywaji wa pombe kupita kiasi, ukosefu wa mazoezi ya mwili na uchafuzi wa hewa, mambo ambayo pia huathiri afya ya akili.

Akizungumza kuhusu hatua hiyo, Mkurugenzi Mkuu wa WHO, Dk Tedros Ghebreyesus amesema kupitishwa kwa malengo madhubuti ni ushahidi wa dhamira ya dhati ya nchi wanachama kulinda afya za wananchi wao.

Azimio hilo limeweka kwa mara ya kwanza malengo matatu ya kimataifa yatakayoharakishwa ifikapo 2030, yakiwemo kupungua kwa watumiaji milioni 150 wa tumbaku, kuongezeka kwa watu milioni 150 wenye shinikizo la damu wanaodhibiti hali zao, pamoja na watu milioni 150 kupata huduma za afya ya akili.

Ili kufanikisha malengo hayo, nchi wanachama zimetakiwa kuimarisha sera, mifumo ya huduma za afya ya msingi, ulinzi wa kifedha, mipango shirikishi ya kitaifa na mifumo madhubuti ya ufuatiliaji na ukusanyaji wa takwimu kuhusu NCDs na afya ya akili.