MIGUEL Gamondi yupo Misri kwa sasa akikinoa kikosi cha timu ya taifa, Taifa Stars kinachojiandaa na fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON) 2025 zitakazofanyika Morocco kuanzia Desemba 21, lakini huku nyuma jamaa ametoa maagizo kwa mabosi wa Singida Black Stars anayoinoa kuchomoa mtu pale Yanga.
Taarifa kutoka Singida zinasema kuwa, mabosi wa klabu hiyo inayoshiriki michuano ya Kombe la Shirikisho Afrika kwa mara ya kwanza ikiwa hatua ya makundi na kuvuna pointi moja hadi sasa baada ya kucheza mechi mbili za Kundi C, wameanza mchakato wa kutaka warudishiwe beki wa kati aliyepo Yanga, Frank Assinki.
Beki huyo Mghana alipelekwa Yanga kwa mkopo katika usajili wa dirisha kubwa msimu huu, kutokana na kukosa namba mbele ya mabeki Anthony Tra Bi Tra, Mukrim Issa na Kennedy Juma na wakati mwingine Gamondi humtumia kiungo mkabaji Morice Chukwu kucheza nafasi hiyo kikosini.
Hata hivyo, kutokana na kutingwa na mechi ngumu katika Ligi Kuu na Kombe la Shirikisho Afrika mbali na Kombe la Shirikisho (FA) na Kombe la Mapinduzi itakayoenda kucheza hivi karibuni, Gamondi ameagiza beki huyo wa kati arudishwe haraka kikosini kabla hajarejea kutoka Morocco.
Taarifa hizo zinasema kuwa, sababu ya Gamondi kumtaka Assinki ni kuimarisha eneo hilo la beki ya kati, kwani huenda Tra Bi anayemaliza mkataba wake wa miaka miwili akaondoka katika dirisha dogo litakalofunguliwa Januari Mosi 2026.
Tra Bi alijiunga na Singida msimu uliopita akitokea ASEC Mimosas ya Ivory Coast na ni kama hajaeleweka vyema mbele ya kocha Gamondi ambaye amekuwa akiwapishanisha na mabeki wengine wa kati wa kikosi hicho sambamba na kiungo Chukwu anayependa kumtumia kama beki wa kati.
Chanzo cha kuaminika kutoka ndani ya Singida kimeliambia Mwanaspoti, uongozi wa klabu hiyo umeamua kutekeleza agizo la Gamondi kwa kutuma barua ya maombi ya kuvunja mkataba wa mkopo uliobaki miezi sita uliobaki wa beki Assinki ili aweze kurejea katika timu hiyo kipindi cha dirisha dogo msimu huu.
“Gamondi hajaridhishwa na uwezo wa Tra Bi na ndio maana unaona kuna wakati huwa anamtumia zaidi Morice Chukwu ambaye amekuwa panga pangua kikosi cha kwanza huku akitaka Assinki aliyepo Yanga kwa mkopo arudishwe haraka,” chanzo hicho kilisema na kuongeza;
“Tayari tumeiandikia Yanga barua kumuomba Assinki arudi kikosini dirisha hili kama mambo yataenda kama yalivyopangwa basi Tra Bi anaweza akatolewa kwa mkopo ili amalize mkataba wa miezi sita uliobaki kwa sasa kikosini kabla ya kufikia tamati.”
Chanzo hicho kilisema kwa mwenendo wa timu hiyo iliyopoteza mechi ya mwisho ya Ligi Kuu nyumbani mbele ya TRA United kwa mabao 3-1, imepanga pia kusajili kipa mmoja wa maana ili kupunguza makosa waliyonayo hasa eneo hilo la ulinzi. Hata hivyo, Singida kwa sasa ina makipa watatu akiwamo Amas Obasogie, Hussein Masalanga na Metacha Mnata, huku jina la Khomein Abubakar aliyekuwa akiidakia enzi ya Ihefu kabla ya kwenda Yanga, akitajwa huenda akarejea hapo.
Wakati Singida ikiwaza kumrudisha Assinki ambaye hana namba ya kudumu kikosi cha kwanza cha Yanga kutokana na uwepo wa pacha ya Dickson Job na Ibrahim Hamad ‘Bacca’ inaelezwa dakika 180 alizocheza amenogewa Jangwani na hatamani kuondoka tena kwa wababe hao wa Ligi Kuu Bara.
Rafiki wa karibu wa mchezaji huyo, ameliambia Mwanaspoti, Assinki amesikia tetesi za kutaka kurejeshwa Singida, lakini mwenyewe hayupo tayari kurudi kwani anafurahia maisha ndani ya Yanga.
“Assinki ameomba nafasi ya kuaminiwa zaidi ili kuonyesha uwezo alionao katika nafasi hiyo, licha ya kutambua ugumu wa namba kutokana na uwepo wa wachezaji ambao yatari wametengeneza bondi ya muda mrefu na amesema hayupo tayari kuondoka kwani anafurahia maisha ndani ya timu hiyo.”
Beki huyo amecheza mechi mbili za ligi kutokana na Bacca kutumikia adhabu ya kufungiwa mechi tano na katika mechi hizo mbili Yanga haijaruhusu bao dhidi ya Fountain Gate waliyoifunga 2-0 na ushindi wa 1-0 mbele ya Coastal Union.