DPP amfutia kesi ya uhaini Irene na kumwachia huru

Dar es salaam. Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, imemfutia kesi na kumuachia huru, mshtakiwa Irene Mabeche (58) aliyekuwa anakabiliwa na kesi ya Uhaini, baada ya Mkurugenzi wa Mashtaka nchini (DPP) kutokuwa na nia ya kuendelea na mashtaka dhidi yake.‎

‎Uamuzi huo umetolewa na Hakimu Mkazi Mkuu wa mahakama hiyo, Hassan Makube, baada ya wakili wa Serikali, Eric Davies kuieleza mahakama DPP amewasilisha hati ya kutokuwa na nia ya kuendelea na kesi dhidi ya mshtakiwa.‎

‎Wakili Davies alidai kuwa DPP amemfutia kesi hiyo ya uchunguzi namba 26387 ya mwaka 2025 chini ya kifungu namba 92(1) Cha Sheria ya Makosa ya Jinai, Sura ya 20 ilivyofanya marejeo mwaka 2023.‎

‎”Kesi imeitwa kwa ajili ya kutajwa na Mkurugenzi wa Mashtaka nchini hana nia ya kuendelea na kesi hii, hivyo tunaomba kupitia kifungu hiki mahakama imuondolee mashtaka dhidi yake” amedai Wakili Davies.‎

‎Hakimu Makube amekubaliana na ombi hilo na kumwachia huru mshtakiwa huyo, chini ya kifungu hicho.‎

‎”Mahakama inakubaliana na ombi la upande wa Jamhuri kama lilivyowasilishwa, hivyo  inakuachia huru mshtakiwa,” amesema Hakimu  Makube. ‎

‎Kwa mara ya kwanza Irene alifikishwa mahakamani hapo Novemba 7, 2025 na kusomewa kesi ya uhaini yenye mashtaka mawili ya kula njama na kutenda kosa.

‎‎Katika kesi ya msingi, mshtakiwa anadaiwa kwa nyakati tofauti kati ya Aprili Mosi na Oktoba 29, 2025 alikula njama za kutenda kosa la uhaini.‎

‎Katika shtaka la pili, Irene anadaiwa Oktoba 29, 2025 katika maeneo mbalimbali ya Jiji la Dar es Salaam, wakiwa chini ya utii wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania alinuia kuzuia Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2025, usifanyike.‎

‎Inadaiwa kuwa mshtakiwa huyo alitangaza nia hiyo kwa lengo la kuitisha Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na kuithibitisha nia hiyo kwa kusababisha hasara kubwa kwa mali za Serikali zilizokusudiwa kutoa huduma muhimu.‎

‎Hadi anafutiwa kesi hiyo, mshtakiwa huyo amekaa mahabusu kwa siku 39 kutoka na kesi hiyo kutokuwa na dhamana kwa mujibu wa sheria.