Hersi afafanua ukweli ulivyo madai ya kuishambulia Simba

BAADHI ya mashabiki wa Simba wanalia juu ya uwasilishaji uliofanywa na Rais wa Yanga na Mwenyekiti wa Chama cha Klabu za Soka Afrika (ACA), Injinia Hersi Said kwenye kongamano la soka lililoandaliwa na Shirikisho la Mpira wa Miguu la  Kimataifa (FIFA) wakidai bosi huyo aliwamaliza, lakini mwenyewe ametoa ufafanuzi.

Akizungumza na Mwanaspoti akiwa Qatar kulikofanyika kongamano hilo la siku mbili, Hersi amesema mjadala huo unapotoshwa na hawezi kuishambulia Simba kama inavyoelezwa na watu ambao hawakufuatilia alichosema.

Hersi amesema kwenye mchango wake alionyesha namna klabu nyingi Afrika zinavyokabiliana na udhaifu mbalimbali, matatizo ya kiutawala, miundombinu na udhamini unaojitosheleza.

“Kwanza nikupongeze nyie Mwananchi, ni mwandishi wa tatu ambao mmeonyesha uthubutu wa kutafuta uhalisia wa kipi ambacho kimezungumzwa, nimeona mjadala hapo nyumbani ni kama unapotoshwa hivi kwa namna kilichojadiliwa,” amesema Hersi.

“Sio kweli mchango wangu ulikuwa unaishambulia Simba, ilikuwa inazungumzia maendeleo ya klabu na mabadiliko yake ya kiungozi, eneo la kwanza nilizungumzia changamoto za eneo hilo, huwezi kukimbia uongozi bora unaopaswa kuziendesha klabu zetu, nikatoa mifano ya klabu zetu nikianza na Yanga tulipotoka tena tukaonyesha video za vikao vya wanachama wetu kabla ya mabadiliko ya kiuongozi, baada ya hapo tukaonyesha mambo yanayoendelea kwa wenzetu wa Simba.

“Nataka kukuambia huko nyumbani mnajadili mambo mepesi lakini wenzetu huku wameelimika sana na namna klabu zetu za Afrika zinahitaji kubadilika kiutawala, hatuwezi kufikia hatua kubwa kama tutaendelea kukabiliana na changamoto za kiutawala.”

Aidha, Hersi alifafanua kuwa eneo la miundombinu nalo ni sehemu ambayo klabu zinatakiwa kubadilikapia mfano wake ulionyesha namna Yanga ilivyokuwa na jengo dhaifu mpaka kulibadilisha na kuwa la kisasa.

“Kuna eneo la miundombinu, tukubalieni tuna deni kubwa la kutakiwa kubadilika hapa, pale nikaonyesha picha ya jengo letu la klabu kabla ya kufanyiwa marekebisho makubwa, kupitia mabadiliko ya mfumo wa uendeshaji (transformation), nikaonyesha picha za klabu yetu na jengo letu kabla, husikii watu wa Yanga wakilalamika.

“Utazungumzia kuhusu maendeleo ya kisoka, na soka la vijana, mifumo sahihi ya kuendeleza wachezaji na hasa wadogo wa kiume na wale wa kike hizi ndizo changamotio za klabu zetu hapa Afrika.

“Baada ya kuona hayo, eneo la pili tukaangalia ni njia gani sahihi, nikaeleza njia sahihi ni kubadilisha mfumo wa uendeshaji wa klabu zetu, tulete uongozi ambao una mfumo mzuri, tulete wataalam waingie kwenye mpira, tutafute wadhamini kwani klabu zetu bado zinahitaji sana wadhamini ili ziweze kumudu kujiendesha, haya yanaweza yote yataweza kuchangia maendeleo ya mpira wa Afrika.

“Eneo la tatu tukaonyesha faida ya mabadiliko ya kiuongozi ambayo klabu yetu imeanza kuyapitia. Mfano sisi Yanga kupitia mabadiliko haya tulikuwa tunaingiza kiasi cha Sh10 milioni kwa mwaka lakini sasa unazungumzia klabu kuingiza kiasi cha Sh1.3 bilioni, tulikuwa na wanachama hai wasiozidi 1,000 lakini sasa tumefikisha wanachama hai zaidi ya 90,000, tunaingiza fedha nyingi na bado tunaweza kufanya zaidi, nadhani nyie wanahabari mliona kwenye mkutano wetu mkuu uliopita.”

Hersi aliongeza kuwa hana shida na uongozi wa Simba wala klabu hiyo, lakini mchango wake ulilenga kuzisaidia klabu zote hatua ambayo ilipokewa na mlengo chanya na mkutano huo.

“Nawaheshimu sana Simba, kuanzia mwenyekiti wake Murtaza Mangungu, mwenyekiti wa bodi Magori (Crescentius) nadhani hata wao mkiongea nao watakiri hizo ni changamoto kubwa za klabu zetu, sisi tumekabiliana nazo na tunaendelea na hata wao wanakabiliana nazo,” amesema.

Wakala wa wachezaji kutoka Morocco, Anas El Amran aliliambia Mwanaspoti mchango wa Hersi ulionyesha uhalisia wa klabu za Afrika, akisema kama kila klabu itafanyia kazi mapendekezo yake, soka la Afrika litapiga hatua.

“Nilifuatilia ule mjadala, bahati kubwa kwa Tanzania ni kuwa na kiongozi mwenye maono ya namna ya Said, mchango wake ulibeba taswira halisi ya soka la Affrika hasa kwa klabu zetu, mimi nafanya kazi na klabu mbalimbali Afrika, nyingi zinakabiliana na changamoto kama zile,” amesema El Amran.

“Unaweza kuona klabu inamtaka mchezaji lakini mchezaji akashindwa kuonyesha uwezo wake kutokana na miundombinu, makocha wanashindwa kufikia malengo kutokana na kukosa fedha kuwapata wachezaji wanaowataka, kwahiyo mchango wake ulikuwa ni maisha halisi ya klabu nyingi za Afrika.”