Arusha. Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI) imeingia makubaliano ya uendeshaji wa hospitali ya Arusha Lutheran Medical Center (ALMC) kwa kipindi cha miaka 20 ijayo, hatua itakayoimarisha huduma za matibabu ya kibingwa ya magonjwa ya moyo katika mikoa ya Kanda ya Kaskazini.
Akizungumza katika mkutano na waandishi wa habari leo,Jumanne Desemba 16,2025 Mkurugenzi Mtendaji wa JKCI, Dk Peter Kisenge amesema makubaliano ya ubia huo yanaifanya ALMC kuwa tawi la tano linaloendeshwa na taasisi hiyo.
“Kwa wananchi wa Kanda ya Kaskazini tumepata tawi ambalo taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete itakua inaendesha Hospitali ya Arusha Lutheran Medical Center kwa miaka 20 na itakua ni kituo cha pamoja cha kutibu magonjwa ya moyo na magonjwa mengine yatatibiwa kwenye hii hospitali, ”amesema Dk Kisenge.
Amesema utekelezaji rasmi wa mkataba huo utaanza Januari Mosi, 2026 kwa kambi kubwa ya kuwapima wananchi magonjwa ya moyo lengo likiwa kuwafikishia wananchi huduma za kibingwa karibu badala ya kutumia gharama kubwa kuzifuata Dar es Salaam.
“Arusha ni eneo la utalii, kama mnavyojua watalii wanapokua wanapanga safari zao moja ya mambo wanayozingatia ni huduma za afya za kibingwa iwapo wataugua ghafla wakiwa safarini, hivyo uwepo taasisi yetu utachochea utalii wa matibabu kwa kuimarisha huduma ya magonjwa ya dharura na kuweka mtambo wa moyo unaosaidia kwa waliopata mshtuko wa moyo,”amesema Dk Kisenge.
Dk Kisenge ameongeza kuwa katika kipindi cha miaka miwili ijayo ya utekelezaji wa makubaliano hayo wataanza kufanya upasuaji wa moyo na kuwataka wananchi watumie hospitali hiyo kupata huduma za matibabu kwakua hospitali hiyo ina hadhi ya kimataifa ikitumia vifaa vya kisasa.
Amesema katika ufuatiliaji wa wagonjwa waliopata huduma watakua wakitumia shuka maalumu ambalo litakua likitoa taarifa ya maendeleo ya mgonjwa kwa siku saba kwa kutumia teknolojia ya akili unde (AI).
“Baada ya mgonjwa kuruhusiwa kwenda nyumbani tutaendelea kumfuatilia kwa siku saba kwa kutumia shuka maalumu tukiendelea kumwangalia.
Kama mgonjwa amefanyiwa upasuaji kupitia teknolojia hiyo tutaangalia mapigo ya moyo, tutaona unavyopumua, tutaona oksijeni yako kwenye damu na chochote kikitokea gari la wagonjwa litakuja kukuchukua kuokoa maisha,”amesema Dk Kisenge
Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa ALMC, Dk Goodwill Kivuyo amesema makubaliano hayo yamekuja baada ya hospitali hiyo inayomilikiwa na Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania, Dayosisi ya Kaskazini Kati kuomba kuingia ubia na Serikali mwaka 2023 na kufikia makubaliano mwaka 2025.
“Tunashukuru Serikali kukubali maombi yetu,taasisi yetu inaona hii ni hatua muhimu kwa sababu tumeingia makubaliano na taasisi kubwa nchini ,mnafahamu JKCI inayo matawi makubwa nchini na nje ya nchi, tunaona tumefanikiwa kufanya kazi pamoja nao lengo likiwa kuleta huduma karibu na wananchi,”amesema Dk Kivuyo.
Aidha, Dk Kivuyo ameongeza kuwa lengo kuu la kuanzishwa hospitali hiyo lilikua kutoa huduma bora kwa wananchi wa mikoa ya Kanda ya Kaskazini, nchi jirani na wageni wanaoingia nchini hivyo uwepo wa huduma za kimataifa utaiwezesha kuendelea kutambulika zaidi na kuendeleza malengo ya awali