Dar es Salaam. “Mtaani” au “duniani” kama maneno yasiyo rasmi yanayotumika kumaanisha maisha baada ya shule au chuo, hufikiriwa kama mahali pa mtu kusubiri kuelekezwa nini cha kufanya.
Ukweli ni tofauti. Dunia ni uwanja wa kutumia elimu yako kutatua matatizo ya jamii, siyo kusubiri maagizo.
Iwe utaamua kujiajiri au kuajiriwa, kuna sifa ambazo ni za msingi. Mtu haajiriwi ili afundishwe kila hatua ya kazi, bali huajiriwa atekeleze majukumu na alete thamani mpya. Dunia ya leo inahitaji watu wanaoleta suluhisho, si visingizio.
Katika safari hiyo, uwezo wa kuwasiliana kwa ufanisi ni jambo la msingi. Mawasiliano ni nguzo ya mafanikio katika kila unachokifanya.
Mawasiliano bora yanajumuisha kusikiliza, kuelewa na kujibu kwa usahihi. Lugha unayotumia hubeba elimu yako, ustaarabu wako na utambulisho wako.
Ndiyo maana ni muhimu kujifunza kuwasiliana vyema ukiwa bado shuleni au chuoni, ili jamii ione thamani ya elimu yako badala ya kuishusha kwa kushindwa kuzungumza au kuandika kwa weledi.
Vivyo hivyo, hakuna mafanikio bila ushirikiano. Wahenga walisema kidole kimoja hakivunji chawa. Bila kushirikiana na wenzako kazini au katika biashara, huwezi kufika mbali. Ushirikiano hukupa maarifa mapya, hukufungulia siri nyingi na hukuwezesha kufanya mambo makubwa.
Dunia ya sasa inahitaji watu wanaoweza kuunganisha wengine kwa lengo la pamoja, si wale wanaotengeneza fitina ili waonekane bora.
Msomi wa kweli pia anatambulika kwa uwezo wake wa kutatua matatizo. Msomi si mtatizaji, bali ni mtatuzi. Unaposaidia watu kutatua changamoto zinazowakosesha usingizi, unajijengea ushawishi, heshima na hata kipato. Haya ni mambo ya kujifunza mapema, ukiwa bado shule au chuo.
Katika mafanikio hayo, muda una nafasi ya kipekee. Wachina husema, “nchi ya dhahabu ni sawa na nchi ya muda, lakini huwezi kutumia nchi ya dhahabu kununua muda.” Mafanikio mengi yamefichwa katika matumizi sahihi ya muda.
Fanya mambo kwa wakati, toa ahadi zinazotekelezeka na uzitumie kwa muda uliokubalika. Kama alivyosema muungwana mmoja, ukitaka kazi ifanyike, mpe mtu mwenye majukumu; asiye na majukumu hudhani ana muda mwingi, kumbe muda umeshampita siku nyingi.
Aidha, taasisi na kampuni zinahitaji watu wanaoweza kufikiri kwa uhuru. Ufikiri huru huzaa mawazo mapya yenye tija na kuisukuma taasisi au kampuni mbele. Kufuata mawazo ya wengine bila kuyachambua na kuangalia athari zake za baadaye ni hatari. Elimu isiyojenga uwezo wa kufikiri si elimu kamili, bali ni mkusanyiko wa taarifa tu. Ufikiri ndiyo chanzo kikuu cha ubunifu.
Sambamba na hilo, maadili ni msingi usiopingika. Taasisi, kampuni na serikali vinahitaji watu wanaojua miiko ya kazi zao na wanaoishi kwa misingi ya uadilifu. Mtu mwenye maadili hutambua athari za kila kitendo chake, katika maisha ya kazi na hata baada ya kuondoka duniani. Daima anatamani kuacha alama njema katika kazi, jamii na kwa vizazi vinavyokuja.
Hatimaye, msomi bora ni yule anayejua kudhibiti hisia zake. Kujijua mwenyewe na kuwajua wengine ni msingi wa kuishi vizuri katika jamii. Hakuna ujinga mkubwa kama kumchukia mtu kwa sababu ya kukosolewa au kwa sababu ya hulka zake.
Mwanafalsafa wa China, Lao Tzu, aliwahi kusema: “Kujijua mwenyewe ni elimu; kuwajua wengine ni hekima.”
Kwa jumla, haya yote si mambo ya kusubiri baada ya kuhitimu. Ni misingi ya kujengwa ukiwa bado shuleni au chuoni. Dunia inasubiri kuona matokeo ya elimu yako, si kwa vyeti pekee, bali kwa mchango wako halisi katika kutatua matatizo ya jamii.
