Kanuni mpya kitanzi kwa madereva zaja, wenyewe wasema…

Dar es Salaam. Ili kupunguza ajali za barabarani zinazotokana na uchovu wa madereva, Mamlaka ya Udhibiti wa Usafiri Ardhini (Latra) imekuja na kanuni zitakazowabana madereva wa magari ya kibiashara.

Rasimu ya Kanuni za Usimamizi wa Hatari ya Uchovu kwa Madereva, 2025, inaweka wazi viwango vya saa za kuendesha kwa siku na kwa wiki, pamoja na mapumziko ya lazima kama sehemu ya mkakati mpana wa kudhibiti hatari ya uchovu katika usafiri wa umma na wa kibiashara.

Kwa mujibu wa kanuni zilizopendekezwa, dereva hataruhusiwa kuendesha gari la huduma ya umma kwa zaidi ya saa tisa ndani ya kipindi cha saa 24, wala kuzidi saa 48 za kuendesha ndani ya siku saba.

Pia, dereva hataruhusiwa kuendesha kwa zaidi ya saa tano mfululizo bila kuchukua mapumziko.

Ili kuimarisha usalama, kanuni hizo zinataka mapumziko yawe ya lazima, na madereva watalazimika kupata angalau saa 10 za mapumziko ndani ya kila saa 24, mapumziko ya dakika 30 baada ya kila saa tano za kuendesha mfululizo, na saa 24 za mapumziko mfululizo ndani ya siku saba za kazi.

Zaidi ya hayo, madereva watalazimika kuchukua mapumziko ya lazima kila baada ya saa nne za kuendesha kwa muda wa angalau dakika 10 hadi 20, ili kuhakikisha wako katika hali nzuri ya kuendesha.

Ili kuzipitia kanuni hizo, Wizara ya Uchukuzi, kwa kushirikiana na Mamlaka ya Udhibiti wa Usafiri wa Nchi Kavu (Latra), imepanga kufanya mkutano wa wadau unaotarajiwa kufanyika Desemba 22, 2025.

Desemba 31, 2024, Rais Samia Suluhu Hassan, akitoa salamu za mwaka mpya, alitoa maelekezo kwa Wizara ya Mambo ya Ndani na Jeshi la Polisi kuongeza mikakati ya kuzuia ajali zinazosababishwa na uzembe.

Katika maelezo yake, alirejea takwimu za Jeshi la Polisi zilizoonesha kulitokea jumla ya ajali 17,315 kwa mwaka huo, ambapo Watanzania 1,715 walipoteza maisha. Vifo hivyo vilitokea kuanzia Januari hadi Desemba 2024.

Akizungumza na The Citizen, Mkuu wa Huduma za Kisheria wa Latra, Mwadawa Sultan, amesema kanuni hizo zilizopendekezwa zinalenga kuziba pengo kubwa katika usimamizi wa usalama barabarani kwa kutambua rasmi uchovu wa dereva kama chanzo kinachoongoza cha ajali za barabarani.

“Ingawa sheria zilizopo zinahusu masuala kama leseni na adhabu za mwendo kasi, bado hazijashughulikia ipasavyo hatari zinazotokana na uchovu wa dereva,” amesema.

Akitambua kuwa Tanzania inaendesha mfumo wa usafirishaji wa saa 24, Sultan amebainisha faida zake, lakini akaonya juu ya hatari zinazoweza kujitokeza.

“Ajali zinaweza kutokea si kwa sababu ya mwendo kasi pekee, bali pia pale dereva anapokuwa amechoka, mgonjwa au anapolala, hali inayoweza kusababisha ajali kubwa,” amesema.

Kwa mujibu wake, kuzingatia mwendo kasi pekee hakutoshi kushughulikia chanzo muhimu cha ajali za barabarani. “Dereva anaweza asiwe anaendesha kwa kasi, lakini uchovu bado unaweza kusababisha madhara makubwa kwa abiria na watumiaji wengine wa barabara.”

Amesema baadhi ya kampuni binafsi nchini tayari zinatekeleza mifumo ya usimamizi wa uchovu, ikiwemo matumizi ya vifaa vya tahadhari vinavyowaonya madereva wanaoonesha dalili za kuchoka.

“Hatua hizi zinalenga kuzuia madereva kufanya kazi kupita kiasi, jambo ambalo ni hatari kwa abiria, watumiaji wengine wa barabara na sekta nzima ya usafiri,” amesisitiza.

Kanuni zilizopendekezwa zinakataza wazi dereva au mtoa huduma kuruhusu gari kuendeshwa endapo dereva ana uchovu au anahisiwa kuwa hana uwezo wa kuendesha, kwa kuzingatia hatari kwa abiria, watumiaji wengine wa barabara na miundombinu ya barabara.

Watoa huduma watalazimika kuandaa na kutekeleza Mpango wa Usimamizi wa Hatari ya Uchovu, unaoeleza jinsi saa za kuendesha, mapumziko, mabadilishano ya madereva na ufuatiliaji wa uchovu vitakavyosimamiwa. Mipango hiyo italazimika kuidhinishwa na Latra na kufanyiwa mapitio kila pale mabadiliko ya kiutendaji yatakapofanyika.

Kwa safari ndefu zinazozidi saa nane za kuendesha, kanuni zinataka matumizi ya madereva wenza, hususan kwa mabasi ya masafa marefu, pamoja na vituo maalumu vya kubadilishana madereva.

Magari ya kubeba mizigo na ya abiria wa mijini pia yatalazimika kuhakikisha dereva anapumzika au anabadilishwa baada ya kufikia kikomo cha saa nane.

Madereva, kwa upande wao, watalazimika kutamka rasmi hali yao ya afya na uwezo wa kuendesha kabla ya kuanza kila safari, kurekodi kwa usahihi saa za kazi na mapumziko katika daftari rasmi, na kuripoti uchovu wanaposhindwa kuendelea kuendesha.

Kushindwa kufanya hivyo kunaweza kusababisha adhabu au kusimamishwa kwa vyeti vyao.

Kanuni hizo pia zinampa Latra mamlaka ya kusimamisha au kufuta leseni na vyeti vya madereva kwa ukiukwaji wa mara kwa mara, hasa pale kutokuzingatia kunapohatarisha usalama wa umma.

Madereva na watoa huduma wanaweza pia kukabiliwa na faini au kifungo  jela endapo watapatikana na hatia ya kukiuka masharti hayo.

Pia, kanuni zinatilia mkazo elimu, zikihitaji madereva na watoa huduma wawe na uelewa wa msingi kuhusu chanzo na kinga ya uchovu, ikiwemo hatari za kufanya kazi kwa muda mrefu, kukosa usingizi wa kutosha, msongo wa mawazo na matumizi ya pombe.

Maofisa wanaamini kuwa kanuni hizo zitakapotekelezwa kikamilifu, zitapunguza kwa kiasi kikubwa ajali zinazotokana na uchovu na kuongeza usalama na nidhamu zaidi katika sekta ya usafiri wa barabarani.

Akizungumzia suala hilo, Mwenyekiti wa Chama cha Wamiliki wa Malori Tanzania (Tamstoa), Chuki Shaabani, amesema muongozo wa Serikali unaolenga kudhibiti muda wa uendeshaji wa vyombo vya usafiri ni hatua nzuri itakayosaidia kupunguza ajali za barabarani.

Shaabani amesema Tamstoa ilishaanza kutekeleza utaratibu huo muda mrefu, kwa kuweka kikomo cha madereva kuendesha magari hadi saa 12 jioni.

“Serikali ni kama imekuja kugongea msumari, sisi tulishaanza kudai, na kama wamiliki, tulishaanza kuweka muda wa madereva kuendesha magari yetu mwisho saa 12 jioni,” amesema Shaabani.

Ameeleza uamuzi huo ulitokana na sababu kuu mbili, ikiwemo kujikinga na ajali zinazochangiwa na uchovu wa madereva kutokana na safari ndefu na usalama wa mizigo, kwani malori hubeba mizigo mikubwa ikiwemo madini kama shaba (copper), hivyo kusafiri usiku kuna hatari ya kuibiwa na baadaye kushindwa kulipwa na mwajiri.

Shaabani amesema hatua ya Serikali kuja na muongozo huo itasaidia kuimarisha utekelezaji kwa wamiliki wote wa malori, kwani watakuwa na wajibu wa kuuzingatia kwa maslahi mapana ya usalama na kuboresha sekta ya usafiri nchini.

Kwa upande wake, Msemaji wa Chama cha Wamiliki wa Mabasi Tanzania (Taboa), Mustapha Mwalongo, amesema wanaunga mkono uamuzi huo, huku akieleza walishaanza kuchukua tahadhari kwa kuajiri madereva wawili kwa kila basi.

“Ni utaratibu tuliouanzisha baada ya kuongezeka kwa ajali. Kila safari yenye umbali wa kilomita 700 tunahakikisha basi linakuwa na madereva wawili wa kupokezana,” amesema Mwalongo.

Hata hivyo, Mwalongo amesema hawezi kuzungumzia kwa undani muongozo wa Serikali kwa sasa, kwa kuwa bado haujawafikia rasmi.

“Tunasubiri kuupata na kuusoma ili kuona ni mambo gani mapya yameainishwa kabla ya kuanza kuutekeleza,” amesema.