Arusha. Matumizi makubwa ya kemikali, mbolea nyingi na dawa za kuulia wadudu yanayofanywa na wakulima nchini, yameelezwa ni chanzo cha uharibifu wa ardhi hali ambayo inachangia kwa kiasi kikubwa usalama mdogo wa chakula.
Matumizi hayo pia yameelezwa kuwa hayampi mkulima uhakika kupata mazao mengi licha ya kutumia dawa nyingi wakati wa kilimo, hivyo kushauriwa kulima kilimo ikolojia kinacholenga kuangalia ustawi wa kilimo ili kuwezesha matokeo chanya kiuchumi, kiafya na kimazingira.
Hayo yameelezwa leo Jumanne Desemba 16,2025, Ofisa Masoko kutoka Shirikisho la Wakulima Wadogo Tanzania (Shiwakuta), Jimmy Mongi, alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari walipotembelea soko la mazao ya kilimo ikolojia, Kilombero jijini Arusha.
Amesema kuwa matumizi ya mbolea ya asili yana faida kubwa kwenye ardhi kwa kuwa na mazingira yote yanakuwa salama kutokana na kutokuwepo kwa kemikali kwenye samadi, huku vyakula vinavyozalishwa vikiwa salama na kumlinda mlaji.
Amesema kutokana na baadhi ya wakulima kuwa na matumizi makubwa ya kemikali, wameendelea kupitia vikundi kutoa elimu kwa wakulima ili kuondoa dhana potofu iliyojengeka kuwa kilimo ikolojia ambacho hutumia njia ya asili hakiwezi kuwa cha kibiashara.
Amesema kilimo ikolojia kinatumia njia na mbinu asili kuanzia uandaaji wa shamba, mbolea ambapo kinazingatia usalama wa chakula kwa walaji na usalama wa ardhi hasa katika kipindi hiki ambacho dunia inakabiliana na mabadiliko ya tabianchi, ambayo yameleta athari kubwa kwenye kila sekta ikiwemo kilimo.
“Kuna mtazamo hasi kwenye jamii kuwa kilimo ikolojia hakiwezi kufanywa ekari na ekari hii sio kweli na uzuri mmejionea hiki ni kilimo salama ambacho mkulima anaweza kupata mazao mengi na soko ni kubwa kama mnavyojionea lakini afya ya walaji ikawa ni salama na ardhi yetu pia ikawa salama vilevile, kwani matumizi ya kemikali nyingi huathiri rutuba ya ardhi,” amesema.
“Kuna mazao yanatoka mfano Uganda (limao), Rwanda tunawauzia vitunguu, Kenya wananunua viazi, karoti na mahindi na sisi pia tunanunua mazao toka kwao kutegemea na msimu, hivyo mnaona ilivyo muhimu kote kuhakikisha mazao yanakuwa na ubora na salama.”
Meneja wa Soko la Kilombero, Jeremia Katemi, amesema kuwa mbali na usimamizi wa soko hilo pia wamekuwa wakishirikiana na wadau wengine ikiwemo Mtandao wa Wakulima Wadogo mkoa wa Arusha (Mviwaarusha) na Shiwakuta,kuhusu kilimo ikolojia ambapo wamekuwa wakiunganishwa na wakulima wa kilimo hicho.
Amesema kuwa soko hilo linapokea matunda na mbogamboga kutoka nchi mbalimbali ikiwemo Rwanda, Uganda na Kenya ambapo udhibiti wa usalama na ubora wa chakula hufanyika mipakani hivyo kilimo ikolojia kikitumika kote usalama wa chakula utakuwa mkubwa kutokana na matumizi madogo ya mbolea na kemikali.
Mmoja wa wafanyabiashara wa matunda na mbogamboga sokoni hapo, Mwajuma Ally, amesema mazao yanayozalishwa kwa mfumo wa kilimo ikolojia ni salama na kuwa inasaidia kuongeza usalama kwa walaji.
