Kitambala atabiriwa makubwa Azam FC

BEKI wa zamani wa Yanga, Djuma Shaban amesema baada ya mshambuliaji wa Azam, Jephte Kitambala kuifunga Simba, timu zingine zinatakiwa zijipange kumzuia, kwani atafunga sana.

Kitambala alisajiliwa na Azam msimu huu akitokea AS Maniema Union ambayo ilimchukua akitokea TP Mazembe, huku Desemba 7 mwaka huu akifunga bao moja wakati Azam ikiichapa Simba 2-0 katika mechi ya Ligi Kuu Bara.

Akizungumza na Mwanaspoti, Djuma amesema anamfahamu vyema Kitambala, hivyo kabla hajatua Azam, alifahamu atakwenda kuisaidia timu hiyo.

Amesema kama Kocha Florent Ibenge ndiye aliyemchagua asajiliwe, basi hajafanya makosa kwani mshambuliaji huyo ana uwezo mkubwa wa kutengeneza na kufunga mabao.

“Ili uweze kumzuia Kitambala kirahisi, unahitaji kuwa na beki mbishi kama Ibrahim Bacca kwani ni mshambuliaji mwenye akili sana.

“Ukiacha uwezo wake wa kufunga, ana uwezo wa kupambana kwani ana nguvu za mwili na ni ngumu kwa mabeki kumzuia kirahisi, japo wapo wachache ambao watamsumbua kidogo.”

Aliongeza kuwa: “Azam itakwenda kunufaika sana na uchaguzi waliofanya kumsajili Kitambala, pia uwepo wa kocha Ibenge kuna vitu atamuongezea na watafikia malengo ya msimu huu.”