Dar es Salaam. “Mvumilivu hula mbivu.” Methali hii inajidhihirisha wazi kupitia safari ya maisha ya Mkurugenzi wa Taasisi ya Her Initiative, Lydia Moyo.
Ni safari iliyoanza katika mazingira duni ya shule ya kata na leo imegeuka kuwa chemichemi ya matumaini kwa maelfu ya mabinti wanaopambana kutimiza ndoto zao.
Aianza safari yake ya elimu katika Shule ya Msingi Kimara Baruti, alikohitimu mwaka 2006.
Mwaka uliofuata alichaguliwa kujiunga na Shule ya Sekondari King’ongo, ambako mazingira ya kujifunzia yalikuwa magumu kuliko alivyotarajia.
Anasimulia kuwa wakati huo walimu walikuwa wachache, baadhi ya madarasa hayakuwa yamekamilika, na hakukuwa na maktaba wala maabara kama mambo muhimu katika kujifunza masomo ya sayansi.
“Nilivyofika King’ongo, baadhi ya madarasa yalikuwa bado kwenye ujenzi. Hakukuwa na maktaba, maabara wala rasilimali za kutosha za kujifunzia,” anasema.
Zaidi ya hayo, baadhi ya wanafunzi walilazimika kutembea hadi kilomita tatu ili kufika shuleni. Licha ya mazingira hayo magumu, Lydia alijiaminisha kuwa changamoto hizo hazitakuwa kikwazo cha kufikia malengo yake ya masomo.
Akiwa na umri mdogo lakini maono makubwa, alianza kuchukua hatua za makusudi kuhakikisha anajenga msingi imara wa elimu.
Alijiwekea malengo ya muda wa kusoma, akahakikisha anafuata mpango wa masomo kwa nidhamu, na kutumia ipasavyo maarifa aliyoyapata darasani. Pale ambapo hakuielewa mada, hakuwa na aibu kuuliza walimu au kujadiliana na wenzake.
“Nilizingatia yale niliyofundishwa. Nikikwama, nauliza. Nilijenga urafiki na wanafunzi wa shule mbalimbali ili tujifunze kwa pamoja. Hilo lilinisaidia kujua mbinu tofauti za kujifunza,” anaeleza.
Hatua hizo, pamoja na ukaribu wake na walimu waliomsaidia pale alipohitaji ushauri, zilimsukuma kufanya vizuri kitaaluma.
Matokeo yake, Lydia aliibuka kuwa mmoja wa wanafunzi wawili pekee waliopata daraja la kwanza shuleni hapo na baadaye kujiunga na kidato cha tano, ndoto aliyoiota kwa muda mrefu.
Hata hivyo, mafanikio yake hayakuondoa maumivu aliyobeba moyoni alipoona baadhi ya wanafunzi wenzake wakikatisha masomo.
Baadhi yao walishindwa kuendelea kwa sababu ya umaskini, mimba za utotoni au changamoto nyingine za kijamii.
“Moyoni nilikuwa na maumivu juu ya watu ambao safari yao iliishia njiani. Nilijiuliza ni kwa namna gani ninaweza kuwasaidia wasikate tamaa,” anasema.
Akiwa kidato cha tano, Lydia pamoja na wanafunzi wenzake wawili waliamua kuanza kuchukua hatua. Walijifunza haki za wasichana kisha wakaanza kuzielimisha kwa wenzao na shule jirani. Hatua hiyo ilikuza kiu yake ya kusaidia wasichana kutambua thamani yao na kupigania ndoto zao.
Ndiyo ukawa mwanzo wa kampeni mbalimbali alizoanzisha; kampeni zilizolenga kumwezesha mtoto wa kike kujitambua na kutimiza malengo yake. Walileta watu wa mfano kutoka katika sekta mbalimbali kuzungumza na wanafunzi, hatua iliyowafanya mabinti wengi kuanza kujiamini na kutazama mbele kwa matumaini mapya.
Alipofika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), ari hiyo ilizidi kuongezeka. Mbali na kuwafundisha wasichana kuhusu haki zao, aliwatia moyo kujifunza ujasiriamali ili waweze kujitegemea kiuchumi.
Kupitia jukwaa alilolianzisha na kulipa jina la ‘Panda’, aliandaa mafunzo ya kuwajengea mabinti ujuzi wa kujiajiri na kubuni miradi midogo midogo.
Baada ya kuhitimu chuo na kufanya kazi kwa muda wa miaka miwili, Lydia alihisi wito wa ndani uliomtaka ajikite kikamilifu katika harakati za kuwawezesha wasichana.
Aliamua kuacha kazi na kuwekeza nguvu zake zote katika Shirika la Her Initiative, hatua ambayo haikuwa rahisi hata kidogo.
Changamoto ya kukosa ufadhili kuendesha miradi aliyoianzisha ilimfanya afikie mahali pa kukata tamaa. Mwaka 2021, hali ilikuwa mbaya zaidi. Rasilimali zilikuwa finyu, na taasisi ilikosa hata pesa za uendeshaji.
“Mwaka 2021 ilionekana kama jahazi linazama. Nilikuwa nimewekeza kila kitu katika taasisi lakini hatukuwa na fedha. Iliniuma sana,” anasema.
Hata hivyo, maumivu hayo ndiyo yakawa chanzo cha ujasiri mpya. Aliandika barua ya wazi kwa wafadhili, akiwaomba wawekeze katika miradi ya kumuendeleza kijana, hasa msichana. Barua hiyo ilisambaa mitandaoni na kuibua hamasa mpya.
“Hapo ndipo taasisi yetu ilipopata sura mpya. Kufikia Novemba 2021, wadau mbalimbali walijitokeza kufanya kazi nasi,” anasema.
Leo, Her Initiative inatekeleza miradi kadhaa inayolenga kuwawezesha vijana kiuchumi, kuwapa elimu ya ujasiriamali na kuwajengea uwezo wa kutambua haki zao. Kazi zake zimemletea Lydia tuzo nyingi, ikiwemo ya kimataifa ya Global Citizen.
Lydia anatoa wito mahsusi kwa vijana wanaopambana na safari ya elimu. Anasisitiza kuwa changamoto zinazowakabili ikiwemo hali ngumu ya kiuchumi, zisigeuke kuwa sababu ya kuacha shule au kutupa ndoto zao.
“Mnapaswa kufahamu kwamba hata baadhi ya viongozi na wataalamu maarufu walipitia magumu, lakini hawakukata tamaa,” anasema.
Anawahimiza vijana wasihofu kuwa na ndoto kubwa, waamini ndani yao kuwa wanaweza kuwa vile wanavyotaka. Ili kufanikiwa, anawashauri kumtanguliza Mungu, kujiamini, kufanya kazi kwa bidii na kujifunza kutoka kwa waliotangulia.
“Ni muhimu kuheshimu mchakato wa kufikia malengo. Mafanikio ni safari ya milima na mabonde, hayapatikani kwa urahisi,” anasisitiza.
Safari ya Lydia ni ushahidi kwamba hata kutoka katika mazingira duni, ndoto zinaweza kutimia pale zinapoambatana na juhudi, nidhamu na moyo wa kutokata tamaa.
