:::::
Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) mnamo Disemba 16, 2025, imekamata shehena kubwa ya mafuta ya kupikia ya magendo, jumla ya madumu 18,000 yaliyokuwa yakiingizwa nchini kinyume na taratibu za kiforodha kupitia Bandari ya Kunduchi, jijini Dar es Salaam.
Kamishna Mkuu wa TRA, Bw. Yusuph Juma Mwenda, alizungumza mara baada ya zoezi hilo na kueleza kuwa bidhaa hizo za magendo zimekuwa tishio kwa uchumi wa nchi, kwa kuwa zinapunguza mapato ya serikali na kudhoofisha ukuaji wa viwanda vya ndani.
Aidha, aliongeza kuwa bidhaa hizo zisizopitia ukaguzi wa mamlaka husika huweza kuwa hatari kwa afya za walaji, hivyo ni wajibu wa kila mmoja kushiriki katika kuzuia biashara hiyo haramu.
TRA imesisitiza kuwa itaendelea kuchukua hatua kali dhidi ya wahusika wa biashara za magendo, huku ikihamasisha wananchi kushirikiana katika kutoa taarifa ili kulinda uchumi wa Taifa.







