Ruvuma. Mamia ya watu wamejitokeza katika kijiji cha Luanda kilichopo Halmashauri ya Mbinga mkoani Ruvuma, kwa ajili ya kuhitimisha safari ya mwisho ya aliyekuwa Mbunge wa Peramiho (CCM), Jenista Mhagama.
Jenista ambaye amekuwa mbunge wa Peramiho kuanzia mwaka 2005, alifariki dunia Alhamisi, Desemba 11, 2025 jijini Dodoma, kwa matatizo ya ugonjwa wa moyo.
Katika maziko hayo, mamia ya watu wamejitokeza kushiriki ikiwemo idadi kubwa ya wabunge wa Bunge la Tanzania wakiongozwa na Spika, Mussa Azzan Zungu, Waziri Mkuu, Mwigulu Nchemba na viongozi wengine wa Chama cha Mapinduzi na vyama vingine vya kisiasa.
Mbali na viongozi hao, wakazi mbalimbali wa mji wa Peramiho na waombolezaji kutoka maeneo tofauti wamesafiri mpaka kijijini hapa kwa ajili ya kutoa heshima zao za mwisho katika maziko yake yanayotarajiwa kufanyika alasiri leo.
Mwili wa marehemu uliwasili katika kijiji cha Ruanda tayari kwa ibada fupi ya misa, kabla ya kupelekwa rasmi katika makaburi ya Senta B kwa ajili ya maziko.
Akisoma wasifu wa marehemu jana, Katibu wa Bunge, Baraka Leonard, alisema Jenista Mhagama alizaliwa Juni 23, 1967, katika Kijiji cha Parangu, Peramiho, mkoani Ruvuma.
Alipata elimu ya msingi Parangu na kuendelea na elimu ya sekondari kuanzia mwaka 1982 hadi 1985, kabla ya kujiunga na Chuo cha Ualimu Korogwe, ambako alihitimu masomo ya ualimu.
Mwaka 1999, alipata Shahada ya Kwanza ya Uongozi na Utawala kutoka Chuo Kikuu cha Cambridge, na hadi anafariki dunia alikuwa akiendelea na masomo ya Shahada ya Uzamili (Masters) kwa njia ya masafa nchini Uingereza.