Maofisa Uhamiaji watatu kunyongwa kwa mauaji

Kigoma. Yametimia! Ni maneno unayoweza kuyatumia kuelezea hukumu ya Mahakama Kuu kwa waliokuwa maofisa watatu wa Uhamiaji, kuhukumiwa adhabu ya kifo kwa kumuua Mtanzania waliyemshuku sio raia wa Tanzania.

Waliohukumiwa kunyongwa hadi kufa ni Fredrick Kyomo, Joachim Trathizius na Mabruki Hatibu ambao wamepatikana na hatia ya kumuua Enos Elias, ambaye ni mkazi wa Kakonko mkoani Kigoma.

Hukumu hiyo imetolewa jana, Jumatatu Desemba 15, 2025 na Jaji Augustine Rwizile wa Mahakama Kuu kanda ya Kigoma, akisema ushahidi umethibitisha hakuna mtu au watu wengine waliofanya mauaji hayo isipokuwa maofisa hao.

“Kwa kuegemea msingi wa ushahidi wa namna walivyomkamata, kumpiga na kumpeleka mahali panapojulikana, kisha kukutwa amekufa ni vitendo tosha vya kuthibitisha washitakiwa walifanya hivyo kwa nia mbaya,” amesema Jaji Rwizile.

Elias alikamatwa na maofisa hao katika kizuizi cha Kihomoka wilayani Kakonko Oktoba 27, 2023 na kupelekwa ofisi za Uhamiaji kwa mahojiano na alifanikiwa kuwasiliana na ndugu zake ili wampelekee Kitambulisho cha Taifa (Nida).

Hata hivyo, ndugu walipofuatilia katika ofisi hizo waliambiwa alikuwa ameachiwa Oktoba 28, 2023 lakini akawa hapatikana na wala simu yake haipatikani hadi mwili wake ulipopatikana Oktoba 29, 2023 na kuzikwa kwa kukosa ndugu.

Iligundulikaje ndiye Elias?

Novemba 9, 2023 Ofisi ya Mkuu wa Upelelezi Mkoa wa Kigoma (RCO), ilimtuma kachero wake kwenda Kakonko kuchunguza kutoweka kwa Elias, aliyekuwa mikononi mwa Uhamiaji kwa tuhuma za kutokuwa raia.

Kwa mujibu wa ushahidi uliotolewa mahakamani na mashahidi wa Jamhuri, marehemu Elias alikuwa ni Mtanzania aliyezaliwa Wilaya ya Kakonko na ndugu zake wengine wa kuzaliwa ni Anjelina, Advera, Levina na Plaxeda.

Oktoba 27, 2023, Elias akiwa katika usafiri wa umma akisafiri ndani ya Mkoa wa Kigoma, alikamatwa na maofisa uhamiaji katika kizuizi cha Kihomoka wakimshuku kuwepo nchini kinyume cha sheria kwa maana kuwa sio raia wa Tanzania.

Maofisa watatu waliokuwa washitakiwa katika kesi hiyo, Fredrick Kyomo, Joachim Trathizius na Mabruki Hatibu, walimpeleka katika ofisi yao kwa ajili ya mahojiano na akawaomba wamwachie huru kwani yeye ni raia wa Tanzania.

Hata hivyo, walikataa kumwachia wakidai kuwa hakuwa na Nida na ili aweze kuachiwa, alitakiwa kuwasilisha kitambulisho cha mmoja wa wazazi wake, hivyo akawekwa mahabusu hadi Oktoba 28, 2023.

Aliwasiliana na ndugu zake ambao ni Anjelina Elias aliyekuwa shahidi wa 5 na Leopard Salvatory kwa mara ya mwisho Oktoba 28, 2023 wakati akisubiri kitambulisho cha Nida cha mama yake mzazi ili aweze kuachiwa huru.

Ingawa maofisa uhamiaji hao walieleza kuwa walimwachia huru siku hiyo ya Oktoba 28, 2023 baada ya kumalizana naye kuhusu suala lake la uraia, ndugu zake waliokuwa wakimfuatilia hawakufanikiwa kuwasiliana naye na akawa ametoweka.

Katika Kijiji cha Chilambo kilichopo Wilaya ya Kakonko, kuna vilima vya Kachikiri na Kichacha ambapo katika eneo hilo kuna njia ya kwenda Burundi.

Oktoba 29, 2023, wakati wanarudi nyumbani baada ya doria, shahidi wa tano wa Jamhuri, Pius Paulo aliyekuwa Mwenyekiti wa Kijiji cha Chilambo akiwa na Yolam Kasase na Marco Joseph, walikuta mwili umetelekezwa katika vilima hivyo.

Waliamua kuwajulisha polisi na jioni, shahidi wa pili na kachero mwenye Cheo cha Koplo, Hamis aliyekuwa shahidi wa tatu wakiongozana na shahidi wa kwanza, Sharifu Husein ambaye ni tabibu walifika katika eneo hilo.

Pamoja na watu wengine, walikwenda eneo ambalo mwili huo ulikuwepo, ulichunguzwa na kuthibitika kuwa alikuwa ni mfu na iliamuliwa kuwa, kwa vile hajatambuliwa basi uongozi wa kijiji utafute eneo na umzike na ilifanyika.

Mwili unafukuliwa na kutambuliwa

Novemba 9, 2023, ASP Josephat Pombe aliyekuwa shahidi wa saba alitumwa kutoka Ofisi ya RCO Kigoma kwenda Kigoma kusaidia upelelezi wa kutoweka kwa Elias, siku iliyofuata alikutana na faili la mwili wa mtu uliozikwa Chilambo.

Shahidi huyo alifanikiwa kupata amri ya Mahakama ya kufukuliwa kwa mwili huo, ambapo aliwaita ndugu wa Elias akiwamo Angelina na mama yake na kwa kusaidiana na viongozi wa kijiji waliozika mwili, walisaidiana kuufukua.

Mwili huo ulikuwa umeharibika, mama mzazi aliutambua kuwa ni mwili wa mtoto wake hivyo wakaruhusiwa kuuchukua na kwenda kuuzika.

Kutokana na mtiririko wa matukio ya kukamatwa kwa Elias na baadaye kutoweka, maofisa hao watatu walikamatwa na kushitakiwa kwa mauaji ya Elias lakini walikanusha kuhusiana na mauaji hayo hadi walipotiwa hatiani kwa mauaji.

Baadhi ya mashahidi wa Jamhuri wakiwamo ndugu wa marehemu, walielezea namna walivyopata taarifa za kukamatwa kwa ndugu yao, walivyofuatilia na baadaye mmoja wa ndugu zao kuanza kufuatiliwa hadi akaamua kutoroka.

Ndugu hao walielezea namna ndugu yao alivyowapigia simu na kuwaeleza kuwa kinatakiwa kitambulisho cha Nida cha mama yao, lakini walipokwenda kukipeleka, maofisa waliokuwa wanamshikilia waliwaeleza kuwa tayari walimwachia.

Kulingana na ushahidi huo, Jaji alisema hakuna ubishi, alikuwa mikononi mwa maofisa Uhamiaji kabla ya kutoweka kwake na kupatikana akiwa marehemu.

Shahidi wa saba wa Jamhuri ambaye ni ASP Pombe alieleza kuwa baadhi ya maingizo (entry) yaliyohusu kukamatwa kwa marehemu yalifutwa na baada ya Jaji kupitia kumbukumbu hizo, alibaini zilifutwa baada ya mwili wa Elias kupatikana.

Ushahidi wa shahidi wa sita wa Jamhuri ambaye ni mgambo ndio ambao ulitoa mwanga wa nini kilitokea, alieleza kuwa Oktoba 27, 2023, marehemu alikamatwa na washitakiwa na kupelekwa ofisini kwao kwa mahojiano.

Akiwa hapo, alimsikia Eliass akiwasiliana na ndugu zake ili wamletee kitambulisho cha Nida cha mama yake mzazi lakini hakikupelekwa kwa haraka na ndipo walipoanza kumwadhibu kwa kumpiga kwa fimbo katika ofisi yao hiyo.

Alieleza kuwa, Fredrick Kyomo ndio alianza kumpiga kwa fimbo na baadaye aliingia Kapifu na kumuuliza kama ana kitambulisho cha Nida na alipomwambia hana, alianza kumpiga kwa kutumia kipande cha chuma kilichokuwamo ofisini.

Kwa mujibu wa shahidi huyo, ilipofika saa 11 jioni, washitakiwa hao walimpakia kwenye gari na kwenda naye kusikojulikana na baada ya dakika 30, ni Hatibu pekee ndio alirudi mwenyewe kwenye gari na ndipo baada alisikia wameua.

Katika hukumu yake, Jaji amesema ushahidi wa shahidi wa sita wa Jamhuri unaonesha kuwa marehemu alipigwa kwa fimbo na kipande cha chuma na kwamba ni mshitakiwa wa kwanza alianza kumpiga kisha washitakiwa wengine.

Ndugu wa marehemu aitwaye Leopord ndiye alitumwa kufuatilia kuhusu ndugu yake lakini walipofika maofisa hao wakamwambia kuwa jina lake halikuwamo miongoni mwa watu ambao wako kwenye kumbukumbu zao.

Lakini shahidi wa tano alipozungumza na Elias akiwa ofisi ya uhamiaji alimweleza kuwa alimuona akiwa amedhoofu na alikuwa hajala chakula tangu alipokamatwa.

“Shahidi wa sita alisema (marehemu) alipigwa na alipodhoofika aliingizwa kwenye gari na kupelekwa kusikojulikana. Ina maana mshitakiwa wa tatu anayedaiwa kumchukua alitakiwa aeleze mahali alipompeleka,” amesema Jaji Rwizile.

Jaji amesema kumbukumbu zinaonesha hakuna shahidi hata mmoja wa Jamhuri anayethibisha kuwa aliona washitakiwa wakifanya mauaji hayo na hata shahidi wa sita aliona wakimpiga, lakini hakuona wakimuua.

“Kwa vyovyote vile, shahidi wa sita aliona washitakiwa wakimpiga marehemu tena ndani ya ofisi yao na sio moja kwa moja kuwa ni kwa kipigo hicho ndio kilisababisha kifo chake. Kwa maneno mengine ushahidi wote ni wa mazingira.”

Jaji huyo amesema ushahidi ulionesha kuwa mwili ule ulipoonekana ulikuwa na michubuko kwenye miguu na maeneo mengine ya mwili na kwamba alikufa kutokana na majeraha kichwani yaliyosababishwa na kupigwa na kitu butu.

Jaji amesema kwa kuzingatia ushahidi, inatosha kuthibitisha kuwa ni washitakiwa hao ndio waliofanya mauaji hayo hasa ushahidi wa shahidi wa sita aliyeona wakimpiga na aina ya silaha walizozitumia.

“Alipigwa kwa fimbo maeneo mbalimbali ya mwili na baadaye kupigwa na kipande cha chuma. Kwangu mimi naona alikufa kutokana na mateso yaliyosababishwa na washitakiwa walioko mbele ya mahakama,” amesema Jaji.

Alisema kwa namna walivyomkamata, kumshikilia, kumpiga na kumpeleka eneo wanalolijua na baadaye kupatikana akiwa mfu, ni ushahidi unaotosha kuthibitisha kuwa washitakiwa hao ndio walimuua Elias kwa kukusudia