Dar es Salaam. Marekani imesema iko tayari kuipa Ukraine hakikisho la usalama linazofanana na la Jumuiya ya Kujihami ya Mataifa ya Magharibi (Nato), ili kulinda makubaliano ya kusitisha mapigano yanayoendelea nchini humo.
Wakati Marekani ikitoa hakikisho hilo kwa Ukraine, suala la udhibiti wa ardhi, hususan Donbas, bado limekuwa kikwazo kikubwa cha kufikiwa kwa amani Ukraine ambako mashambulizi yamekuwa yakiathiri amani na shughuli za kiraia.
Marekani imetangaza kuwa ipo tayari kutoa dhamana za usalama thabiti kwa Ukraine, zitakazofanana na zile za Nato kuhusu ulinzi wa pamoja, iwapo makubaliano ya kusitisha mapigano yatapatikana.
Kauli hiyo ilitolewa jana, Jumatatu Desemba 15, 2025 baada ya mazungumzo yaliyofanyika Berlin kati ya maofisa wa Marekani, viongozi wa Ulaya na ujumbe kutoka Kyiv, ambao pamoja na mambo mengine ulilenga kuangazia hali ya amani katika mapigano yanayoendelea Ukraine.
Katika kikao hicho, Maofisa wa Marekani walisema dhamana hiyo ya kiusalama inalenga kuzuia Russia kuvunja makubaliano yoyote ya amani, wakiongeza kuwa wanatarajia Moscow itayakubali masharti ya kusitisha mashambulizi yake Ukraine.
Hata hivyo, inaripotiwa kuwa hawakutoa maelezo ya kina kuhusu suala la uhuru na udhibiti wa ardhi ya Ukraine litakavyoshughulikiwa, licha ya kusisitiza kusitishwa kwa mapigano na kuipatia ulinzi nchi hiyo dhidi ya mashambulizi.
Rais wa Ukraine, Volodymyr Zelensky, alielezea mazungumzo hayo kuwa mazuri lakini magumu, akisisitiza kuwa Kyiv inahitaji ufafanuzi wa wazi kuhusu dhamana za usalama zitakazotolewa kabla ya kukubali makubaliano mengine.
Kwa muda mrefu, Ukraine imekuwa ikidai dhamana imara ili kuhakikisha Russia haitaishambulia tena baada ya kusitishwa kwa mapigano, hatua ambayo imekuwa ngumu kufikiwa kutokana na mashambulizi kuendelea kutokea.
Kwa upande mwingine, Marekani pia ilionya kuwa ofa hiyo ya dhamana za usalama haitabaki mezani kwa muda mrefu bila maamuzi ya haraka, badala yake itatumia kama njia ya haraka kurejesha amani huku hatua zaidi zikichukuliwa.
Inaelezwa kuwa kwa mara ya kwanza, Zelensky ameonyesha kuwa Ukraine inaweza kuacha matarajio ya kujiunga na Nato ikiwa itapata dhamana thabiti za usalama kama sehemu ya makubaliano yaliyofikiwa.
Licha ya maendeleo hayo, eneo la mashariki mwa Donbas bado ni chanzo kikuu cha mvutano, ambapo Marekani inapendekeza kuanzishwa kwa eneo huru la kiuchumi Donbas, hatua ambayo ingewataka Waukraine kuondoka katika baadhi ya maeneo wanayoyadhibiti.
Aidha, Zelensky amekiri kuwa bado kuna tofauti kubwa za mitazamo kati ya pande zinazohusika kuhusu mustakabali wa eneo hilo, ambapo Russia kwa sasa inadhibiti sehemu kubwa ya Donbas na inaitaka Ukraine kukabidhi eneo lote, jambo ambalo Kyiv imekataa.
Pamoja na hatua hizo, mazungumzo juu ya mustakabali wa eneo hilo yanaendelea, hata hivyo pengo kati ya msimamo wa Russia na Ukraine bado ni kubwa hali inayoonesha wasiwasi wa kufikiwa muafaka wa haraka katika kumaliza mzozo huo.
