BODI ya Ligi Zanzibar, imeitoza faini ya Sh1 milioni Black Sailors inayoshiriki Ligi Daraja la kwanza Zanzibar kwa kosa la mashabiki wa timu hiyo kufanya vurugu baada ya kumalizika kwa mechi.
Adhabu hiyo imetolewa na Kamati ya Uendeshaji na Usimamizi wa Bodi ya Ligi katika kikao chake kilichofanyika Desemba 3, 2025, ilipopitia mwenendo na matukio mbalimbali ya Ligi Daraja la Kwanza ikiwemo mchezo namba 78 kati ya Kundemba na Black Sailors uliochezwa Desemba Mosi, 2025 kwenye Uwanja wa Mao A, saa 10 jioni.
Katika taarifa iliyotolewa na Ofisa Habari wa ZBL, Issa Chiwile, kamati hiyo imebaini katika mechi hiyo hiyo kulitokea vurugu baada ya dakika tisini kukamilika zilizofanywa na mashabiki wa Black Sailors wakiongozwa na Hassan Issa ‘Nakuna’, kitendo ambacho ni kosa kisheria chini ya sura ya 20 kanuni ya mashindano ya 2025-2026.
“Timu ya Black Sailors imetozwa faini ya Sh1 millioni kwa makosa ya wapenzi na mashabiki wa timu hiyo kufanya vurugu na ghasia baada ya kumalizika kwa mchezo. Adhabu hii imetolewa chini ya SURA ya 20 (1), (2) na (3) (ii) za kanuni ya mashindano 2025-2026,” imesema taarifa hiyo.
Mbali na faini hiyo, pia Kocha wa Makipa wa Black Sailors, Rashid Ghilman amefungiwa kukaa kwenye benchi la ufundi kwa michezo mitano mfululizo.
Kwa upande mwingine, Mashabiki wa timu hiyo akiwamo Nakuna, Juma Ramadhan ‘Kijuma’ na Murtala Maulid, wamefungiwa kujihusisha na mpira wa miguu ikiwamo kuhudhuria viwanjani kutizama michezo itakayoandaliwa na Shirikisho la Mpira wa Miguu Zanzibar (ZFF) kwa muda wa miaka miwili, huku shabiki mwingine Awadh Juma akipewa onyo kwa kosa la kutoa lugha zizisofaa wakati wa vurugu hizo.
